in

Simba wanguruma Ligi ya Mabingwa Afrika

Mabingwa wa soka nchini Tanzania wamedhihirisha kuwa wamepania kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Afrika mbele ya watetezi Al Ahly baada ya kuichabanga klabu ya El Merreikh ya Sudan kwa mabao 3-0 katika mchezo uliochezwa leo jumanne saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin William Mkapa jijini Dar es salaam.

Licha ya kucheza bila mashabiki wao ambao ni kama wachezaji wa 12 uwanjani, Simba haikuonesha dalili zozote za kuyumbishwa na uamuzi huo wa Shirikisho la Soka Barani Afrika la kuitaka klabu hiyo kucheza mchezo wa nyumbani bila mashabiki wake ikiwa ni njia ya kuzuia maambukizo ya ugonjwa wa virusi vya Corona. Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kucheza bila mashabiki kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Mashabiki wa Simba wamejizolea umaarufu kutokana na kujazana uwanjani hapo kuwaunga mkono wachezaji wao, hali ambayo imewahi kutafsiriwa na kocha wa mabingwa watetezi wa taji hilo Al Ahly, Pitso Mosimane kwamba Simba inayo silaha kubwa kwenye uwanja wake wa nyumbani ambao ni mashabiki.

Ujio wa rais mpya wa shirikisho la soka CAF Patrice Motsepe pamoja na bodi ya shirikisho hilo lilipiga marufu mashabiki wa SImba kuingia uwanja kwa kile ilichokiita kushindwa kutekeleza maagizo ya namna ya kujilinda la maambukizo ya corona.

Wakati Simba ikiwa imecheza mchezo wake dhidi ya El Merreikh bila mashabiki, wapinzani wao AS Vita wakiwa nyumbani jijini Kinshasa waliruhusiwa kuingiza mashabiki uwanjani, hata hivyo hawakuweza kuokoa timu hiyo kupata kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa wageni Al Ahly ya Misri.

El Merrekh walicheza mchezo huo bila wachezaji wake 8 ambao walikutwa na maambukizo ya ugonjwa wa corona. Wachezaji Abdul Rahman Karango, Al Taj Yaqoub, Bakhit Khamis,Ramadan Wonder,Tony,Bakri Al Madina,Saif Al Damazin na Imad Abdel Moneim. El Merreikh wamedai kuwasilisha malalamiko yao CAF dhidi ya Simba kutokana na wachezaji hao kukutwa na corona kwa madai ya kufanyiwa hujuma.

Simba walianza mchezo wao dhidi ya El Merreikh kwa umakini na kuhakikisha wanazuia presha yoyote kutoka kwa El Merreikh ambao walitaka kupata bao la mapema ili kuichanganya Simba.

Hata hivyo alikuwa winga machachari wa Simba, Luis Miquissone aliyeipatia timu yake bao la kuongoza baada ya kazi nzuri iliyofanywa na mshambuliaji Chriss Mugalu,beki wa kulia Shomari Kapombe na kiungo Clotous Chama. 

Bao hilo lilionekana kutowashtua El Merrikh ambao waliendelea kucheza kwa utulivu lakini hawakuwa hatari mbele ya lango la Simba.

Simba walijiamini. Walicheza kwa utulivu, walitawala mchezo kwa pasi fupi na haraka pamoja na ubunifu mkubwa kutoka safu ya kiungo na washambuliaji. 

Kutoka akili kubwa ya Chama, hadi ubunifu na kasi ya Miquissone na Shomari Kapombe, pamoja na ubabe wa kutuliza mpira gambani na kupambana na mabeki wa Chris Mugalu uliwafanya El Merreikh waonekane si tishio mbele ya Simba.

Umakini,ubunifu na akili kubwa ya naodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ ulionekana kuwa hatari mbele ya El Merreikh ambao walishindwa kuwazidi maarifa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara. 

Matunda ya hali hiyo yalionekana baada ya Mohammed Hussein kupachika bao maridadi na kuwaacha hoi wachezaji wa El Merreikh. 

