in

Siri ya Uingereza kufanya vizuri Olimpiki

MWISHO wa Michezo ya 30 ya Olimpiki iliyofayika London, Uingereza, ndio mwanzo wa michezo ya 31 itakayofanyika Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2016.

Kati ya mambo yaliyojitokeza kwenye michezo ya mwaka huu, ni wenyeji kutumia vyema rasilimali zao na kufikia kilele cha mafanikio ya miaka 104.
Ni kweli kwamba Marekani na China zimefanya vizuri kwa wingi wa medali kwa ujumla, zikiwamo za dhahabu.
Ni kweli pia Michael Phelps wa Marekani ametangazwa kuwa mwanamichezo mahiri zaidi wa muda wote katika Olimpiki kwa wingi wa medali zake za dhahabu.
Lakini kama kuna la kujifunza katika mageuzi ya michezo kwa nchi kwa ujumla, na ufanisi wa mchezo mmoja hadi mwingine, Uingereza ni somo tosha.
Fahari ya taifa hili kwa maandalizi mazuri, sherehe bora za ufunguzi na murua za ufungaji michezo ni heshima yao kama waandaaji.
Mchezoni, wanamichezo wake wengi hawakuwa na ajizi. Walitumia vyema mafunzo ya makocha na jitihada binafsi katika vitendo, wakapata medali.
Kocha na Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chama cha Mbio za Baiskeli Uingereza, David Brailsford, ambaye pia ni kocha wa timu hiyo, amepata mafanikio makubwa.
Katika Olimpiki hii ameshuhudia medali 12, nane kati ya hizo zikiwa za dhahabu. Ni huyu pia aliyechochea ushindi wa Bardley Wiggins katika mashindano ya Tour de France, akiwa meneja mkuu wa Team Sky.
Daima timu au mchezaji anapofika kileleni changamoto zinazowakabili huongezeka, maana wanakuwa wameshajiwekea kipimo cha juu kisichotakiwa kushuka tena.
Wakati mawazo na mipango ya wadau vikielekea Rio, Uingereza na timu yake – Team GB, wana mtihani wa kushikilia kiwango chao au kukipandisha juu tayari kwa michezo ijayo nchini Brazil.
Tayari matumaini yamekuzwa katika michezo hii, ambapo nchi imevuna medali medali 65. Wana dhahabu 29, fedha 17 na shaba 19. Haijapata kutokea tangu mwaka 1908.
Tayari wanamichezo wengine wanaangalia jinsi ya kufuata nyayo za hao wa mbio za baiskeli na wapiga makasia waliokusanyia nchi medali tisa, zikiwamo nne za dhahabu.
Mwalimu Brailsford anasema Uingereza inatakiwa kukaza kamba kwa kuhakikisha hawapotezi kanuni walizotumia kufikia hesabu nzuri ya jumla iliyowaweka juu kiasi hicho – nafasi ya tatu kwa ujumla.
“Mambo yamekwenda vizuri, ugharimiaji umeleta tofauti kubwa katika jinsi nchi ilivyofanya vizuri kwenye michezo. Inaendeshwa na kusimamiwa vizuri. Inafanya kazi.
“Kinachonitatiza kidogo ni hili suala la kutaka kubadilisha mfumo. Wanakuja watu wanataka kuanza mambo upya kwa mawazo tofauti katika kila kitu,” anasema.
Maoni yake ni kwamba njia ambazo Uingereza imeanza kufuata zinatakiwa kuenziwa. Hataki kuona wanasiasa wakiingilia kuelekeza cha kufanya, wakati tayari mafanikio yameanza kuonekana.
Badala yake, anaona dalili za mafanikio zaidi zitatokana na vyama vya michezo tofauti kushindana katika kila kimoja kujaribu kuongoza michezo kisomi.
“Kwa kifupi ni kwamba mfumo huu unafanya kazi, tusipouingilia na kuuvuruga, utaendelea kufanya kazi.
“Huwezi kuwekeza kwenye michezo kama tunavyofanya uache kufanikiwa…mbaya ni kugutuka na kufanya mabadiliko yasiyo na msingi. Kwa hiyo wanasiasa kaeni mbali, elekezeni fedh kwenye michezo, ziende kwa wakurugenzi,” anasisitiza.
Kwa watakaosikiliza ushauri bila shaka wataona mafanikio, kama aliyowezesha Brailsford kwenye Michezo ya 30 ya Olimpiki.
Michezo hiyo ya London 2012 ilianza kwa sherehe ya ufunguzi. Mashujaa saba wa Olimpiki wa Uingereza wa miaka iliyopita walikabidhi mienge yao kwa kizazi kingine –wanamichezo chipukizi saba  wanaotabiriwa kuwa nyota siku zijazo.
