Simba kimenuka


*Wapigwa 3-2 na JKT Ruvu, Azam sare
*Yanga wameung’ang’ania uongozi wa ligi

Wekundu wa Msimbazi – Simba wameshindwa kuchanua baada ya kushindwa kwata la maafande wa JKT Ruvu na kulala kwa mabao 3-2.

Katika mechiiliyopigwa Uwanja wa Taifa Jumapili hii, hadi nusu ya kwanza inamalizika Mnyama alikuwa akilia kwa mabao 2-0 yaliyopachikwa na Hussein Bunu na Emmanuel Swita.

Simba waliendelea kusuasua kipindi cha pili kwa kukubali bao la tatu, mfungaji akiwa tena Swita lakini Simba wakamrudi Amisi Tambwe aliyefunga mabao mawili, moja kwa penati na jingine akiunganisha majalo ya Amri Kiemba, lakini hayakutosha kuwapa ushindi wala sare.

Azam nao walishindwa kufurukuta vilivyo mbele ya maafande wa Prisons wa Mbeya, na kwenda nao sare ya 2-2.

Katika mechi ya Azam, Kipre Tchetche alizawadiwa kadi ya pili ya njano, kisha nyekundu katika dakika ya 58 na kuwafanya Azam kucheza pungufu.

Prisons walikuwa kwenye eneo la kushuka daraja, lakini kwa mechi tatu zilizopita wamebadilika na kushinda, na hata sare hapo Azam Complex ni pointi muhimu sana kwao.

Matokeo ya Jumapili hii yanamaanisha kwamba Yanga ambao ni mabingwa watetezi wanabaki kileleni kwa kuwa na pointi 38, Azam wakifuatia kwa pointi 37 huku Mbeya City wakiwa wa tatu kwa alama zao 35. Simba ni wa nne na mkusanyiko wao wa alama 32.

Posted under:  

Tags:  , , , , ,

Comments