Organisations & Sports Bodies

TOC

KAMATI YA OLIMPIKI TANZANIA – TOC

Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ilirithi shughuli zote za Commonwealth Games Association iliyoanza rasmi kazi zake hapa nchini mwaka 1957.

Kamati ya Olimpiki Tanzania ni miongoni mwa taasisi chache nchini za michezo  zenye sura halisi ya Muungano.

Taasisi hiyo ya TOC ina wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano. Kamati hiyo hivi sasa ipo chini ya uenyekiti wa ndugu Gulam Abdulla toka Zanzibar. Katibu Mkuu ni ndugu Filbert Bayi.

Ndugu Bayi ni miongoni mwa wanariadha walioiletea sifa nchi yetu, baada ya kupata medali kule Lagos, Nigeria katika Michezo ya Afrika mwaka 1973.

Kadhalika katika  Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Christchurch, New Zealand mwaka 1974 na Michezo ya Olimpiki ya Moscow, Urusi ya mwaka 1980.

Ni zaidi ya miaka 32 leo Tanzania haijaweza kupata medali yoyote katika michezo ya Olimpiki, licha ya kushiriki mashindano hayo mara kadhaa.

Kuna baadhi ya wachambuzi wa michezo wanadai kuwa Tanzania ina nafasi finyu sana kupata medali yoyote katika michezo hiyo iwapo hali itaendelea ilivyo.

Baadhi wanadiriki hata kusema kuwa medali za Moscow (ikiwamo na ya Suleiman Nyambui) zilikuwa ni bahati, kutokana na ukweli kuwa nchi nyingi za magharibi zilisusia toshiriki michezo hiyo kutokana na sera za Warusi kuivamia nchi ya Afganiastan wakati ule.

Tanzania ilikuwa na timu kubwa sana iliyokwenda Urusi mwaka 1980. Pamoja na riadha, ndondi, mpira wa meza na kuogelea, Tanzania pia ilipeleka timu ya mpira wa magongo, yaani hockey.

Takribani wanamichezo 100 walishiriki michezo hiyo. Sina hakika lini tena tutaweza kupeleka timu kubwa kama hiyo, ikitiliwa maanani kushiriki kwetu hivi sasa kutategemea sana kufikia viwango vilivyowekwa  na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC)  kwa kushirikiana na vyama husika vya kimataifa.

Kamati ya Olimpiki Tanzania ni miongoni mwa vyama vichache nchini vinavyopata ruzuku ya kutosha kutoka IOC.

Shughuli nyingi za chama hicho, ikiwa ni pamoja na gharama za kodi ya pango, mishahara ya wafanyakazi, safari za nje kwa mwenyekiti na katibu mkuu hugharamiwa na IOC.

Pamoja na malalamiko mengi ya wadau wa michezo nchini kwa TOC, bado kamati inastahili pongezi kwa mafunzo mbalimbali ya utawala kwa vyama vyote vya michezo nchini.

Kamati hiyo imeweza kufundisha wataalamu mbalimbali, ikiwa pamoja na kupeleka nje walimu wa michezo mbalimbali.

Kamati pia imeweza kupata jengo lake la kudumu  kule Dole, Zanzibar – Olympic Africa.

Kituo hicho kinatumika kwa shughuli mbalimbali, ikiwa pamoja na kuendesha mafunzo.

Kamati imepanga kuendesha mkutano mkuu wa uchaguzi Desemba mwaka huu, hivyo inatarajiwa mabadiliko makubwa ili kuongeza ufanisi wa kamati hiyo.

NINI KIFANYIKE

Pamoja na kuhitaji mabadiliko makubwa katika mfumo mzima wa kamati hiyo – TOC – bado kunahitajika watu wenye uzoefu na uelewa mpana zaidi katika shughuli za Olimpiki duniani.

Licha ya uzoefu na uelewa, bado panahitajika weledi na uaminifu wa kweli katika kuongoza kamati hiyo.

Kutokana na fedha nyingi inazopatiwa Kamati ya Olimpiki Tanzania, ingekuwa vyema pia kuwepo mipango endelevu katika usimamizi mzuri wa kupata wanamichezo bora watakaoshiriki michezo ya Olimpiki.

Kazi hiyo nyeti ifanywe kwa uangalifu kwa kushirikiana na vyama kwa kipindi cha miaka minne na si mwezi mmoja kama ilivyo sasa. Tanzania inaweza kuwa na timu nyingi bora.