in , , ,

Sunderland hoi England, hai Afrika

LAITI tamaa au matarajio yangekuwa na jedwali la msimamo, basi klabu iliyo Ligi Kuu ya England (EPL), Sunderland wangekuwa juu.

Dimbani Sunderland wapo hoi, wakichukuliwa moja ya timu ndogo ambao kwa misimu kadhaa wamekuwa wakiepuka katika tundu la sindano kushuka daraja.

Lakini barani Afrika ni klabu tofauti kabisa, wakijitanua kimtandao na kibiashara na pia wakijengea uwezo chipukizi kwa mikakati ya kisoka, ikiwa ni pamoja na nchini Tanzania.

Hata msimu huu, Sunderland wanajaribu kukiepuka kikombe cha kushuka daraja England, wamemfuta kazi kocha Gus Poyet na kumpa kazi ya mechi tisa mkongwe Dick Advocaat kuhakikisha hawashuki daraja.

Sunderland wanafanikiwa zaidi nje ya dimba, na tangu 2012 walianzisha mawasiliano na Afrika kupitia moja ya kampuni ya mafuta iliyoanza kudhamini klabu hiyo.

Sunderland wanaokwenda kwa jina la utani la ‘Black Cats’ wametokea kuwa na washabiki Afrika kutokana na jezi zao zilivyoandikwa ‘Invest in Africa’, yaani ‘Wekeza Afrika’, na hii iliwapa nguvu kuingia barani kwa nguvu.

“Tuna misingi mitatu muhimu ya kazi ambayo ni soka, biashara na operesheni za jamii. Tupo Tanzania, Afrika Kusini na Ghana na tunatarajia kufanya kazi walau kwenye nchi nyingine moja barani Afrika mwaka huu,” anasema Hutchinson.

Sunderland pia ni mshirika wa utalii na Tanzania, ambapo katika dimba lake – Stadium of Light linalochukua washabiki 49,000 kuna mabango yanayoshawishi watu watalii Tanzania.
“Tunakuza utalii wa Tanzania kupitia ule umaarufu wa Ligi Kuu ya England kuwafikia watu bilioni 4.2 wanaofuatilia ligi hii maarufu zaidi duniani.

“Klabu inatumia chombo hiki kikubwa cha masoko cha Premier League kuikuza Tanzania, kuonesha watu kwamba ni mahali pa kutembelea.
“Tunaendesha mashindano kwa ajili ya kuwafanya washabiki wetu wabaini kwamba kuna maajabu nchini Tanzania na kuwashawishi wakatembelee,” anasema mkurugenzi huyo.

Wamejipanga kuungana na klabu kubwa za England ambazo pengine zimekuwa na washabiki wengi kwa muda sasa, kutokana na mageuzi ya soka ya England, yakizitenga kama tano au sita kuwa bora mara kwa mara kwenye msimamo wa ligi.

“Tamaa yetu ni kuwa klabu inayojulikana na kuheshimika. Wengi wanashabikia Manchester United, Arsenal, Liverpool na Chelsea na baada ya hapo tunakuja sie wengine, sasa tunataka baada ya hao tuwe sie Sunderland,” anasema Mkurugenzi wa Biashara wa Sunderland, Gary Hutchinson.

Klabu hii imeweka mikakati makini kufikia soko kupitia biashara na viungo vya jamii na wanajivuna kwamba wamepata wachezaji Waafrika waliocheza kwa mafanikio.

Waafrika waliocheza Sunderland ni pamoja na wachezaji wa Ghana, Nahodha wa Tomu ya Taifa, Asamoah Gyan, John Mensah na Sulley Muntari. Yupo pia mshambuliaji kutoka Benin, Stephane Sessegnon.

Mdhamini wa Sunderland yupo Johannesburg, Afrika Kusini ambapo pia wana mkataba na klabu ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini ya Bidvest Wits na wana makubaliano na wakfu ya Nelson Mandela.

Nchini Ghana pia Sunderland wanakuza vipaji wakiwa na klabu yenye makazi yake jijini Kumasi, Asante Kotoko.

Kwa klabu nyingine nyingi za soka, hulithamini Bara la Afrika tu pale wanapoweza kutengeneza fedha au kupata mchezaji mzuri na kumnyakua.

Sunderland wana falsafa tofauti, ambapo Mkuu wa Uendelezaji wa Soka ya Kimataifa wa Sunderland, Graham Robinson anasema ni ngumu sana kupeleka wachezaji Uingereza na Ulaya.

“Mpango wetu ni kuendeleza wachezaji ili wawe na kiwango cha juu na wacheze Afrika na kukuza soka maana kwenda Ulaya ni mmoja au wawili tu wanafuzu na maelfu watabaki Afrika.

“Tunataka wawe mahiri katika kila idara na wafuzu kucheza soka ya juu Afrika maana nako soko ni kubwa,” anasema Robinson ambaye pia anatoka Afrika Kusini.

Sehemu ya mkakati wa Sunderland ni kwa wanasoka na makocha wa Afrika kwenda klabuni Sunderland na kujifunza jinsi wenyewe Sunderland wanavyofanya kazi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Tetesi za usajili majuu…

Bale, Kane watakiwa Man United