Baada ya hapo waliwasha moto kwenye Mwenge mkubwa katika Uwanja wa Olimpiki.
 Mmoja wa chipukizi hao alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 18 – Katie Kirk.
Huyu alikuwa kwenye timu iliyopata ushindi wa kwanza katika mbio za kupokezana vijiti katika michuano ya Ubingwa wa Ulaya mwaka jana.
Sasa amenuia, na yupo katika mipango ya kuhamia kwenye mbio za mita 800 kwa ajili ya michezo ijayo ya Olimpiki.
Katie anayetoka Belfast, anasema kwamba mfano uliowekwa na wana Team GB waliopata medali ni hamasa tosha kwake kufanya kazi kwa nguvu zaidi kulifikia lengo lake.
“Hii inakuhamasisha kuongeza jitihada kwa sababu unajua unataka uwepo na ushindane katika ngazi hiyo.
“Medali zote zilizopatikana zina maana kubwa mno, kwa sababu ukifuatilia waliozipata, utaona jinsi walivyokuwa wakipiga hatua moja baada ya nyingine.
“Nakumbuka kumtazaa Mo Farah miaka michache iliyopita, alikuwa akikimbia vyema lakini hakuwa vizuri kama alivyo leo. Hii inaonesha kwamba ukiongeza bidii utafikia ngazi unayotaka,” anasema binti huyo.
Katie alichaguliwa na Dame Mary Peters, mwanariadha pekee alyepata medali ya dhahabu katika Olimpiki ya mwaka 1972 iliyofanyika Munich.
Mchezo alioshindia dhahabu, leo hii hujumuisha hatua mbalimbali, zikiwamo riadha, kuruka na kulenga shabaha. Ndio mchezo alioshinda Jessica Ennis.
“Nilikuwa na kocha mmoja, aliyezoea kukandamiza mkono wangu kwa nguvu huku akisema; ‘umefanya vyema, lakini ungeweza kufanya vizuri saidi’.
“Lakini leo wachezaji wana wataalamu wa saikolojia, wana wataalamu wa mifumo ya kibayolojia…kila aina ya wataalamu kwenye masuala ya afya, tofauti kabisa na enzi zetu,” anasema Peters.
“Ukipata watoto katika miaka yao ya awali – China wanawaanzia katika umri wa miaka mitatu – unaweza kuwajenga kuwa mabingwa.
“ Lakini si kila mtu anataka kufuata njia hiyo, wengine wanataka kuwa na nyakati nyingi za kupumzika na furaha zaidi.
“Hata hivyo, hakuna jambo la furaha zaidi ya unavyojisikia baada ya kushinda, umesimama kwenye jukwaa na unasikiliza wimbo wa taifa unapigwa,” anatoboa siri hiyo.
Gemma Gibbons alitwaa medali ya fedha kwenye judo na mwanatimu mwenzake, Karina Bryant siku iliyofuata akapata shaba.
Kilichotokea baada ya hapo ni kwamba ushindi ulichochea mapenzi kwenye mchezo huo. Mara watu 5,000 wakaomba kujiunga na klabu mpaka tovuti ikalemewa na kushindwa kufanya kazi kutokana na wingi wa waombaji waliokuwa mtandaoni.
Wiki moja baadaye, Gemma alikuwa Hyde Park akionesha medali yake kwa watoto waliokuwa wamepigwa na butwaa wakiwa mazoezini.
Michezo inayochukuliwa kuwa ni midogo inahitaji kutangazwa na ikitokea kuna ushindi wa medali, basi huvutia wachezaji wapya wanaoweza kuwa nyota wa siku zijazo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Judo Uingereza, Andrew Scoular alikuwa na haya ya kusema: “Sasa watu wameona wanamichezo wanashinda medali kwenye Michezo ya Olimpiki, upenzi unaanza kuwepo.
“Ukizingatia idadi ya watu wanaoongezeka kila mara na mchezo wenyewe unavyokua, lazima kutazama kwa makini, kuibua vipaji na kuvikuza kwa ajili ya Rio na baada ya hapo,” anasema Scoular.
Wanaamini kwamba siku moja watakuwa katika mafanikio ya wenzao wa mbio za baiskeli na upigaji makasia, kwa kutawala michezo mingine.
Gemma alisema: “Nadhani judo ya Uingereza inaweza kuwa hivyo. Ni wazi tuna safari ndefu baso, lakini nahisi hii tayari ni hatua ya kwanza. Tukiipiga ipasavyo, katika miaka minane au 12, tutakuwa kama wa mbio za baiskeli.”

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Siri ya Uingereza kufanya vizuri Olimpiki

Balozi Kallaghe: Tunahitaji mipango ya muda mrefu michezoni