in

Simba wamefanya ukatili wa soka

SIMBA SC

MICHUANO ya CECAFA inaendelea katika viwanja mbalimbali jijini Dar es salaam na kuzishirikisha timu nane zilizoko kwenye makundi mawili. Mashindano hayo yameibuka dakika za lala salama kabla ya pazia la msimu mpya kufunguliwa ifikapo Septemba 25 kwa mechi ya ngao ya jamii kati ya Simba na Yanga.

Mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba  hivi karibuni walitangaza kujitoa kushiriki mashindano  ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati maarufu kama Kagame Cup mwaka huu 2021. Timu nyingine ambayo ilijitoa kushiriki mashindano Tusker ya Kenya.

Baada ya timu hizo kujitoa zikapunguza idadi ya washiriki ambapo sasa timu 8 zinaendelea na michuano hiyo katika makundi mawili A na B. Hatua ya vigogo hivyo viwili kujitoa mashindanoni zilinifikirisha mno, kwamba haiwezekani kua na mbadala wa kushiriki zaidi ya kusingizia kuwapumzisha wachezaji walioshiriki Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika? Kwamba Tusker na Simba hazikuwa na njia nyingine ya kuendelea kushiriki mashindano hayo? Sidhani.

Nionavyo mashindano haya yanatengeneza nafasi kwa wachezaji wao. Kwa mfano Simba wana vikosi vitatu; timu ya wanaume inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania, timu ya vijana inayoshiriki mashindano ya Ligi kuu kwa ngazi ya vijana na timu ya wanawake inayoshirki Ligi Kuu upande wa wanawake.

Kwa vile mashindano ya CECAFA yanahusisha timu za wanaume bila shaka Simba na Tusker walikuwa na nafasi ya kuamua namna ya kupanga vikosi vyao vya kushiriki mashindano. Tumeona fursa waliyotoa klabu kama Yanga na Azam FC ambao wanatumia sehemu kubw aya vikosi vyao vya vijana kwenye mashindano haya.

Yanga na Azam kama zilivyoamua Simba na Tusker kupumzisha wachezaji wao wa vikosi vya kwanza, nao wamewapumzisha. Sehemu kubwa ya kikosi cha Yanga na Azam ni wale ambao hawajapata nafasi ya kutosha kuwakilisha timu hizo kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, pamoja na wachezaji wapya waliosajiliwa hivi karibuni.

Sasa turudi kwa Simba, wao walikuwa na kikosi cha vijana kilichoshiriki Ligi Kuu ngazi za vijana na kufungwa na Mtibwa Sugar katika nusu fainali. Vijana wa Simba walipaswa kutumika katika mashindano hayo, pamoja na wachezaji ambao wamesotea benchi sehemu kubwa ya msimu uliopita.

Chukulia wachezaji kama Mirad Ibrahim, Gadiel Michael,Ibrahim Ajibu, Duchu na wengine ambao hawajacheza mechi 20 kwa msimu. Kwa mchezaji kucheza chini ya mechi 20 kwa msimu haijengi uwezo wake wa ushindani,ubunifu,utimamu wa mwili na uwezo wake wa kusakata kandanda.

Sasa ubora wa wachezaji ambao haujaonekana katika mechi za Ligi Kuu utaonekana wapi ikiwa timu imejitoa kwenye mashindano ya CECAFA ambayo ni rahisi kumjenga mchezaji kama ambavyo mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayofanyika visiwani Zanzibar kila mwaka mwezi Januari.

Ingelikuwa rahisi Simba kueleza kuwa hawataki kushiriki CECAFA kwa vile ni mashindano yasiyoeleweka wala kuwa na ratiba maalumu na washindi kutopata fedha za maana. Hizi zingekuwa sababu za kuwaamsha zaidi CECAFA kwamba wanapaswa kuangalia suala la zawadi za washindi kwenye mashindano yao.

Haiwezekani timu ikatumia kiasi cha shilingi milioni 100 kuandaa timu kushiriki michuano ya CECAFA halafu mshindi wa kwanza wa mashindano anapewa zawadi ya Milioni 30. Huo ni utani ambao timu nyingi zinadharau mashindano ya CECAFA.

Mashindano hayo licha ya kupoteza heshima yake kutokana na kutoeleweka ratiba zake kila mwaka, lakini yanabaki kuwa sehemu muhimu ya kuwaandaa wachezaji kimwili,kiushindani na saikolojia.

Wachezaji wale ambao hawakutoa mchango mkubwa kwa kikosi cha kwanza wangeliweeza kutumika kuimarishwa viwango na kupimwa ikiwa wanapaswa kubaki klabuni kutoa changamoto kwa wale wa kikosi cha kwanza.

Vilevile mashindano ya CECAFA yangeliwezesha kikosi cha viana cha Simba kutumia kama njia ya kuwatia uzoefu wa mashindano makubwa wangalia vijana. kwa desturi ya soka letu wachezaji vijana huwa wanaepushwa kukabidhiwa majukumu mazito lakini kwa baadhi ya nchi zilizoendelea kisoka zinawakabidhi majukumu makubwa ili kuwajengea uwezo zaidi siku zijazo.

Wachezaji vijana wanaandaliwa kwa kupewa nafasi ya kushiriki mashindano au mechi nzito ili kupata ubora,uwezo wa kumudu presha na namna wanavyoweza kutumikia timu kubwa kongwe kama Simba.

Kwahiyo kujitoa CECAFA kunawanyima fursa timu ya viaja kuonesha umahiri pamoja na kufanya biashara ya kuuza wachezaji wangali makinda. Hakuna timu kubwa itakayomnunua mchezaji mwenye miaka 30 kutoka kwenye klabu zetu kwenda Ligi zilizoendelea lakini wanapoona wachezaji wadogo kiumri kama Duchu wanaweza kuweka fedha zao kwa sababu wana uhakika atakuwa na misimu mingine 6 ya kucheza soka.

Hilo lilikuwa suala la Simba kuamua namna ya kuwatangaza wachezaji wao wa kikosi cha pili pamoja na wale wanaokosa nafasi kwenye mashindano ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Si kweli kwamba CECAFA ni mashindano ambayo hayawezi kumsaidia mchezaji licha ya matatizo ya waandaaji wenyewe. Haya ni mashindano yanayojenga njia na kuonesha vipaji vya wachezaji,makocha na viongozi wao. Kuitosa michuano hiyo kwa sababu moja pekee bado hairidhishi wala kueleweka. Kilichofanyika ni kuwanyima fursa wachezaji wao wenyewe kuonesha umaridadi wa vipaji uliopo kwa mabingwa wa soka nchini na washindani wakubwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Lionel Messi

Messi anaondoka, lakini anakwenda wapi?

Premier League 2021-22

EPL ina mechi kali za ufunguzi