in , , ,

Raila Odinga awapa ‘tano’ Arsenal

*Awafagilia wachezaji na kocha kwa kiwango
*Atapendekeza majina kwa usajili msimu ujao

Mwanasiasa na mfanyabiashara mashuhuri wa Kenya, Raila Odinga amewasifu Arsenal kwa kufanya vyema msimu huu kwenye Ligi Kuu ya England.

Katika makala yake aliyoandika kwa lugha ya Kiingereza, Odinga ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya na shabiki mkubwa wa Arsenal amesema kwamba washabiki wa Arsenal kote duniani watakubali kwamba maendeleo yao ni makubwa sana.

Odinga anasema kwamba kwa kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na kujihakikishia kuingia moja kwa moja kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao na kufika fainali ya Kombe la FA kunamfanya apate kigugumizi kueleza furaha aliyo nayo.

“Hii ni nafasi nzuri zaidi tuliyopata kushika katika misimu mitano iliyopita na ya pili kwa wingi wa pointi katika kipindi hicho. Ni msimu wa pili mfululizo pia Arsenal wanamaliza ligi mbele ya ile timu nyingine inayocheza pale Old Trafford (Manchester United),” anasema Odinga.

Mwanasiasa huyu anasema kwamba kushika nafasi ya tatu badala ya nne ni muhimu, kwani huondoa shinikizo kwa timu katika maandalizi yake ya kiangazi kuendea msimu mwingine, ambapo hakuna mechi za mtoano. Kadhia hiyo wameachiwa Manchester United.

Odinga anasema kwamba uendelevu katika mafanikio wa kocha Arsene Wenger unahitaji kupewa msisitizo wa aina yake katika miaka 17 ambayo amekuwa akimaliza katika nafasi nne za juu na walau kufika hatua ya mtoano ya UCL.

“Tukiwa na msingi huu, washabiki wengi wanaona kuna kila sababu ya kuwapokonya Chelsea kombe msimu ujao baada ya kusubiri kwa zaidi ya muongo mmoja. Msimu huu mafanikio yamechangiwa na mengi, ikiwa ni pamoja na kuwa na kikosi shindanishi,” anasema Odinga aliyepoteza mbio za urais kwa Uhuru Kenyatta.

Anasema kunasa wachezaji kama Alexis Sanchez kutoka Barcelona msimu uliopita, Mesut Ozil na kwa namna ya pekee anawataja Olivier Giroud, Aaron Ramsey, Danny Welbeck, Santiago Carzola na Alex Oxlade Chamberlain, anaosema wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ufungaji na utengenezaji fursa za kufunga mabao.

“Hii ikichangiwa na kurejea uwanjani kwa Theo Wacott na Jack Wilshere tuna uhakika wa kuwa na kikosi imara zaidi tunapoelekea Agosti kuanza ligi ya msimu ujao. Ngome yetu imeimarika sana, ambapo kati ya wengine, Calum Chambers na Hector Bellerin wamethibitisha ubora wao.

“Wawili hawa pamoja na kijana wa Samba aliyesajiliwa, Gabriel Paulista wataongeza nguvu kwa Laurent Koscielny na Per Mertesacker na pia watakuja kuziba mapengo yao misimu inayokuja,” anasema na kuongeza kwamba Francis Coquelin amefanya kazi kubwa kwenye kiungo cha ukabaji tangu arejeshwe kutoka Charlton Desemba alikokuwa kwa mkopo.

Odinga anaongeza kuwa, pamoja na sifa alizotoa, panahitajika kusajiliwa wachezaji kadhaa ili kuwapaisha zaidi nyumbani na UCL, akisema kwenye ushambuliaji Wenger anatakiwa kusajili mpachika mabao asiyeumia mara kwa mara.

“Watu kama Karim Benzema (Real Madrid), Jackson Martinez (Porto), Edinson Cavani (PSG) au Gonzalo Higuain (Napoli), ambao kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari wanaweza kupatikana ndio wanaogonga kichwani.

Anasema Coquelin anahitaji ushindani kwenye nafasi yake, ambao haoni kwamba utatoka kwa ama Mikel Arteta wala Mathieu Flamini, bali ama wamchukue nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama au Mfaransa Morgan Schneiderlin watakaofanya kazi nzuri.

Anasema kufikiria kusajili mtu kama Paul Pogba ni anasa isiyostahili na kwamba akiingia itakuwa mwisho wa akina Carzola, Ozil au Walcott. Anasema ngome yao ingekuwa bora zaidi ikipata watu kama Mats Hummels wa Borrusia Dortmund na ama Marcelo wa Real Madrid au Jordi Alba wa Barcelona.

Kuhusu golini, anasema ingefaa wakamsajili Petr Cech wa Chelsea anayetaka kuondoka Stamford Bridge. Hata hivyo, anasema kwamba matarajio baada ya kusema hivyo ni wapinzani wao kukosa usingizi mara nyingi, wakati Arsenal wakiimba ‘In Arsene We Trust’.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
kaseke.

Simba, Yanga waanza usajili

Drogba, Falcao kwaheri