in

Sarpong anaweza kuyakuta mabegi yake ‘Airport’

Michael Sarpong

Yanga wana pointi 37 za Ligi Kuu Tanzania Bara. Pointi zao zinawafanya  waongoze Ligi baada ya kucheza mechi 15. Katika mchezo wao wa mwisho  dhidi ya Mwadui, walishinda mabao 5-0. Mshambuliaji mwingine wa Yanga  Yacouba Sogne alipachika mabao mawili katika ushindi huo.  

Huyu ni mshambuliaji ambaye alianza taratibu kuliko Michael Sarpong.  Yacouba anacheza tofauti na Sarpong, pia ana uwezo mkubwa wa  kuchezesha timu hata kama yeye hafungi, ni aina ya wachezaji ambao  wanaifanya timu inufaike na kitu cha ziada kutoka kwake.  

Sasa kwa upande wa Sarpong amekuwa mchezaji mwenye machachari  mengi dimbani. Mabeki wa timu pinzani huwa zinamuwinda kila mechi  anayopangwa. Ni mshambuliaji ambaye ambaye ananikumbusha mtindo  wa Joseph Kaniki maarufu kama Golota.  

Kaniki alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti lango la  adui,matumizi ya nguvu na alikuwa hawezekaniki. Hata hivyo Joseph  Kaniki hakuwa na kasi kama ilivyo kwa Michael Sarpong.  

Ukizungumzia washambuliaji wenye nguvu na machachari kwa sasa jina la  Michael Sarpong litakuwepo. Ana nguvu, mpambanaji na zaidi ni  mshambuliaji ambaye anamfanya beki awe macho wakati wote. Mabeki  wanatakiwa kuwa macho si kwa kuhofia kufungwa bao bali namna Sarpong  anavyocheza na kuwa tishio kwa timu zao. 

Michael Sarpong ni miongoni mwa washambuliaji waliosajiliwa msimu huu 2020/2021 akichukua nafasi ya David Molinga. Sarpong ana uzoefu wa Ligi  za Afrika mashariki kwa vile amewahi kicheza soka nchini Rwanda. Katika  ardhi ya Tanzania hii ni mara yake ya kwanza kucheza timu za hapa.  

Ukitazama orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jina la Michael  Sarpong halipo kati ya watano wa juu. Orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu  watano inashikiliwa na John Bocco (Simba), Adam Adam(JKT  Tanzania),Prince Dube (Azam),Cletous Chama(Simba)Meshack Ibrahim  (Gwambina), Meddie Kagere (Simba), Michael Sarpong na Obrey 

Chirwa(Azam). Wafungaji hawa ni wale ambao wana mabao zaidi ya  manne.  

Hii ina maana Michael Sarpong amefikisha mabao manne licha ya Ligi Kuu  kufikisha mzunguko wa 15. Yanga wamecheza mechi 15 hadi sasa. Mshambuliaji wa kigeni kuishindwa kufurukuta mbele ya wazawa ni jambo  linaloleta mjadala.  

Orodha ya wafungaji wanaoongoza Ligi Kuu ni wazawa. Washambuliaji wa  kigeni watatu Prince Dube,Middie Kagere na Obrey Chirwa wamepanya,  pamoja na kiungo Cletous Chama. Yanga licha ya kuwa na washambuliaji  wa kigeni bado hawajafurukuta kupachika mabao. 

Michael Sarpong ndiye mshambuliaji kiongozi wa Yanga. Nafasi  anayocheza ni kuhakikisha anapachika mabao ya kutosha ili kulinda namba  yake kikosi cha kwanza na kuipa mabao ya kutosha Yanga kuelekea mbio za  ubingwa. Middie Kagere na Obrey Chirwa wana mabao manne kila mmoja,  ambayo hajafikiwa na Sarpong. 

Wafungaji wenye mabao manne ndio wa chini zaidi, akiwemo Sarpong.  Hapo ndipo linakuja swali, licha ya juhudi zake kuhakikisha timu inafunga  mabao na kuibuka washindi kwanini wastani wa upachikaji wa mabao  hauridhishi?  

Je, itatosha pekee Sarpong kubaki Yanga kwa vile anashughulika sana  kuhakikisha wanapata ushindi wakati katika mechi 15 amepfunga mabao  manne tu? Hayo ni baadhi ya maswali ya kujiuliza nafasi ya ushambuliaji  Yanga. 

Ni wazi kuwa Michael Sarpong anatakiwa kujirekebisha haraka. Wakati  anaanza kucheza Yanga kulikuwa na matumaini ila makubwa lakini kadiri  siku zinavyoenda ndivyo anavyozidi kupotea huku wenzake wanaiva akiwemo Yacouba Sogne na Deus Kaseke. 

Ujio wa Ntabanzokiza ni tishio na ujumbe kuwa uongozi wa Yanga  hauridhishwi na kasi ya upachikaji wa mabao. Sarpong amekuwa akikosa  muendelezo mzuri wa kupachika mabao. Mfano Mwadui FC imeruhusu  kufungwa mabao 28 msimu, hali ambayo ingekuwa rahisi kwa 

mshambuliaji huyo kutumia mechi hiyo kupachika mabao ya kutosha kwa  vile ni rahisi. Ushindi wa mabao 5-0 wa Yanga unamaanisha Mwadui  wameruhusu nyavu zao kutikisha mara 33 katika mechi 15 msimu huu. Unashindwaje kutamba na kupachika mabao ya kutosha mbele ya timu  dhaifu kama Mwadui ? 

Hapo ndipo linakuja suala la kuwekwa becnhi. Mchezaji wa nje anapokaa  benchi ni hasara kubwa kwa timu na yeye binafsi. Sarpong alipaswa  kutumia mechi ya Mwadui FC ndio kupiga mabao mengi hata kuibuka na  ‘hat trick’, lakini haikuwa hivyo. Sarpong kama sio kufunga kwenye mchezo  wa Mwadui basi alipaswa kutengeneza mabao matatu kwa wengine. 

Sarpong ili aweze kung’ara inabidi kocha Cedric Kaze ampunguzie  majukumu ya kuzunguka kutafuta mipira. Kazi ambayo anapaswa aifanye  ni kucheza katika eneo lake la ushambuliaji. Mchezaji kama Ntabazonkiza  anaweza kufanya kazi ambazo alikuwa anazifanya Sarpong basi itamsaidia  kung’ara. 

Kiufundi Sarpong sio mchezaji mbovu bali anashindwa kujua jukumu lake  la kwanza ni lipi kama mshambuliaji kiongozi. Sina uhakika kama Yanga  wataharakisha kumuondoa labda kama watampata mshambuliaji mwingine  mfano Meddie Kagere.  

Lakini marekebisho kwa Sarpong yanatakiwa kuwa pande zote; kwa  mwalimu Cedric Kaze kumuongezea maarifa na kumchorea eneo  analotakiwa kubaki, pili kumpa changamoto ya kupachika mabao ya  kutosha angalau 20 kwa msimu huu. Nje ya hapo haitashangaza kuona  Sarpong akiyakuta mabegi yake yakiwa uwanja wa ndege tayari kwa safari  ya kurudi kwao Burkinabe.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tuisila Kisinda

Tuisila Kisinda ‘TK Master’ zali la mawinga wa Yanga

Tanzania Sports

Huu ni mwisho wa utawala wa La Liga duniani?