in

Simba katikati ya wababe wa soka Afrika

Ingawa Yanga ni klabu iliyotwaa mataji ya Ligi Kuu mengi zaidi kuliko zingine nchini  Tanzania, lakini Simba ndio yenye mafanikio zaidi kwenye soka la Kimataifa. Yanga  wamelitwaa taji la Ligi Kuu mara 27.  

Hata hivyo kwenye michuano ya kimataifa jina la klabu ya Simba linachomoza zaidi  kuliko Yanga. Hiyo ni miongoni mwa sababu ambazo zinaifanya timu hiyo kwa sasa  kuwa katikati ya vigogo wa soka barani Afrika ambao wanatarajiwa kushiriki African  Super League. 

Wakati mwaka 2021 unaeleke ukingoni ni wakati ambao bila shaka yoyote Shirikisho la  Soka Afrika lipo kwenye hatua za mwisho za kutengeneza utaratibu wa kuendesha  mashindano ya Africa Super League. Swali je timu zipi zinaweza kushiriki African Super  League? 

TANZANIASPORTS katika uchambuzi huu inaangazia sifa mbalimbali za timu ambazo  zinatarajiwa kushiriki mashindano hayo. Kati ya timu 20 zinazotakiwa kushiriki  mashindano hayo, tayari timu 15 zinajulikana, miongoni mwao ni Simba ikichomoza  kutoka ukanda wa Afrika masshariki. 

AL AHLY (Misri) 

Mabingwa wasioshindika barani Afrika kwa muda mrefu na ndio klabu ya karne katika  bara hilo kwa mujibu wa shiikisho la CAF. Hakuna wasiwasi wowote kwa timu hii kuwa  nambari moja katika soka barani Afrika kwa sababu mafanikio yake yanajieleza bayana.  

Baada ya kufungwa katika fainali mbili za Ligi ya Mabingwa mwaka 2017 na 2018,  walifanikiwa kurekebisha makosa yao na kuwa timu kabambe Afrika. Na sasa  wamefanikiwa kutwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika mfululizo. Ni  miongoni mwa alama ya soka la kiarabu barani Afrika. 

ESPERANCE (Tunisia) 

Ukizungumzia soka la Afrika na mafanikio yake ngazi ya klabu bila shaka hii ni klabu  mojawpao itakayokuwa kwenye orodha yako. Mafanikio yao makubwa ni baada ya  kutwaa mataji mawili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018 na 2019. Hii  nayo ni timu inayotarajiwa kushiriki African Super League. Bila shaka yoyote watatoa  ushindani mkali kwenye michuano hiyo kama ilivyo ada kwao. 

WYDAD CASABLANCA (Morocco)

Watanzania wengi wanaifuatilia klabu hii. Sababu moja kubwa ni kuwepo kwa nyota  wao Simon Msuva ambaye amewahi kutamba katika klabu ya Yanga miaka ya nyuma.  Msuva anakipiga katika klabu yenye ushindani mkali kwemye Ligi Kuu Morocco.  

Klabu hii ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa baran Afrika mwaka 2017, na mwaka 2019  ilifika fainali ya Ligi hiyo lakini ikachapwa Esperance ya Tunisia. Kuanzishwa kwa  African Super League kutashuhudiwa tena umahiri na ushindani wao wanaotoa kila  mara ikiwemo msimu uliopita ambako walitolewa katika hatua ya nusu fainali na Kaizer  Chiefs. 

RAJA CASABLANCA (Morocco) 

Ni miamba mingine kutoka nchini Morocco ikiwa na sifa za kipekee katika mashindano  ya soka barani Afrika. Miamba imerudi Ligi ya Mabingwa baada ya kupoteana kwa  miaka 15 bila kushiriki mashindano makubwa Afrika. Na sasa Raja Casablanca  wanarejesha makali yao.  

Ndani ya miaka minne wameshinda mataji mawili ya Kombe la Shirikisho CAF kwa  kuwachapa wababe wa Algeria, JS Kabylie, na ilitwaa Super cup mwaka 2019.  

Je ikiwa watashiriki African Super League kutarejesha mafanikio yao kwenye soka kama  kipindi cha mwaka 1997 na 2004? 

SC ZAMALEK (Misri) 

Wababe wa soka Afrika, hilo halina mashaka kabisa, lakini Zamalek haijashinda taji  laLigi ya Mabingwa Afrika tangu wachukue lile la mwaka 2002. Hata hivyo mwaka 2009  walishinda Kombe la Shirikisho, na baadaye wakafanikiwa kufika fainali ya Ligi ya  Mabingwa. Na sasa wanaweza kung’arisha nyota yao kwenye African Super League. 

