Ronaldo Mwanasoka Bora

Ronaldo Mwanasoka Bora tena

Kwa mara ya pili mfululizo, mchezaji wa Real Madrid na Timu ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo amechaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia.
Ronaldo amewapiku washindani wenzake wawili kwenye Ballon d’Or, ambao ni Lionel Messi wa Barcelona na Argentina na kipa Manuel Neuer wa Bayern Munich na Ujerumani.

Ronaldo (29) amepata asilimia 37.66 ya kura zote na hii ni mara ya tatu anashinda tuzo hiyo. Messi aliyepata kuitwaa mara nne alipata 15.76%, akimzidi kidogo tu Neur aliyepewa 15.72%.

Ronaldo aliyefunga mabao 52 katika mechi 43 mwaka jana, alionekana mwenye hisia kali wakati wa kupokea tuzo yake kutoka kwa mchezaji wa zamani wa Arsenal, Barcelona na Ufaransa, Thierry Henry.

“Ningependa kuwashukuru wote walionipigia kura, rais wangu, kocha wangu na Real Madrid, umekuwa mwaka ambao hautasahaulika. Kutwaa tuzo hii hatimaye ni kitu cha pekee kabisa,” akasema Ronaldo.
Kiungo wa Real Madrid na Colombia James Rodriguez ametuzwa kwa kufunga bao zuri zaidi kwa 2014 wakati Kocha wa Ujerumani, aliyetwaa Kombe la Dunia, Joachim Low ametangazwa kwua kocha bora wa dunia.
Washindani wale watatu wa Ballon d’Or wamejumuishwa kwenye Timu ya Dunia, pamoja na mabeki Philipp Lahm, David Luiz, Thiago Silva na Sergio Ramos.
Viungo wa kikosi cha dunia ni Andres Iniesta, Toni Kroos na Angel Di Maria wakati mshambuliaji mwingine ni Arjen Robben.

Posted under:  

Tags:  ,

Comments