in , , ,

YA GAMBIA YALIKUWA FUNZO LA KWENDA GABON NA INDIA.

Mwaka 2005 ulikuwa mwaka mchungu kwenye tasnia ya mpira hapa Tanzania.

Nuru hafifu iliyoanza kujipenyeza taratibu kwenye mboni ya macho yetu
ilifunikwa na wingu zito giza likatanda machoni mwetu.

Furaha ya muda tuliyoipata ilipotea ghafla, vilio na majonzi
yaliyatawala kwenye ukoo wetu wa soka.

Ukoo ambao ni maskini wa kutupwa, ukoo ambao hauna mafanikio ya
kujivunia, ukoo ambao tajiri mkubwa ni mwenye malapa tena ya rangi
mbili tofauti yalitoboka chini. Huyu ndiye tajiri mkubwa wa kujivunia
kwenye ukoo wetu kutokana na hiki anachomiliki.

Ukoo ambao umekuwa ukiyaota mafanikio bila ya kuamka na kuyatafuta
mafanikio kwa nguvu, ubunifu na nidhamu kubwa .Na hii ni kwa sababu
Chief waliopitia kuongoza ukoo huu hakuna aliyewahi kuwa na hasira za
dhati kuhusu kuondoa umasikini wa ukoo wetu.

Nuru ya utajiri ilijaribu kujipenyeza mwaka 2005 lakini kauli ya
ng’ombe wa masikini hazai ilijidhirisha kwenye kikosi chetu cha
Serengeti boys cha Mwaka 2005.Tukiwa tayari tumefuzu kucheza Afcon ya
vijana chini ya umri wa miaka 17 na kupangwa na Nigeria, Ivorycost na
Afrika Kusini.

Januari 28, 2005 CAF ikaiondoa Tanzania kwenye fainali hizo kwa
kumchezesha Nurdin Bakari dhidi ya Rwanda na Zambia kutokana na
kudanganya umri.

TFF ilieleza kwenye taarifa za wachezaji kwamba Nurdin alizaliwa mwaka
1988, lakini katika orodha iliyotumwa CAF na klabu yake ya Simba
kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa, ilionyesha kwamba mchezaji huyo
alizaliwa mwaka 1983!

Kwa maana hiyo ukijeba wa Nurdin ukaikosesha Tanzania kushiriki
fainali na nafasi yake ikachukuliwa na Zimbabwe ambayo hata hivyo
iligeuka kuwa daraja la timu nyingine.

Serengeti Boys inakumbuka pia ilivyozikosa fainali za mwaka 2013 kule
Morocco baada ya Congo-Brazzaville kuwafungashia virago katika raundi
ya pili.

Mapito haya yote yanaonesha ni lini ilitakiwa kuwa siku yetu na ni
wapi tulitakiwa kwenda pindi siku hiyo itakapowadia.

Siyo ndoto tena, muda huu tumeshapata mwanga wa kututoa katika giza
nene lililotawala katika mboni zetu.

Muda mwingi tumekuwa tukijifuta machozi yetu kwa leso ya vumbi.
Tumekuwa wazuri wa kujiongezea kilio sisi wenyewe.

Safari hii umakini unahitajika Sana, tunahitaji kuifua ipasavyo leso
yetu yenye vumbi ili tujifute machozi bila kutokwa machozi.

Kwenda Gabon isiwe ndiyo mwisho wa furaha yetu, viongozi, wachezaji na
makocha wa Serengeti boys wanatakiwa wajue kuna kwenda India kwenye
kombe la duniani la vijana waliochini ya umri wa miaka 17 baada ya
hapa kama watafanikiwa kuingia nusu fainali hii.

Ni nafasi nzuri kwa wachezaji kujituma ili wajiuze, wengi walipitia
michuano hii ya vijana mpaka wakawa wachezaji wakubwa.

Na ni wakati sahihi kwa TFF kukilea hiki kikosi kwa ajili ya timu ya
taifa ijayo. Sisi watanzania Kwa ujumla tumechoka kufutwa machozi kwa
leso ya vumbi..

Ni wakati sahihi kwa vijana kujenga historia yao ambayo dunia haitowasahau.

Sisi Watanzania hatutoisahau Serengeti boys ya kina Nurdin Bakari kwa
sababu ilifuzu michuano ya soka la vijana Africa lakini ikapokonywa
nafasi. Sisi Watanzania hatutoisahau pia Serengeti boys hii kwa Sababu
imefanikiwa kwenda Gabon.

Kwenda Gabon haitoshi, wanatakiwa waipe sababu dunia ya kutowasahau
katika kumbukumbu za wanadunia.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NI MARA CHACHE KUSHUHUDIA USIKU USIO NA GIZA KAMA USIKU WA NOU CAMP

MS

TUWE MAKINI NA VIPIMO VYA NDIMI ZETU KWA SAMATTA