in , ,

Spurs kumpoteza Gareth Bale?


*Real Madrid, Man U waandaa dau
*Mwenyewe adaiwa kuanza kuaga

Licha ya Tottenham Hotspur kusisitiza nyota wao, Gareth Bale atabaki klabuni, inadaiwa anajiandaa kujiunga Real Madrid.
Vyombo vya habari vya Hispania vimeripoti kwamba mchezaji huyo raia wa Wales ameshakata shauri la kuhama, na kwamba huenda akatua Madrid.
Taarifa hiyo inakuja saa chache tu baada ya Kocha wa Spurs, Mreno Andre Villas-Boas kudai kwamba kutokana na ukimya anaouona, anachukulia kwamba watabaki naye msimu ujao.
Bale alikuwa na makali yasiyo ya kawaida msimu uliopita, ambapo ni kama vile aliibeba timu hiyo iliyokaribia kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini wakaadhibiwa na jirani zao wa London Kaskazini, Arsenal.
Pamoja na Real Madrid, inasemekana Manchester United nao wanajiandaa kupeleka dau lao kwa Spurs kwa ajili ya mchezaji huyo mwenye ufundi wa aina yake kufunga mipira ya adhabu ndogo.
Manchester United wanadaiwa kuandaa dau la pauni milioni 60, wakati huu ambapo maombi yao ya kumsajili Cesc Fabregas wa Barcelona yamegonga mwamba mara mbili. Hata hivyo, inadaiwa kwamba nahodha huyo wa zamani wa Arsenal anafikiria upya maisha yake Camp Nou, ikizingatiwa kwamba hapati namba kirahisi katika kikosi cha kwanza.
Gazeti la Marca la Hispania, linadai kwamba Bale atajiunga Real Madrid wanaonolewa na Carlo Ancelotti kwa pauni milioni 85, na kwamba atasaini mkataba wa miaka sita.
Iwapo kweli ataondoka, litakuwa pigo kubwa kwa Villas-Boas na Spurs kwa ujumla, kwa sababu kikosi chao kitakuwa na upungufu, hata kama wamesaini na watasaini viungo na wapachika mabao wapya.
Inadaiwa Bale ameshawaambia wakuu klabuni kwake kwamba anataka kuondoka msimu huu wa kiangazi, na huko Hispania inaelezwa kwamba atapata mshahara wa pauni milioni 8.5 hivi kwa mwaka, baada ya wakala wake, Jonathan Barnett kukutana na wawakilishi wa Real Madrid.
“Nataka kurudia kile ambachom nimekuwa nawaambia msimu uliopita, na mwanzo wa maandalizi ya msimu huu.
“Bale ni mchezaji tuliyedhamiria kubaki naye, ni mchezaji wa Tottenham, ni mmoja wa wachezaji mashuhuri zaidi duniani na tunaendelea kumchukulia kama mmoja wetu kwa wakati ujao,” Villas-Boas akasema.
Bale ameumia kidogo mazoezini, kwa hiyo hatarajiwi kucheza kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Sunderland, lakini kocha huyo anasema atacheza mechi itakayofuata.
Gazeti jingine la Hispania, El Confidencial linasema kwamba shinikizo la sasa la Real Madrid kumtaka Bale linatoka kwa kocha Ancelotti.
Bale alifunga mabao 21 katika mechi 34 za Ligi Kuu ya Uingereza msimu uliopita.
Makali ya Bale yalionekana baada ya Spurs kumchukua Villas-Boas baada ya kumfukuza kazi Harry Redknapp ambaye sasa anawafundisha Queen Park Rangers walioshuka daraja. Bale mwenyewe anasema mafanikio yake yametokana na kufundishwa vyema na Mreno huyo.
Kwa ubora alio nao, wengi wanalitaja jina lake likiwa la tatu kwa ubora baada ya Lionel Messi wa Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arsenal wawatega Liverpool

Bado tuna ushamba kwenye soka!