Mohammed Hussein alipachika bao hilo kwa shuti kali huku akitegemewa kuwa angepiga krosi ambayo El Merreikh walijipanga kukaba kwa kuziba nafasi (‘zonal marking).

Bao la tatu la Simba lilipachika kwa shuti kali na mshambuliaji wake Chris Mugali baada ya kupokea krosi maridadi ya Luis Miquissone kutoka winga wa kushoto, ambapo Mugali alituliza gambani kabla ya kuachia mkwaju mkali kwa mguu wa kulia.

Tanzania Sports
Heka Heka Golini…

Bao hilo liliua kabisa matumaini ya El Merreikh kuondoka angalau na pointi moja mbele ya wenyeji wao.

Katika mchezo huo Simba wlaimpoteza beki wao Joash Onyango ambaye aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na beki mkongwe Erasto Nyoni. 

Kama ilivyo kawaida kwenye michezo mingine, Luis Miquissone alibuka kuwa nyota wa mchezo huo baada ya kupachika bao la kwanza na kutengeneza bao la tatu.

Kwa ushindi huo Simba wanaongoza kundi A wakiwa wakina pointi 10 wakifuatiwa na Al Ahly wenye pointi 7 na AS Vita wenye pointi 4. Simba wamebakiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya Al Ahly itakayofanyika jijini Cairo nchini Misri, na mwingine utakuwa jijini Dar es salaam ambapo watawakaribisha AS Vita. 

Simba wanahitaji sare pekee kuweza kuwa vinara wa kundi hilo hadi mwisho. Wanahitaji sare jijini Cairo pamoja na sare nyingine jijini Dar es salaam au kuibuka na ushindi ili kutangaza ubabe zaidi kwenye kandanda msimu huu.

Katika mchezo huo kocha wa Simba, Didier Gomes alipanga kama ifuatavyo; Aishi Manula alirejea langoni baada ya kukosekana katika mchezo uliopita kutokana na kuwa majeruhi, wakati wengine walikuwa Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Joash onyango, Kennedy Juma, Taddeo Lwanga, Muzamiru Yassin,Cletous Chama,Bernard Morrison,Chris Mugalu na Luis Miquissone. 

Benchi walikuwepo Beno Kakolanya,Erastro Nyoni,Larry Bwalya, Jonas Mkude,Miraj Ibrahim,Meddie Kegere na Francis Kahata. 

Tanzania Sports
SIMBA

Kwenye mchezo wachezaji wa kigeni walioanza katika kikosi cha  Simba walikuwa sita; Joash Onyango,Taddeo Lwanga,Cletous Chama,Bernard Morrisson,Chris Mugalu,Luis Miquissone, na baadaye waliingia Larry Bwalya,Meddie Kagere na Francis Kahata.

ROBO FAINALI

Matokeo ya mchezo dhidi ya El Merreikh yanaonesha Simba wamebakiza mguu mmoja kufuzu hatua ya robo fainali, ambapo kwa msimamo wa kundi hilo ulivyo ni Al Ahly wanaweza kiufikisha pointi 12 ikiwa watashinda michezo miwili iliyosalia dhidi ya Simba jijini Cairo na El Merreikh nchini Sudan. AS Vita ikiwa watashinda michezo yake miwili wanaweza kufikisha pointi 10 sawa na za Simba sasa. 

Hata hivyo Simba kati michezo miwili watakuwa nyumbani dhidi ya AS Vita jijini Dar es salaam ambako si rahisi timu ya kigeni kuibuka na ushindi kwani zote zimefungwa. Simba wanahitaji ushindi dhidi ya AS Vita na sare mbele ya A Ahly jijini Cairo.

REKODI

Simba wanakuwa klabu ya kwanza kutoka tanzania kaatika michuano ya ligi ya mabingwa afrika hatua ya makundi ya kucheza michezo minne bila kufungwa na kufikisha pointi 10.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Barbara Gonzalez

MAFANIKIO YA UONGOZI WA BARBARA NDANI YA SIMBA

JPM

Magufuli ameng’arisha sekta ya michezo