in , ,

Simba imeshinda lakini isisite kujifunza kwa Al Ahly

Hakuna furaha kama kuupanda mlima ambao huonekana mrefu kwa wengi. Ushujaa hujaa ndani yako pale unapofika ƙkatika kilele cha mlima huo.

Inawezekana kabisa ushindi wa Simba wa jana ulikuwa kama kupanda mlima mrefu ambao wengi huogopa sana kuupanda.

Na kwa kiasi kikubwa walifanikiwa kuupanda huo mlima,lakini wamebakiza kitu kimoja cha msingi sana.

Nacho ni kufika katika kilele, kufika sehemu ambayo macho ya wengi yatamtazama kama mtu shujaa zaidi katika bara hili.

Ushujaa ndiyo unaokosekana katika kikosi cha Simba. Kuifunga Al Alhly haimanishi kuwa wao ni mashujaa katika mpira.

Kwa kifupi kufika KIBO au MAWENZI hakukupi nafasi ya wewe kuonekana mwamba. Cha muhimu ni wewe kupigana ili kufika kileleni tu.

Kilele ambacho kitawafanya wengi wakuheshimu na kukuona kama mtu mkubwa unayeogopeka sana katika maisha ya soka.

Natamani sana Simba ifikie katika hatua hii, natamani kuiona siku moja Al Alhly wakiwa nyumbani kwao wawe wanaiogopa Simba kila inapotua Cairo.

Hatua ambayo Simba itakuwa inagombania wachezaji na kina TP Mazembe, Al Ahly, Mamelodi Sundows.

Sehemu ambayo jezi ya Simba iwe imechafuka kwa matangazo mengi ambayo ni pesa kwao katika biashara hii ya mpira.

Mpira ni biashara, huwezi kuendesha mpira bila pesa na kitu chochote kinachohusisha pesa huwa ni biashara.

Hivyo Simba inatakiwa ifike katika hatua hii. Hatua ya kuwa na wadhamini wengi ndani ya klabu ili kuipa nguvu Simba kufika katika kilele cha mlima ushujaa.

Msimu jana nilikuwa natazama mechi ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika, ambapo niliwashuhudia mabingwa Esperance.

Ulitazama jezi zao? kuanzia fulana yake mpaka bukta ya timu? Zilikuwa zimejaza matangazo ya biashara.

Huku ndiko Simba inapotakiwa kufika, kutengeneza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara kuja kuweka pesa zao kwa ajili ya kuwekeza Simba.

Simba inatakiwa kuwavutia mashirika ya ndege yaje kuwekeza pesa zao hapa. Ndege ambayo itakuwa na msaada ya kuwasafirisha wachezaji katika michuano mbalimbali.

Leo hii Simba haina GYM ya wachezaji kufanyia mazoezi, wakati kuna GYM nyingi sana ambazo zinaweza zikaidhamini Simba kwa makubaliano ya kibiashara.

Uliwaona jana Al Ahly kwenye jezi yao kifuani? , uliwaona UMBRO? Hawa ni watengenezaji wa jezi za Al Ahly.

Na hawa pia wanahusika kuuza jezi zote za Al Ahly, kiasi kwamba wao ndiyo wanahakikisha kuna faida kubwa inayopatikana kupitia mauzo ya jezi za Al Ahly.

Hiki kitu kinawezekana sana kwa Simba, Simba ina mashabiki wengi sana hapa nchini. Mashabiki ambao wanaweza wakawa chachu ya kununua jezi hizo.

Hakuna kinachoshindikana, tunakiwa tufike alipo Al Ahly, kumfunga pekee hakutoshi. Kumfunga hakutoshi kutupa nafasi ya sisi kufurahia.

Tuwekeni mazingira bora ya sisi kufika hapo walipo. Wanafanya usajili kwa njia gani? vipi kuhusu Academy zao zinazozalisha wachezaji?

Vipi kuhusu kuwa na timu ya ‘Scouting’ kwa wachezaji imara ndani ya timu?. Huku ndiko tunapotakiwa kupatazama.

Ushindi huu usitufanye ƙkabisa kusahau tunapoelekea. Tunatakiwa tutengeneze njia bora ya sisi kufika sehemu ya kufika mbali.

Pamoja na kuwafunga Al Ahly tunatakiwa tukae na kujifunza kipi kimewasaidia wao kufika sehemu ambayo wapo walipo.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ligi yetu inazungumza UONGO sana

Tanzania Sports

Tanzia kwa kipa hodari Gordon Banks