in , , ,

Suarez kuwashitaki Liverpool

*Gareth Bale hayupo msafara wa spurs
*Clint Dempsey aamua kurudi Marekani

 

Mpachika mabao Luis Suarez anafikiria kuchukua hatua za kisheria, kuwashinikiza Liverpool kumwachia ajiunge na Arsenal.
Raia huyo wa Uruguay amesema anataka kuwasilisha rasmi kusudio la kuondoka Anfield, na ikishindikana atakwenda mahakamani, ikiwa mzozo wake hautapatiwa ufumbuzi mapema.
Suarez (26) anaamini kwamba dau la Arsenal la pauni milioni 40 na pauni moja, ni tosha kutengua kifungu cha mkataba wake, hivyo kumuweka huru kuhama.
Liverpool wanadai sivyo, kwamba tafsiri yake ni kwamba ikiwa patakuwa na dau linalozidi pauni milioni 40, mchezaji huyo anatakiwa kuarifiwa tu, lakini si ruksa kuhama, kwani baada ya hapo klabu itatathmini kiasi cha fedha wanachotaka kwa mauzo yake.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ameweka wazi nia yake ya kumpata Suarez, lakini akasema yupo tayari kwa mazungumzo ili kufikia mwafaka, lakini kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers anasisitiza kwamba mshambuliaji huyo hawezi kuuzwa pungufu ya pauni milioni 50, japokuwa hangependa kumuuza kwa sasa.
“Tunataka kumsajili Suarez kama inawezekana, tunaheshimu kile Liverpool wanchotaka kufanya, hivyo sipendi sana kuzungumzia masuala ya Suarez, maana yanahusu Arsenal na Liverpool. Naamini kwamba tunaweza kufanya suala hili faragha kwa kadiri tunavyoweza, jambo ambalo ni gumu katika dunia ya sasa,” akasema Wenger.
Mfaransa huyo anasema kwamba bado muda wa usajili ni mrefu, na kwamba ukiacha Manchester City, klabu nyingi hazijaweza kufanya chochote, bali Arsenal wanafanya kazi kwa bidii sana kuimarisha kikosi chao.

GARETH BALE HAYUPO NA SPURS

20130730-091832.jpg

Nyota wa Tottenham Hotspurs, Gareth Bale hajaandamana na klabu yake katika safari ya mechi baina yao na Monaco ya Ufaransa.
Licha ya kwamba kutokuwapo kwake kunaongeza hisia juu ya uwezekano wa kuhamia Real Madrid wanaomsaka kwa udi na uvumba, Bale anauguza majeraha madogo ya mguu.
Bale (24) ameeleza wazi nia yake ya kukubali mwito wa kwenda kuchezea miamba hao wa Hispania, lakini si kocha wake, Andre Villas-Boas wala mwenyekiti Daniel Levy walio tayari kumwacha aende, wakitafuta kila njia kumbakisha White Hart Lane.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, amedokeza kwamba alipokuwa Madrid alijaribu kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales, lakini haikuwezekana.
“Nadhani safari hii mambo yatakamilika, kwa hiyo nafurahi kwamba watapata mchezaji mahiri kabisa, wakati umefika, kijana huyo anatakiwa kwenda sasa, ana thamani kubwa,” akasema Mourinho.
Mrithi wa Mreno huyo katika dimba la Santiago Bernabeu, Carlo Ancelotti, amesema kwamba wanafanyia kazi uhamisho wa Bale, na kwamba mazungumzo yanaendelea.

CLINT DEMPSEY KURUDI MAREKANI

Mshambuliaji wa Spurs, Clint Dempsey ameamua kuihama klabu hiyo na kujiunga na Seattle Sounders ya nyumbani kwake, Marekani.
Dempsey (30) alijiunga na Spurs msimu uliopita wa kiangazi kutoka Fulham ya London pia, kwa dau la uhamisho la pauni milioni sita, dau analotarajiwa pia kuhamishwa nalo.
Dempsey alifunga mabao 12 katika mechi 43 alizochezea Spurs msimu uliopita. Spurs hawana kikwazo, kwa sababu tayari wamefikia makubaliano ya kumsajili mpachika mabao kutoka Valencia, Roberto Soldado.
Dempsey amelichezea taifa lake Marekani katika mechi 99, ambapo alihama klabu ya Kimarekani ya New England Revolution kujiunga na Fulham mwaka 2007.
Amefunga jumla ya mabao 50 katika mechi 184 za Fulham, kabla ya Spurs kuwazidi kete Liverpool na Aston Villa hadi kumsajili, japokuwa kocha wa Fulham, Martin Jol hakutaka kumwachia.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Mtanzania bingwa kuruka kamba

TENGA AMSHUKURU MSAJILI KWA KUSAJILI KATIBA YA TFF