MAMELODI SUNDOWNS (Afrika kusini) 

Hii ni miamba ya soka kusini mwa bara la Afrika na mshindani mahiri katika bara zima.  Mamelodi wanatamba kwenye Ligi Kuu Afrika kusini lakini ipo dhana kwamba timu hii  bado inatafuta ubabe wa soka katika mashindano ya Afrika kwa ujumla tangu  kuondokewa na kocha wao Pitso Mosimane.  

Msimu uliopita 2020/2021 walitolewa katika hatua ya nusu fainali na waliokuja kuwa  mabingwa Al Ahly. Mamelodi Sundowns wamewahi kutwaa taji la Ligi ya mabingwa  Afrika mwaka 2016. Michuano ya African Super League itakuwa sehemu yao ya  kutangaza umwamba katika kandanda. 

TP MAZEMBE (DRC)

Washindi waliotoweka ghafla kwenye anga za soka la Afrika. Kwa mujibu wa shirikisho  la Soka Afrika, CAF linasema TP Mazembe ni klabu iliyocheza fainali 10 za CAF katika  kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2018. 

Tangu walipopata mafanikio hayo wakiwa na nyota wao Mbwana Samatta na Thomas  Ulimwengu raia wa Tanzania hawajawahi kurudia tena kilele cha mafanikio hayo, lakini  wamebaki kuwa klabu tishio katika soka la Afrika. 

RS BERKANE (Algeria) 

Nyota mpya, klabu mpya inayong’ara katika soka barani Afrika kwa sasa. RS Berkane  msimu uliopita walitwaa Kombe la Shirikisho wakiwa wamenufaishwa na uwekezaji na  usajili mzuri klabuni hapo. Ujio kocha Florent Ibenge kutoka klabu ya AS Vita ya DRC  kumeongeza uimara na ushindani. Ni timu ya kuchungwa endapo itashiriki kwenye 

African Super League. 

HOROYA (Guinea) 

Huenda ikawa timu inayoshangaza kutajwa kwenye mashindano ya African Super  League. Horoya hawajawahi kufika fainali yoyote ya mashindano ya CAF tangu  walipofanya hivyo mwaka 1978. Miamba hiyo kutona Guinea walitolewa kwenye hatua  ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.  

ETOILE DU SAHEL (Tunisia) 

Miamba ya soka ya Tunisia ambayo haina taji lolote la Afrika tangu walipotwaa Ligi ya  Mabingwa mwaka 2007, lakini walitwaa pia Kombe la Shirikisho mwaka 2015. Ni klabu  inayojumuishwa kwenye mashindano ya African Super League. 

PYRAMIDS (Misri) 

Ikiwa imeanzishwa miaka michache iliyopita na kupata uwekezaji mkubwa, Pyramids  wameonesha kuwa wanaweza kumsajili mchezaji kwa gharaa yoyote na kuwa tishio  katika soka barani Afrika. Mwaka 2020 walifungwa katika mchezo wa fainali ya Kombe  la Shirikisho CAF. 

JS KAYBLIE (Algeria) 

Walifungwa kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita, lakini kizazi cha  dhahabu cha klabu hiyo kimeendelea kutoa matumaini kuwa kinaweza kufanya mambo  makubwa zaidi kwani kushiriki kwao fainali tatu mfululizo kwa misimu mitatu  kumewapa uzoefu zaidi. hawa ni mabingwa Afrika mwaka 1981 na 1990. 

AS VITA (DRC)

Washindi wa pili wa Ligi ya mabingwa Afrika mwaka 2014 na Kombe la shirikisho  mwaka 2018. Hata hivyo msimu huu AS Vita wamempoteza kocha wao Florent Ibenge ambaye amehamia RS Berkane. 

KAIZER CHIFES (Afrika kusini) 

Walifungwa katika mchezo wa fainali msimu uliopita na Al Ahly. Ni mongoni mwa timu  ambazo zinaweza kushiriki michuano ya African Super League lakini walikuwa na hali  mbaya Ligi Kuu Afrika kusini.  

SIMBA (Tanzania) 

Katika ukanda wa Afrika mashariki Simba ndio wababe ambao wametajwa kuwa na sifa  za kushiriki African Super League. Ni timu ambayo kwa miaka minne imewakilisha  Tanzania kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Ukubwa wa sifa za makocha ni ubora wa Ligi Kuu Bara 

SIMBA SC

Mambo  ya kuchungwa na Simba jijini Lusaka