in , , ,

Ramsey wa Arsenal arejea

*Benteke nje kwa miezi sita

Kiungo Aaron Ramsey aliyewabeba Arsenal tangu mwanzo wa msimu hadi alipoumia Desemba 26 mwaka jana, anarejea uwanjani.
Ramsey (23) ni moja ya sababu za Arsenal kupanda hadi nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi, lakini mambo yalibadilika tangu kuumia kwake na wenzake wakiwamo Theo Walcott, Alex Oxlade-Chamberlain ambapo timu ilianza kuporomoka.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema nyota huyo ambaye msimu huu ameshafunga mabao 13 licha ya kuwa nje kwa mechi nyingi, atakuwa kwenye kikosi kinachosafiri kukabiliana na Everton kwenye dimba la Goodison Park Jumapili hii.
Mchezaji huyu wa Timu ya Taifa ya Wales alikuwa anasumbuliwa na nyonga, na aliumia wakati timu yake ikipata ushindi wa 3-1 dhidi ya West Ham. Wenger amesema kuwa na mtu kama Ramsey anayeweza kuisaidia timu ni muhimu sana.
Arsenal sasa wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 64 huku Everton wakiwafuatia kwa pointi 60 na bado wana mchezo mmoja mkononi. Liverpool wanaongoza ligi kwa pointi 71, Chelsea wana pointi 69 na Manchester City wanazo 67 na michezo miwili mkononi.
Nafasi ya sita inashikwa na Tottenham Hotspur ambao kama Everton wanagombea kuwapokonya Arsenal nafasi ya nne ili kuwa moja ya timu nne zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Spur wana pointi 56 hivyo bado wapo mbali.

BENTEKE NJE MIEZI SITA
Wakati Ramsey akirejea, Aston Villa wamepata pigo kubwa baada ya mpachika mabao wao, Christian Benteke kuumia mazoezini na imeelezwa kwamba hatacheza kwa miezi sita ijayo.
Benteke (23) aliumia kwenye mazoezi ya timu hiyo, na inamaanisha pia kwamba hataweza kuiwakilisha nchi yake ya Ubelgiji kwenye michuano ya Kombe la Dunia Brazil inayoanza Juni 12 mwaka huu.
Kocha wa Villa, Paul Lambert alisema habari hizo ni za kusikitisha sana kwa Benteke mwenyewe na klabu kwa sababu alihitaji na kuhitajiwa kucheza wakati huu kuliko mwingine wowote.
Benteke aliyezaliwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kabla ya kupata uraia wa Ubelgiji alijiunga na Villa Agosti 2012 kwa kitita cha pauni milioni saba akitoka klabu ya Genk ya Ubelgiji.
Msimu uliopita aliifungia timu yake mabao 23 kwenye mashindano yote lakini baadaye alitikisa kibiriti kuondoka kabla ya kupozwa na kukubali kubaki. Msimu huu amefunga mabao 11 tu na amekwenda miezi mine bila kufunga hata moja.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Robben: Man U kama mpira wa mikono

Wanasoka wadakwa kwa kupanga matokeo