ROY KEANE AMNANGA ALEX FERGUSON

Nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane amesema kwamba kocha aliyeng’atuka katika klabu hiyo, Sir Alex Ferguson bado ana uchu wa madaraka.

Keane aliyeondoka baada ya kukosana na klabu hiyo na pia amekuwa akitupiana maneno na Fergie amedai kwamba Ferguson anatafuta nguvu za kimadaraka na kimamlaka ili adhibiti mambo Old Trafford.

Fergie alistaafu Mei mwaka huu na kumpendekeza raia mwenzake wa Scotland, David Moyes aliyekuwa Everton kuchukua nafasi yake, huku Fergie akiingia kwenye bodi kama mkurugenzi.
Tangu hapo Manchester United wamefanya vibaya kwenye ligi, ambapo sasa wanashika nafasi ya tisa baada ya kupoteza mechi tano, jambo ambalo si kawaida kwao.

“Kila kitu hapo Ferguson anafanya kwa ajili ya udhibiti na mamlaka,” anasema Keane aliyecheza hapo chini ya Ferguson tangu 1993 hadi 2005 akacheza mechi 326 kama mmoja wa viungo bora zaidi na akafunga mabao 33.

“Bado anapigania kupata mamlaka hadi sasa hivi ili awe na sauti kwenye timu japokuwa sio kocha tena – kuna ubinafsi mkubwa sana unaohusishwa hapa,” anasema Keane.

Mchezaji huyo wa zamani na mchambuzi wa masuala ya soka kwa sasa ni kocha msaidizi wa Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Ireland na anasema hawana tena uhusiano hata kidogo na Fergie.

Comments