in , , , ,

Simba: Uchaguzi uko pale pale!

KAMATI ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imesema kuwa Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo uko pale pale kama (Juni 29 mwaka huu) kama ilivyotangazwa na pia imetangaza kumuengua tena mgombea wa nafasi ya Urais, Michael Wambura.

Akizungumza jana jijini, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Damas Ndumbaro, alisema kuwa kamati yake ilikutana juzi jioni kujadili tamko la Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) la kusimamisha uchaguzi wa Simba na kuona kwamba hana mamlaka hayo kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za shirikisho hilo.

Ndumbaro alisema kuwa ibara ya 10(6) ya kanuni ya uchaguzi za TFF zilizopitishwa mwaka jana inaeleza kuwa mwenye mamlaka ya kubadili tarehe ya uchaguzi, kusitisha au kufanya vinginevyo ni Kamati ya Uchaguzi.

Alisema kuwa si Rais wa TFF, Kamati ya Utendaji ya TFF, Mkutano Mkuu wa Simba au Kamati ya Utendaji ya Simba yenye mamlaka ya kusimamisha uchaguzi.

“Kama tungepokea ombi, tungelijadili, Kama FIFA walipokuja mwaka jana walitoa pendekezo kwa Kamati ya Uchaguzi na baadaye Lyatto (Deogratius-Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF) ndiye alitangaza kusogeza mbele sio Tenga (Leodegar) inakuaje Malinzi anasimamisha uchaguzi wakati Blatter (FIFA) hakufanya hivyo,” Ndumbaro alisema.

Aliongeza kuwa huwezi kusimamisha uchaguzi na kuitaka Kamati ya Utendaji ya Simba kuteua Kamati ya Maadili wakati wajumbe sita kati ya tisa ni wagombea na wana kesi ya kujibu wamefikishwa katika kamati ambayo wanatakiwa kuiunda.

Alisema pia kutokana na TFF kukataa Kamati ya Maadili isisikilize malalamiko waliyoyawasilisha, kamati hiyo inajipanga kupeleka malalamiko hayo ya wanachama FIFA huku ikiendelea na taratibu nyingine za uchaguzi.

KUMUENGUA WAMBURA

Ndumbaro alisema kuwa kamati yake imeuondoa Wambura kwa sababu mgombea huyo aliyekuwa amerejeshwa kwenye mchakato wa uchaguzi na Kamati ya Rufani ya TFF kwa kosa la kurudia kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa.
Mwenyekiti huyo alisema kwa kufanya hivyo, Wambura anaenguliwa kwa mujibu wa ibara ya 6( 1) (a-g), 6(1) (i) na 14 (3) za kanuni uchaguzi za TFF.

“Tulishamuandikia barua ya onyo Wambura, Evans Aveva na Julio (Jamhuri) ambao walifanya kampeni wakati wa kwenda na kurudisha fomu,” alisema Ndumbaro.

Aliongeza kuwa siku moja baada ya Kamati ya Rufani kutangaza kumrejesha Wambura kwenye mchakato huo baada ya kushinda rufaa yake, mgombea huyo alisema ‘Simba inahitaji wadhamini na si wafadhili’, Simba ilikuwa na viwanja vitatu lakini kimoja kimeuzwa na wajanja wa mjinisasa ina viwanja viwili’, hizi ni kauli za kampeni na hazihusiani na maamuzi ya Wakili, Julius Lugazia.

MALINZI, WAMBURA

Malinzi alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba alisema kwamba hana cha kuzungumza.
Wambura alisema kuwa yeye anachofahamu ni kwamba uchaguzi wa Simba umesimamishwa na hatambui kuenguliwa tena.
Katibu huyo wa zamani wa FAT alisema pia yeye hakufanya kampeni bali alikuwa anamjibu aliyekuwa mfadhili wa Simba, Azim Dewji.

WANACHAMA SIMBA

Mapema jana wanachama wa Simba waliokuwa wameshika kadi zao mkononi walifika makao makuu ya klabu hiyo wakisema kuwa wanataka uchaguzi uendelee.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake, Ras Simba (05757), alisema kuwa maamuzi ya Malinzi ni ya kukurupuka na wao wanataka zoezi la uchaguzi liendelee.
Simba alisema kwamba kitendo cha kuusimamisha uchaguzi huo ni kuiingilia klabu hiyo kuelekea kipindi muhimu cha usajili na maandalizi ya timu.

“Maamuzi yake mengi ni ya kukurupuka, hata alipomtaka Rage (Ismail) aitishe mkutano mkuu, alimgomea, hata sisi hatutaki asituingilie,” alisema mwanachama huyo.

Fihi Kambi (04717), alisema kuwa kwa nini kiongozi huyo amesimamisha uchaguzi baada ya Kamati ya Maadili kutakiwa kukutana, na akahoji ameona nini kitafuata.

Paul Makoye (537) alisema kuwa alimtaka Malinzi awe mwaminifu kwa katiba ya TFF na wanachama wa shirikisho hilo.
mwisho.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Ivory Coast yaanza vyema

Mourinho, Wenger wakunwa na wachezaji