Toure mwanasoka bora Afrika

Kiungo wa Manchester City, Yaya Toure amechaguliwa kuwa mwanasoka bora wa Afrika kwa mara ya nne.

Mchezaji huyu raia wa Ivory Coast, ametangazwa kuibuka katika nafasi hiyo na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), akiweka rekodi mpya.

Toure (31) amepewa ushindi huo baada ya kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa klabu yake kutwaa ubingwa wa England na pia kutwaa Kombe la Ligi. Amewasaidia Ivory Coast pia kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2015.

Kiungo huyu aliwapiku mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang na kipa wa Nigeria, Vincent Enyeama. Toure amefunga mabao 20 kwa City katika kampeni zao za ubigwa na pia alifunga bao la kusawazisha kwenye mechi ya fainali ya Capital One Cup dhidi ya Sunderland, City wakaja kushinda 3-1.

Kwa msimu huu amefunga mabao sita katika mechi 26 za mashindano yote, yakiwamo mabao sita kwenye mechi za ugenini. Mwaka jana aliorodheshwa miongoni mwa wachezaji wa kuwania mchezaji bora wa dunia katika hatua za mwanzo, lakini akachujwa.

Aliendelea na mechi za fainali za Kombe la Dunia mwaka jana, licha ya kupewa habari za kifo cha mdogo wake, ambaye pia alikuwa mwanasoka, Ibrahim Toure. Alipamba vichwa vya habari juu ya sakata la kutopewa keki ya siku yake ya kuzaliwa wala salamu kutoka kwa mabosi wa Man City, akatishia kuhama.

Mshambuliaji wa Everton, Samuel Eto’o ndiye mwanasoka pekee wa Afrika aliyepata kutwaa tuzo hiyo mara nne, lakini nayo haikuwa mfululizo, tofauti na Toure.

Posted under:  

Tags:  ,

Comments