in , , ,

Super Sunday kicheko Manchester United

*Liverpool bado, Arsenal, Man City nguvu sawa

*Andre Villas-Boas acheka, Newcastle pia safi

Manchester United wamefanikiwa kuvuna pointi tatu kwa Liverpool, huku Arsenal wakitoka sare na Manchester City.
Mashetani Wekundu walionekana kuzidiwa nguvu tangu mwanzo, na kocha wao Sir Alex Ferguson amekiri ubutu katika mchezo, lakini walipata mabao 2-1 Anfield.
Bao la penati katika dakika za mwisho liliizamisha Liverpool iliyocheza kwa kujituma na kwa kasi tangu mwanzo, hata kumiliki mpira kuliko wapinzani wao.
Pengine kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa Jonjo Shelvey kipindi cha kwanza kwa mchezo wa rafu kumewagharimu The Reds.
Machungu ya Liverpool yameendelea wakati wakikumbuka vifo vya washabiki wao 96 vilivyotokea Aprili 1989 katika uwanja wa Hillsborough uliopo
Sheffield, Uingereza.
Familia za waathirika zilikuwa uwanjani, maua yakatolewa na maputo kurushwa kwa heshima yao, hisia zikawa kali uwanjani, kabla ya mchezo kuanza.
Hata hivyo, kocha Rodgers anaona kwamba mwamuzi Mark Halsey alichangia kushindwa kwao, kwa kumtoa nje Jonjo, akihoji kwa nini Jonny Evans wa United naye hakupewa kadi nyekundu, wakati rafu waliyocheza ni ile ile.
Alikuwa nahodha Steven Gerrard aliyeandika bao la kwanza muda mfupi baada ya mapumziko, na kuweka hai ndoto za kocha Brendan Rodgers kupata ushindi wa kwanza msimu huu.
Lakini Rafael aliweka rehani ndoto hizo kwa kusawazisha bao hilo dakika chache baadaye, huku Robin van Persie akitia lakiri ushindi kwa mkwaju wa penati ambao nusura Pepe Reina audake.
Kama vile kuna tatizo jijini Manchester, upande wa pili Roberto Mancini amewalalamikia vijana wake wa Man City kwa mchezo legelege, kutotumia vyema nafasi za kufunga na kuruhusu bao lao la mapema kurudishwa mwishoni.
Arsenal ya Arsene Wenger waliingia Etihad kwa kujiamini, lakini wakicheza kwa utaratibu kuusoma mchezo, kabla ya beki Joleon Lescot kupachika bao la kichwa kutokana na kona.
Arsenal walitawala zaidi mchezo mzima, kiungo cha Santi Cazorla, Aaron Ramsey na Abou Diaby kikiwa imara, lakini kigugumizi kilikuwa kwenye wamaliziaji.
Alikuwa Laurent Koscielny, beki aliyeshika nafasi ya Thomas Vermaelen, aliyempeleka wavuni Joe Hart kuokota mpira baada ya mkwaju wake mkali wa karibu wa kushitukiza.
City walikosa aina ya uchezaji waliozoeleka nao mwishoni mwa msimu uliopita – kumiliki mpira na kushambulia kwa kasi, na sasa Mancini anasema wanatakiwa waache kutambia ubingwa, wajenge timu.
Manchester City wameshinda mechi mbili tu kati ya tano msimu huu, na kila moja wamekuwa wakipachikwa walau bao moja.
Arsenal wameshinda mbili na kutoka sare tatu, wakiwa wamefungwa mabao mawili tu hadi sasa, machache kuliko timu zote za Ligi Kuu ya England mwaka huu.
Kwa upande mwingine, Ande Villas-Boas alikuwa mwenye furaha baada ya mechi ya timu yake, Tottenham Hotspur iliyoifunga Queen Park Rangers (QPR) bao 2-1.
Huu ulikuwa ushindi wa kwanza nyumbani White Hart Lane kwa Spurs, uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu, na umemuepusha Villas-Boas kuzomewa.
QPR walitangulia kupata bao kupitia kwa Bobby Zamora aliyekuwa Spurs kabla, jambo lililosababisha kocha kubadili mfumo wa kucheza.
Matunda yalionekana, baada ya shinikizo kuwazidi QPR kiasi cha kujifunga wenyewe kupitia kwa Alejandro Faurlin, kisha mchezaji wa kimataifa wa England, Jermain Defoe kufunga dakika mbili baadaye.
Nao Newcastle wakicheza nyumbani, walifanikiwa kuwachapa Norwich City bao 1-0, na kumharibia kocha Chris Hughton aliyekuwa akirejea Newcastle akitarajia ushindi au walau sare.
Bao la Newcastle lilifungwa na Demba Ba, likiwa ni bao la tatu katika mechi mbili. Papiss Cisse alikosa penati kipindi cha kwanza.
Norwich imebaki bila kushinda hata mechi moja kati ya tano ilizocheza hadi sasa.
Kwa matokeo ya mechi za Jumamosi na Jumapili, Chelsea wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 13, wakifuatiwa na Man United wenye pointi 12. Everton na West Bromwich Albion zinafuata zikiwa na pointi 10 kila moja, huku Arsenal ikishika nafasi ya tano kwa pointi zake tisa.
Timu nyingine zenye pointi tisa zinazofuata nyuma ya Washika Bunduki wa London ni Fulham na Manchester City.
Tottenham inafuatia na West Ham United na Newcastle, zote zikiwa na point inane.
Swansea ni ya 11 kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na timu nne zenye pointi nne kila moja. Hizo ni Sunderland, Stoke City, Astona Villa na Wigan Athletic.
Southampton iliyozinduka Jumamosi na kushinda inashika nafasi ya 16 kwa pointi zake tatu sawa na za Norwich.
Liverpool na QPR zina pointi mbili kila moja, na zinashika nafasi ya 18 na 19 kwa mtiririko huo, huku mkia ukishikwa na Reading yenye pointi moja tu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Chelsea wagomea kileleni

Terry abwaga manyanga England