in , , ,

Sherwood afukuzwa Villa

 
Hatimaye Aston Villa wametangaza kumfuta kazi kocha wao, Tim Sherwood baada ya mwenendo mbaya wa timu, ambapo baada ya mechi 10 wameambulia pointi nne tu.

Uamuzi huo umekuja pungufu ya saa 24 tangu walipopoteza mechi dhidi ya Swansea kwa 2-1 Jumamosi hii, na muda mfupi baada ya Mwingereza huyo kudai kwamba angeendelea kupambana katika kazi yake.

Sherwood (46) anaondoka akiwaacha Villa katika nafasi ya 19, wakiwa na uwiano mbaya wa mabao ambao ni -8 na ameondoka baada ya kukaa klabuni hapo kwa miezi minane tu. Alifurahia sana uteuzi huo na alishaanza kuhudhuria mechi Villa Park kabla ya kuajiriwa, akalalamikiwa na baadhi ya watu kwamba alikuwa akiwaombea mabaya makocha waliokuwapo.

Mwenyewe alikuwa hana kazi baada ya kufukuzwa Tottenham Hotspur kutokana pia na kushindwa kumudu kazi hiyo. Kabla yake kocha hapo alikuwa Paul Lambert akisaidiwa na Roy Keane aliyeacha kazi ili kujikita katika ukocha msaidizi wa Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Ireland.

Kichapo kutoka Swansea kilikuwa cha sita mfululizo kwenye Ligi Kuu ya England. Klabu katika tamko lake ilisema: “Bodi inaamini kwamba matokeo ya uwanjani hayakuwa mazuri hivyo kwamba lazima mabadiliko yafanyike.”

Kocha wa zamani wa Everton na Manchester United, David Moyes anayefundisha Real Sociedad anapewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Sherwood. Kwa sasa, kocha wa kikosi cha vijana U-21 cha klabu hiyo, Kevin MacDonald atashika nafasi hiyo kwa muda.

Sherwood aliteuliwa Februari mwaka huu na kufanikiwa kuwafikisha Villa fainali ya Kombe la FA na timu wakamaliza msimu uliopita wa ligi wakiwa nafasi ya 17, nafasi moja tu juu ya timu tatu zilizoshuka daraja. Msimu huu ameshinda mechi moja tu kati ya 10 za ligi kuu.

Mwingereza huyu amesimamia mechi 28 tu kwenye mashindano yote – muda mfupi zaidi kwa kocha yeyote yule wa kudumu wa Villa. Klabu wamemshukuru sana Villa kwa jitihada zake zote alizofanya katika kipindi kigumu cha msimu uliopita na kwa michango yake chanya mingi aliyochangia kwenye soka.

Advertisement
Advertisement

Baada ya mechi dhidi ya Swansea Jumamosi hii alikwepa kujibu swali iwapo wiki hii ingemkuta kazini Villa Park, akisema; “mie si mtu sahihi wa kuuliza swali hili … nahisi kana kwamba klabu imo shimoni. Kwa sasa tumetindikiwa.”

Kiungo huyu wa zamani wa Spurs aliteuliwa na klabu yake hiyo ya zamani kuwa kocha White Hart Lane Desema 2013 lakini akafutwa kazi Mei mwaka jana licha ya klabu hiyo kumaliza ligi wakiwa katika nafasi nzuri ya sita.

Majuzi alinukuliwa akisema kwamba anachoshwa na aina ya uchezaji wa wanasoka wa Aston Villa, akisema timu yenyewe inamboa. Hata hivyo, Sherwood alisema kwamba alidhamiria kuendelea na kazi kama askari mstari wa mbele akiwa na panga, na hata akifa afe nalo, na kweli Jumapili hii mwisho wake umefika.

Sherwood alizaliwa Februari 6, 1969 eneo la Borehamwood, England  na alicheza soka kuanzia 1987 hadi 2005, akatamba zaidi akiwa nahodha wa Blackburn Rovers akatwaa nao ubingwa 1995. Amepata pia kuchezea Watford, Norwich, Portsmouth na Coventry City. Amecheza mechi tatu katika Timu ya Taifa ya England mwaka 1999.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Arsenal kileleni

Tanzania Sports

Man United, City doro