in , ,

Samatta wa Ulaya

 

Mshambuliaji anayetesa na Tout Puissant Mazembe (TP Mazembe) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbwana Samatta, anadhaniwa atakuwa  Mtanzania wa tatu kukipiga katika klabu kubwa barani Ulaya.

Samatta yupo kwenye kiwango cha hali ya juu kwa muda sasa, ambapo alifunga mabao matatu dhidi ya Moghreb Tetouan wa Morocco na kuhakikishia klabu yake nafasi katika nusu fainali za Klabu Bingwa Afrika.

Hat-trick hiyo imekuja muda mfupi tu baada ya kuonesha kiwango kizuri kwenye mechi ya nyumbani baina ya Tanzania na Nigeria, ambapo Super Eagles walibanwa 0-0. Laiti mipangilio ya Watanzania ingekuwa vyema, wangeweza kuibuka na ushindi katika mechi hiyo ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2017.

Ni Watanzania wawili tu waliopata fursa ya kucheza soka katika ligi ya juu kabisa Ulaya, nao ni Renatus Njohole aliyefanikiwa kwa kiasi kikubwa akicheza nchini Uswisi na klabu ya Yverdon Sport kati ya 1999 na 2001.

Mwingine aliyechezea nafasi na anayefananishwa na Mario Balotelli wa Italia ni Haruna Moshi ambaye alipata anfasi kucheza klabu ya Gefle IF ya Sweden, lakini akaamua mwenyewe kuachia fursa hiyo na kurudi nyumbani akiwa katika umri ambao angeweza kufanya vyema.

Samatta aliyepata kuhusishwa na kuhamia klabu ya Urusi ya Spartak Moscow nusura apelekwe kwa mkopo klabu ya Lille ya Ufaransa msimu uliopita lakini dili likayeyuka. Japokuwa bado ana ndoto za kucheza Ulaya wakati ujao, anataka kuhakikisha kiwango chake kinakuwa endelevu akiwa na Mazembe na Taifa Stars.

Anasema haelewi kwa nini Tanzania haina wachezaji wengi barani Ulaya lakini anaona fahari kubwa anapopamba vyombo vya habari baada ya kusaidia klabu yake na timu ya taifa.

“Sielewi kwa nini hatuna wachezaji wengi Ulaya lakini naamini kwamba naweza kuwa mmoja wao huko. Kabla sijaja hapa (Kongo) si watu wengi walijua juu ya soka ya Tanzania lakini sasa mambo yanabadilika.

“Kama nchi hatuna wachezaji wengi ng’ambo kwa hiyo unapopata fursa ya kuchezea timu kubwa kama Mazembe kila mmoja anakuona na kutaka kukufahamu. Daima kuna shinikizo kwangu ili niifungie nchi yangu kwa sababu ndicho kitu ambacho hufanya hapa Mazembe, kwa hiyo nikienda nyumbani washabiki wanatarajia nifanye hivyo kule,” anasema Samatta.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Mazembe akitokea Simba miaka minne iliyopita na anasema kwamba anashukuru kwa kupata fursa ya kuchezea klabu iliyopata kuwa mabingwa wa Afrika mara nne.

Samatta anaeleza kwamba akiwa na klabu kubwa hiyo anajifunza mambo mengi na kama timu wamekuwa wakisaka ushindi kwa udi na uvumba, iwe nyumbani au ugenini na anasema ni Mazembe waliomsaidia kuvuka kutoka eneo moja kwenda jingine.

Mchezaji huyo aling’amuliwa na Patrick Phiri aliyewafundisha Simba mara kadhaa na anapoulizwa juu ya kijana wake huyo, Mzambia Phiri anasema hashangai kuona aking’ara hadi sasa, kwani alionesha tangu mwanzo kudhamiria kupata mafanikio.

Phiri anasema kwamba mchezaji huyo ana kipaji na amekuwa akikitumia vyema na kwamba walimsajili Simba walipokuwa na tatizo na washambuliaji, na katika mechi ya kwanza tu akafunga mabao matatu na baada ya hapo akaendeleza mserereko na kuonwa na wamiliki wa Mazembe waliomtwaa baadaye.

Phiri anaongeza kwamba tangu alipoanza kuchezea Simba, alikuwa wa kwanza kuingia uwanja wamazoezi kila siku, ambapo walikuwa wakianza mazoezi saa 12 asubuhi, lakini yeye alifika saa 11.30 hata kabla ya kocha.

“Nilikuwa namtumia kama mfano kwa wachezaji wengi. Ilikuwa kawaida kwangu kumkuta uwanjani maana alifika kabla ya wengine wote. Nikimuona leo nitampongeza sana kwa sababu ameshika yale niliyokuwa namshauri,” anasema Phiri aliyerejea Simba msimu uliopita kabla ya kutimuliwa kwa kiwango duni cha timu.

TP Mazembe awali ilijulikana kwa jina la Tout Puissant Mazembe  Englebert na mara ya mwisho kucheza Tanzania waliwanyuka Simba, ambao hadi leo wanawakumbuka kwa mbinyo wao unaowakosesha hamu ya kukutana nao tena.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TIMU YA WIKI EPL

Tanzania Sports

Diego Costa ashitakiwa