in , , , ,

STARS YASHINDWA KUTAMBA NYUMBANI

0-0

Taifa Stars imelazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Nigeria jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam kwenye mchezo wa Kundi G wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017.

Kwenye mchezo huo Stars ilionyesha kiwango kilichopitiliza ila tu ikashindwa kuzitumia nafasi ilizotengeneza.

Kwa upande wa Nigeria hawakuweza kutengeneza nafasi yoyote ya wazi kwenye dakika zote za mchezo. Mtetezi wao alikuwa golikipa Carl Ikeme aliyeokoa michomo kadhaa ya washambuliaji wa Stars na kuufanya mchezo ubaki bila mabao.

Kikosi cha Taifa Stars kilionyesha kujiamini tangu dakika za mwanzoni za mchezo. Ni Thomas Ulimwengu aliyesumbua mno ngome ya Nigeria kupitia upande wa kulia kwenye dakika za mwanzo.

Mapema kwenye dakika ya 3 Ulimwengu alijaribu kumpita Kingsley Madu lakini mlinzi huyo wa Nigeria akamchezea madhambi na Stars wakatunukiwa Mpira wa adhabu ambao haukuweza kuzaa matunda yoyote.

Timu ziliendelea kushabuliana kwa zamu lakini Stars walionekana kuutawala mchezo zaidi. Kwenye dakika ya 21  Mrisho Ngassa alitishia kumpita Kenneth Omeruo lakini mlinzi huyo alimchezea madhambi na mwamuzi akaamuru mpira wa adhabu upigwe.

Mbwana Samatta alipiga mpira ule wa adhabu kwenye dakika ya 22. Shuti lake kali lililokuwa likielekea wavuni lilipanguliwa na golikipa Ikeme.

advertisement
Advertisement

Stars waliendeleza makali yao kwa kutawala eneo la kiungo kupitia Himid Mao na Mudathir Yahya. Hili likapelekea mwalimu Sunday Oliseh kufanya mabadiliko ya mapema kwenye dakika ya 36. Alimtoa kiungo Lukman Haruna na kumuingiza Sylvestre Igboun.

Kadri kipindi cha mapumziko kilipokaribia makali ya Stars yakapungua na Nigeria wakafanikiwa kuutawala mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa. Nafasi yao nzuri zaidi ilikuja kwenye dakika ya 38 ya mchezo. Moses Simon alipokea krosi ya chini  kutoka kwa Ahmed Musa lakini shuti lake likapanguliwa na golikipa Ali Mustafa.

Kipindi cha kwanza kikamalizika milango yote ikiwa migumu. Kwenye kipindi cha pili cha mchezo Taifa Stars ilirejea ikiwa na makali zaidi.  Nafasi ya wazi kuliko zote ilikuja kwenye dakika ya 64. Mrisho Ngassa alikutana na krosi nzuri akiwa peke yake ndani ya eneo la hatari lakini akapiga kichwa kilichopaa juu ya lango.

Stars waliendelea kuonyesha ubora. Punde baada ya kuingia Said Ndemla alimtengenezea Ulimwengu nafasi nzuri ya kufunga. Shuti zuri la chini la Ulimwengu likazuiliwa na Ikeme kwa mara nyingine.

Mchezo uliendelea kutawaliwa na Stars lakini nafasi walizotengeneza hazikuweza kuzaa mabao na mchezo ukaisha bila mabao.

Kwa matokeo haya Nigeria wanakuwa vinara wa kundi hili wakiwa na alama 4. Misri ambao watacheza mchezo wao hapo kesho dhidi ya Chad wanakuwa kwenye nafasi ya pili wakiwa na alama 3. Stars inajikita kwenye nafasi ya tatu ikiwa na alama 1 na Chad wanaburuza mkia wakiwa na alama sifuri.

Picha kwa hisani ya http://salehjembe.blogspot.co.uk/

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ujerumani wawapopoa Poland

Tanzania Sports

Drogba apiga hat-trick