Simba avutwa sharubu Moro

Kibarua cha mechi tatu mfululizo za ugenini kimeanza kwa ugumu kwa Simba, baada ya kushikwa na Mtibwa Sugar kwa sare ya 1-1.

Alikuwa ni mshambuliaji wao wa zamani, Musa Hassan Mgosi aliyetaka kuwaaibisha Simba kwa kufunga bao la kwanza, lakini Amisi Tambwe akamwambia kwamba alikuwa macho, akarejesha bao hilo baadaye.

Simba waligutushwa mapema juu ya hatari ya walamba sukari hao, kwani licha ya kuikamia mechi hiyo chini ya Kocha Mkuu Zdravko Logarusic, kwani bao la Mtibwa liliwekwa kimiani dakika ya nane tu ya mchezo.

Licha ya Mtibwa kumaliza mechi wakiwa pungufu ya mtu mmoja kutokana na Shaaban Nditi kulimwa kadi nyekundu dakika ya 69, Simba waliambulia pointi hiyo moja tu.

Mgosi alistahili pongezi kwa bao lake, kutokana na kutokuwa legelege wala kulialia alipofanyiwa rafu na Donald Mosoti wa Simba, bali alinyanyuka na kusonga na mpira hadi akafunga na kuwaacha vinywa wazi mashabiki wa Simba wa mjini Morogoro na wale waliosafiri kutoka Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba wamejiongezea pointi moja tu na kufikisha 31 na kuwashusha Mbeya City wenye pointi kama hizo hadi nafasi ya nne, juu wakiwapo Azam wenye 36 na Yanga wakifuatia kwa zao 35. Mtibwa wapo nafasi ya tano.

Baada ya hapa Simba atakuwa na kazi Tanga kwa Coastal Union na Mbeya kwa Mbeya City, zote zikiwa ni mechi ngumu.

Comments