in , , ,

RAIS MALINZI AELEZEA SIKU 100 ZA UTEKELEZAJI WA ILANI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameelezea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ilani yake siku 100 tangu alipoingia madarakani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo (Februari 7 mwaka huu) katika mkutano uliofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi aliainisha maeneo kadhaa yaliyopewa kipaumbele na tayari yameanza kufanyiwa kazi pamoja na changamoto zilizopo.

Alisema muundo wa Idara ya Ufundi umebadilishwa kwa kuundwa vitengo vya ufundi, elimu na maendeleo ya mpira wa miguu huku maeneo ambayo tayari yameanza kufanyiwa kazi kuwa ni;

Ujenzi wa kituo cha mpira wa miguu (football centre of excellency), timu kupanda daraja, kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani, mpira wa miguu wa wanawake, maandalizi ya vijana (grassroot football), tiba, walimu na makocha, utawala, uhusiano na Zanzibar, klabu za mpira wa miguu, wachezaji, masoko na uwekezaji, kitengo cha habari, viwanja na timu ya Taifa (Taifa Stars).

Rais Malinzi amesema changamoto zilizopo kwa sasa ni matumizi ya tiketi za elektroniki, ufinyu wa bajeti, madeni, nidhamu, maadili na uchezeshaji wa waamuzi.

Ametoa mwito kwa wadau wote nchini wakiongozwa na Serikali, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF), Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), vyombo vya habari, mashirika ya umma na kampuni binafsi kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa nia ya kuinua kiwango cha mpira wa miguu Tanzania. (TAARIFA NZIMA YA RAIS IMEAMBATANISHWA)

KILA LA KHERI YANGA, AZAM

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linazitakia kila la kheri klabu za Yanga na Azam ambazo timu zake zinatuwakilisha kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) na Kombe la Shirikisho (CC).

Yanga inacheza na Komorozine ya Comoro katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya CL itakayochezwa kesho (Februari 8 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Nayo Azam inaikaribisha Ferroviario de Beira ya Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya CC utakaochezwa Jumapili (Februari 9 mwaka huu) saa 10 kamili kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Ni matumaini yetu kuwa timu hizo mbili zitatuwakilisha vizuri kwenye michuano hiyo, na kuwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi viwanjani kuziunga mkono hasa kwa vile zinacheza nyumbani.

TWIGA STARS YAHAMISHIA KAMBI DAR

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) imehamishia kambi yake jijini Dar es Salaam kutoka Mlandizi mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya michuano ya Afrika (AWC) dhidi ya Zambia.

Kikosi hicho chini ya Kocha Rogasian Kaijage kimepiga kambi katika hosteli ya Msimbazi Center kikiwa na wachezaji 25 kutoka 30 ambao kilianza nao katika kambi ya Mlandizi mkoani Pwani.

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza dhidi ya Zambia itachezwa Februari 14 kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka. Timu zitarudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.

Wachezaji waliopo katika kikosi hicho ni Amina Ally, Amisa Athuman, Anastasia Anthony, Asha Rashid, Esther Chabruma, Eto Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fatuma Bashiri, Fatuma Hassan, Fatuma Issa, Fatuma Mustafa na Fatuma Omari.

Wengine ni Flora Kayanda, Happiness Hezron, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Najiat Abbas, Pulkeria Charaji, Shelder Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa, Winfrida Daniel na Zena Khamis.

PRISONS, RUVU SHOOTING KUUMANA SOKOINE

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 8 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting itakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi nyingine nne za ligi hiyo zitachezwa keshokutwa (Februari 9 mwaka huu) kwenye viwanja mbalimbali. Mgambo Shooting vs Simba (Mkwakwani, Tanga), Oljoro JKT vs Kagera Sugar (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers vs Coastal Union (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na Mbeya City vs Mtibwa Sugar (Sokoine, Mbeya).

FDL YAANZA VUMBI LA MZUNGUKO WA PILI

Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) unaanza kesho (Februari 8 mwaka huu) kwa mechi za kundi A na B wakati kundi C lenyewe litaanza mechi zake Februari 22 mwaka huu.

Mechi za kundi A ni Green Warriors vs Tessema (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Polisi Dar es Salaam vs Transit Camp (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam). Februari 9 mwaka huu ni African Lyon vs Villa Squad (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Friends Rangers vs Ndanda (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam).

Kundi B kwa kesho (Februari 8 mwaka huu) ni Polisi Morogoro vs Burkina Faso (Jamhuri, Morogoro), Lipuli vs Mkamba Rangers (Samora, Iringa), Kurugenzi vs Kimondo (Wambi, Mufindi) na Mlale JKT vs Majimaji (Majimaji, Songea).

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Simba avutwa sharubu Moro

Arsenal maumivu