Tanzania Yaenda Urusi kwa Riadha Dunia

Bendera ya Taifa la Tanzania inatarajiwa kupeperushwa katika mashindano ya dunia ya mchezo wa riadha, yanayofanyika nchini Urusi.
Chama cha Riadha Tanzania (RT) kinasema kwamba wanariadha wake wanajiandaa kwenda huko, baadhi wakiwa ni wale walioshiriki kwenye Michuano ya Olimpiki jijini London, Uingereza hivi karibuni.
Wanaobeba jina la Tanzania huko ni Mohamed Msenduki, Faustine Musa, Daudi Joseph na Zakia Mrisho ambao kwenye Olimpiki hawakuambulia medali.
Mashindano haya yanaanza Julai 10 na yataendelea hadi Julai 17, yakienda sambamba na michezo mingine. Hata hivyo, RT kama kawaida, wanasema hawana rasilimali fedha, hivyo wanawaomba wadau kujitolea kuwadhamini ili kufanikisha ushiriki wa wachezaji hao.
Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui anasema kwamba mazoezi si tatizo kwa wanaridha hao, kwa vile wapo katika mazingira ya kupata mafunzo makazini mwao, hivyo isiwape shida wadau, kwa vile baadhi ni wanajeshi.
“Najua hii ni kama timu ya taifa inaenda huko kushiriki, hivyo ni vema ikahakikishiwa ushiriki wao unakuwa mzuri na kutuletea medali, sasa ili hayo yafanyike basi tuiunge mkono,” alisema Nyambui na kuongeza kwamba mara ya mwisho mashindano hayo kufanyika ilikuwa 2009 nchini Ujerumani.

Klabu Bingwa Netiboli Mbeya

Wachezaji wa netiboli nchini Tanzania wanatarajiwa kupata changamoto kubwa, kwa sababu Klabu Bingwa ya Netiboli inaandaliwa mkoani Mbeya, na kila timu ingependa kulitwaa taji hilo.
Soka imekuwa ikipewa kipaumbele na wadau wengi wa michezo, lakini sasa lazima kugeukia michezo mingine ambayo kuna watu wanaoipenda, na pia baadhi ya wanamichezo wameonesha kuwa na uwezo nayo.
Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kinaandaa mashindano hayo kwa kushirikiana na Chama cha Netiboli mkoa wa Mbeya, ambapo mashindano yenyewe yatatikisa jiji la Mbeya kuanzia Agosti 24 hadi Septemba 7.
Kama ilivyo kwa klabu za soka zilizo kwenye pilika pilika za usajili, klabu za netiboli nazo zinaingia kwenye usajili wa wachezaji, na mwisho wa dirisha lenyewe ni mwisho wa mwezi Julai. Wanatakiwa kusajili wachezaji wa nje wasiozidi watatu.
Mashindano hayo, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHANETA, Anna Kibira, yatakuwa jukwaa na fursa nzuri za kuiimarisha timu ya taifa, kwa kuangalia iwapo wachezaji waliopo wanafaa au waongezwe wengine watakaowika.
Kama ilivyokuwa kwenye wanariadha wanaokwenda Urusi, CHANETA inaomba wafadhili ili mashindano hayo yaende kama yalivyopangwa. Klabu nne za juu zitashiriki mashindano ya Ligi ya Muungano wa Tanzania, yaani Tanzania Bara na Zanzibar.
Timu za netiboli zinazowika nchini ni pamoja na JKT Mbweni, Jeshi Stars, Uhamiaji, Bandari, Filbert Bayi, Magereza Morogoro, RAS Lindi, Hamabe Mbeya.Magereza Dare s Salaam, Magereza Arusha, Magereza Mwanza, Magereza Mbeya, Mapinduzi Dodoma, Tamisemi, Tumaini na Temeke Queen.

Posted under:  

Tags:  ,

Comments