in , , ,

SHIKENI KALAMU YENYE MACHO, MASIKIO NA AKILI YA KISHERIA.

Alexis Sánchez

Vurugu za usajili tayari zimeshaanza, kila uchwao habari mpya
zimekuwa zikipishana kuingia kwenye ngoma za masikio yetu.

Vurugu hizi zimekuwa kubwa na zimekuwa zikifanywa bila kujali mioyo
yetu sisi mashabiki inaumia au inafurahia kiasi gani pindi habari
hizi tunapozisikia . Na hii yote hukamilisha maana halisi ya neno
shabiki kuwa lazima utaniwe uumie, utambe ufurahie.

Hayo ndiyo maisha halisi ya shabiki, yeye kazi yake ni kutamba mbele
ya mpinzani wake kwa kujiaminisha yeye ndiye anakitu bora kuliko
mwenzake ili mradi tu siku ziende, na ndipo hapa viongozi wengi wa
timu zetu huchukua nafasi ya kusajili mchezaji ili kutimiza matakwa ya
shabiki na siyo matakwa ya benchi la ufundi.

Wakati shabiki akikenua meno kufurahia usajili wa mchezaji nyota ndani
ya timu yake binafsi huwa siyaangalii na kuyafikiria meno 32 ya huyo
shabiki, akili yangu yote huwa inakuwa ikimuwaza mchezaji nyota
aliyesajiliwa na timu ya huyo shabiki.

Maswali mengi huwa yanazunguka sana kichwani mwangu, hivi kipi huwa
kinawapelekea kutia saini ? Ile pesa kubwa ya usajili? Ukubwa wa
timu husika? Au ubora wa timu husika kwa kipindi hicho na ushiriki
wake wa mechi za kimataifa? Au maono ya klabu husika kwenye maendeleo
ya mpira wa miguu bila kujalisha udogo wake? Au ni vipengele vilivyo
ndani ya mkataba ndivyo huwa vinamshawishi pia mchezaji kutia saini?

Maswali yote haya yanaonesha kuwa kuna mengi ya kusoma na kufikiria
kabla ya mchezaji hajasaini mkataba na timu yake mpya.

Kuna vitu vingi sana vya kuangalia, mchezaji macho yake hayatakiwi
kuishia kwenye donge nono la pesa aliloahidiwa na viongozi wa timu
husika. Macho yake yanatakiwa yapenye zaidi ya kwenye hilo donge nono
la pesa.

Najua hapa ndipo palipo na ugumu maana wingi wa pesa za usajili
hufanya wengi wa wachezaji wetu kuwa vipofu na viziwi mpaka kuingia
mkataba ambao unakuwa wa kinyonyaji kwa upande wake bila hata kuusoma
na kuutafakari vizuri.

Ndipo hapa umuhimu wa mawakala au wanasheria unapokuja, lakini cha
ajabu wachezaji wetu walio wengi wao ndiyo mawakala na wanasheria.

Kila kitu wanakifanya wao, kuanzia mazungumzo ya awali ya kusajiliwa
mpaka watakaposajiliwa ndiyo maana akili zao huishia kuangalia na
kusikia pesa ya usajili wanayoahidiwa pekee na kusahau vitu vingi vya
muhimu ambavyo vinatakiwa viwepo kwenye mkataba.

Hakuna golikipa anayewaza kipengele cha Clean sheets (kutofungwa goli
kwenye mechi) anazopata kwenye mechi zitamnufaisha kwa kuingiza pesa
kiasi gani. Kila Clean sheet kwenye mechi inakuwa na marupurupu ya
pesa kiasi gani kwenye kila mechi anayopata clean sheet.

Hakuna mshambuliaji anayefikiria hat trick ( kufunga magoli matatu
kwenye mechi) ina manufaa gani kwenye uchumi wake. Hakuna mchezaji
anayewaza kiwango cha bonus (marupurupu) atakayoyapata kipindi
ambacho timu itashinda au kudraw( kutoa sare au suluhu).Mara nyingi
timu zetu zimekuwa hazina kiwango maalumu cha kuwalipa wachezaji wetu
kipindi ambacho timu inaposhinda au kutoa suluhu au sare.

Kwenye mikataba mingi ya wachezaji kipengele cha timu kushinda au
kupate sare huwa haiainishi kiwango cha pesa ambacho mchezaji atapata,
mara nyingi kiwango hiki cha pesa hutolewa na viongozi wa timu
kulingana na wanavyojisikia.

Wakati mwingine kwenye mechi kubwa kama ya Simba na Yanga, viongozi
wengi ndiyo huwa wanatoa ahadi kubwa sana ili tu wachezaji wa timu
husika wapigane ili kuipata pesa hiyo iliyoahidiwa.

Kiuhalisi hiki kitu siyo kizuri, na hiki kitu kinatakiwa kianzie
kwenye mikataba hii ambayo muda huu wachezaji wanaingia.

Kunatakiwa kuwepo kipengele ambacho kitaainisha marupurupu ya kila
mechi watakayoshinda au kutoa sare. Kiwango cha pesa kinatakiwa
kianishwe ndani ya mkataba kulingana na uzito wa mechi na siyo kupewa
pesa ambayo viongozi hujisikia kutoa wao.

Kuna wakati wachezaji wanatakiwa kutambua kuwa njia za kuingiza mapato
kwa mchezaji ni tatu ambazo ni mshahara, marupurupu na mikataba ya
kibiashara na kampuni mbalimbali za kibiashara. Na vitu vyote hivi
ili uvipate unatakiwa uwe makini na mkataba unayoingia na timu yako
kwanza.

Martin Kiyumbi

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MAENEO YATAKAYOAMUA MECHI YA FAINALI KATI YA REAL MADRID NA JUVENTUS

Tanzania Sports

HIZI VURUGU ZINAFUATA MAELEKEZO YA KOCHA AU TUNAFURAHISHA MASHABIKI?