in

‘Simba ni bingwa Ligi Kuu Bara’

SIMBA SC

LIGI Kuu Tanzania Bara imeendelea kushika kasi kote nchini, ambapo kesho jumapili kutakuwa na mechi kati ya Namungo FC dhidi ya Gwambina FC itakayochezwa mkoani Lindi. Hadi sasa timu nyingi zimecheza zaidi ya mechi 20, huku kinara wa Ligi hiyo Simba akifikisha pointi 61.

Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi hiyo mabingwa wa zamani Yanga walikuwa vinara na walimaliza wakiwa hawagusiki kabisa. hata hivyo katika mzunguko wa pili Yanga wameshindwa kufurukuta zaidi na kujikuta wakiruhusu Simba kuwakaribia zaidi hali ambayo inayeyusha matumaini ya kutwaa taji hilo lenye heshima nchini Tanzania.

Takwimu za msimamo wa Ligi ulivyo hadi sasa utaona wazi kuwa timu tatu zinazochuana kuwania ubingwa hazina uhakika licha ya kutanua misuli yao. Simba,Yanga na Azam ndizo timu zinazopigania nafasi ya kutwaa ubingwa msimu huu 2020/2021 huku  zikiwa na tofauti kubwa ya mechi walizocheza.

Katika mzunguko wa kwanza Simba haikuonesha dalili zozote za kutwaa ubingwa huo na ilionesha wazi huedna wangeupoteza kwa watani wao wa jadi Yanga. Hata hivyo ni Yanga ambao walilazimika kubadilisha benchi lao la ufundi kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.

Makocha wanne wameifundisha Yanga katika nyakati tofauti, ambapo sasa wananolewa na raia wa Tunisia, Nasredine Nabil, na sasa wamemrejesha kocha wao wa zamani Razack Siwa kuwa kocha wa makipa. Siwa amewahi kuwa kocha wa makipa kwa nyakati tofauti na baadaye kaimu kocha mkuu.

Msimamo wa Ligi unaonesha wazi kimahesabu Simba wana nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao kwa msimu wa nne sasa. Simba wamecheza mechi 25, wameshinda mechi 19, wamefungwa mechi mbili, wametoka sare mechi 4 na wamejikusanyia pointi 61 kileleni.

Yanga wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 61 sawa na Simba. Tofauti yao ni kwmaba Yanga wamecheza mechi 29, wameshinda mechi 17, wametoka sare mechi 10, wamefungwa mechi mbili sawa na vinara wa Ligi hiyo Simba.

Nafasi ya tatu inashikiliwa na mabwanyenye  Azam FC wakiwa wamejikusanyia pointi 57 kutokana na mechi 29. Azam wameshina mechi 16, wametoka sare mechi 9, wamefungwa mechi 4.

Nafasi ya nne imekwedna kwa klabu ya Biashara United ya mkoani Mara wakiwa na pointi 45 kutokana na mechi 29 walizocheza. Biashara United wameshinda mechi 12, wametoka sare mechi 9 na wamefungwa mechi 8.

Nafasi ya tano imekwenda kwa KMC FC wakiwa na pointi 41 kutoka kutokana na mechi 29. KMC wameshinda mechi 11, watoka sare mechi 8, wamefungwa mechi 10. Nafasi ya sita imekwenda kwa Polisi Tanzania ambao wamejikusanyia pointi 41 katika mechi 29. Polisi Tanzania wameshinda mechi 9, wametoka sare mechi 14, wamefungwa mechi 7.

Kimahesabu Simba wamebakiza mechi 4 mkononi sawa na kusema ni kiporo ambacho kinatakiwa kukamilisha kabla ya kuzifikia mechi 29 walizocheza wapinzani wake. Kama Simba wanaongoza Ligi kutokana na mechi 25, maana yake wanaweza kushinda mechi zingine.

Si rahisi kwa Simba kufungwa mechi 4 za viporo na kuamini kuwa watapoteza ubingwa wao. Tayari wamefungwa mechi 2 tangu kuanza kwa Ligi ikiwa na maana wana wastani mzuri wa kushinda mechi zao.

Yanga ambao wamecheza mechi 29 sawa na Simba wanalingana kwa pointi na vibara hao 61. Timu zote mbili zimepoteza mechi 2. Tofauti yao ni kwamba Yanga wameshinda mechi 17, wakati Simba wameshinda mechi 19.

Simba wametoka sare mechi 4, wakati Yanga wametoka sare mechi 10. Ukilinganisha mechi 25 kwa 29 kisha timu iliyocheza mechi pungufu inaongoza Ligi kutokana na ushindi wa mechi 19 maana yake ina nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo.

Azam FC na Yanga licha ya kupigania ubingwa zinategema Simba wapoteze mechi zao zote nne ili wao waweze kujitangaizia ubingwa. Simba watataka kushinda mechi 4 za vipoiro, lakini hata kama watashinda mechi 2 maana yake watakuwa wanaongoza Ligi na kuwaacha nyuma Yanga na Azam.

Kutegemea Simba wafungwe ndipo Azam FC na Yanga zitambe kileleni ni habari ngumu ambao haiwezi kudumu ama kutokea katika mazingira ya Ligi ya Tanzania.

Uwezekano wa timu za Yanga,Azam,Biashara United na KMC kulitwaa taji hilo kwa sababu zenyewe katika mechi 29 zimeshindwa kuwaacha mbali mabingwa watetezi Simba kwa tofauti ya mechi nne ambazo ni nyingi mno kimashindano. Simba wako nyuma katika kucheza mechi za Ligi kuu kwa sababu ya ushiriki wao kwenye mashindano ya kimataifa.

Uhakika uliopo ni kwamba Yanga na Azam Fc zinaweza kushiriki mashindano ya kimataifa ya CAF msimu ujao ikiwa zitafanya vizuri katika msimamo wa Ligi pamoja na kunufaika na mafanikio ya klabu ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Aidha, msimamo wa Ligi wenyewe unachotusaidia ni kuona ushindani kuwa mkubwa miongoni mwa timu, kwa sababu hadi sasa ni Mwadui FC pekee wenye uhakika wa kushuka daraja. Lakini timu za Ihefu,Gwambina,Coastl Union na JKT Tanzania yeyote kati yao anaweza kushuka daraja.

Pia kasi ya Biashara United kushikilia nafasi ya nne Ligi Kuu nayo inasisimua na kuleta ladha ya ushindani. Ni matumaini kuwa msimu ujao pia utakuwa katika hali hiyo na kuipa ushindani zaidi Ligi hiyo pamoja na kuvutia mastaa mbalimbali wa  soka,makocha na wataalamu wa mchezo huo kutoka nje ya Tanzania.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
ZZ

Makocha watajwa kumrithi Zidane

SIMBA SPORTS CLUB

Simba wametoa onyo Afrika