in ,

RAPHAEL DAUD, NI NGUMU KUONA MAWIO KWENYE TAA ZA KARIAKOO

Ni sehemu ndogo tu iliyopo Dar-es-Salaam, lakini ni sehemu ambayo ina
umuhimu mkubwa sana hapa nchini, hapana shaka TRA hujivunia eneo hili.
Hata wafanyabiashara hulitukuza eneo hili, utajiri wao ulianzia hapa
na kukua hapa mpaka mitaani wakawa na heshima.

Hapana shaka ndilo eneo ambalo huwezi kuwa mchezaji wa mpira wa miguu
bila kukanyaga, wengi wa wachezaji wetu wanaota kukanyaga eneo hili.

Ni mchezaji gani atafikiria mara mbili mkataba wa Mbao FC na kuuacha
mkataba unaotoka kariakoo?

Ni shabiki gani wa mpira wa miguu hapa Tanzania asiyependa kushuhudia
timu za kariakoo zikija mkoani mwake?, hugeuka siku ya historia na
sikukuu kwa pamoja siku timu hizi mbili kutoka Kariakoo zinapofika
kucheza mechi mkoa fulani

Tiketi huuzwa kwa wingi tofauti na mechi nyingine isiyohusisha timu
moja wapo ya Kariakoo, wamachinga hutumia nafasi hiyo kuwaibia Yanga
na Simba kuuza jezi ambazo bila ruhusa.

Pamoja na kwamba jezi zinazouzwa siyo jezi halali kutoka ndani ya
vilabu hivi viwili vya kariakoo lakini mashabiki hununua kwa kiasi
kikubwa.

Kipimo cha mapenzi ya mashabiki hawa kwa vilabu hivi viwili ni kikubwa
mno, ndiyo maana hata mechi ya Simba na Yanga huwa ni sikukuu kubwa
sana hapa nchini.

Barabara hupambwa kwa magari yenye bendera za hizi timu, vijiwe vingi
vya kahawa hupeperusha bendera za hawa mahasimu wawili.

Biashara nyingi hufungwa mapema sana ili watu wapate nafasi ya kwenda
kushuhudia mechi hii, ndiyo siku ambayo maeneo ya starehe yanayouza
vinywaji baridi na moto hupata wateja wengi.

Masikio ya watu wengi huwa na shauku ya kusikiliza sauti ya mtangazaji
kwenye redio akitangaza goli. Hapo ndipo tambo huanza.

Tambo ambazo huzaa furaha na huzuni ndani ya hizi timu, hajawahi
kutokea shabiki akakubali timu yake ni mbovu mbele ya mpinzani wake
ndiyo maana ni kawaida watu kuwekeana nyumba ,pesa kwa ajili ya mechi
hii.

Burudani huwa inaendelea hata baada ya msimu kuisha, hapa napo kuna
ligi mpya huanza. Ligi ya usajili.

Kipindi hiki huwa tunashuhudia ni nani mwenye msuli mkubwa zaidi ya
mwenzake katika kuwania saini ya wachezaji nyota hapa nchini, na ni
ngumu kwa mchezaji kukataa ombi la kusajiliwa na hizi timu.

Wengi huamini ndoto yao ya kucheza mpira wa kulipwa huanzia hapa, hivo
kukaa kwenye timu hizi huwa ni njia rahisi kwao wao kupanda ndege.

Mwanzoni huja na matumaini mengi ndani yao, huja na nguvu na hasira ya
kupigana sana ili kufika mbali, lakini tatizo hufika pale tu
wanapokanyaga ardhi ya Kariakoo.

Ardhi ambayo kila wakati kuna mwanga , ardhi ambayo ni ngumu kutambua
mchana ni upi na usiku ni upi.Ardhi ambayo imejaa kila aina ya
starehe.

Ardhi ambayo imebeba wasichana warembo ambao mkoani ulipotoka hawapo,
ndipo hapo nguvu yako ya kupigana hupungua.

Malengo yako ya kufika mbali kimpira huanza kudidimia na kujiona
sehemu uliyopo ndiyo sehemu sahihi, ndiyo maana wachezaji wengi huja
pale wakiwa kama nyota sehemu waliyotoka lakini wanashindwa kuonesha
kitu walichokuwa nacho huko walipotoka.

Mbeya City msimu uliopita ilikuwa na Raphael Daudi ambaye alikuwa
kiungo imara tena uwezo wake ulinakshiwa na ufungaji wa magoli pamoja
na utoaji wa pasi za mwisho za magoli

Timu za kariakoo zilimtaka , lakini jangwani ilikuwa sehemu yenye
bahati kwake kufikia, lakini tangu afike hajaamka.

Kanogewa na kitanda cha ugenini, hataki kuamka ili atengeneze kesho
yake aliyokuwa anaitamani wakati yupo Mbeya City.

Kasi ƴyake iko polepole sana, hana njaa tena, kashiba pesa za usajili
hafikirii kupatumia jangwani kama sehemu ya yeye kwenda walipo kina
Simon Msuva.

Muda bado anao, hata hajachelewa cha muhimu ni sisi kumkumbusha tu
kuwa pale kariakoo kila wakati kuna mwanga ni ngumu kujua kama
pamekucha au ni usiku, vazi la utumwa ndilo vazi sahihi kwake ili
afanye kazi bila kusubiri jua kuchomoza.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Dondoo za kombe la Dunia….

Tanzania Sports

GHAFLA NIMEPAKUMBUKA GEZA ULOLE NA BUNJU ARENA