Man City waendeleza mafuriko


*Kibarua cha Sam Allardyce hatarini

Manchester City wamerejea kugawa dozi zisizo za kawaida, ambapo katika nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Ligi wamewachakaza West Ham 6-0.

City wanaofundishwa na Manuel Pellegrini walipata mabao yao kupitia kwa Alvaro Negredo aliyefunga hat-trick (matatu) na mengine kupachikwa na Edin Dzeko mawili na Yaya Toure moja.

Wakicheza nyumbani, City walionesha kuelewana tangu mwanzo na hivyo kumweka Kocha wa West Ham, Sam Allardyce ‘Big Sam’ katika wakati mgumu.

West Ham wapo kwenye eneo la kushuka daraja ambapo msimu huu hawajafanya vyema licha ya usajili wa wachezaji kama Andy Carroll ambaye hata hivyo ametokea kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Allardyce amepata kipigo hicho kikubwa mara ya pili ndani ya wiki moja baada ya kupokea kichapo cha 5-0 kwenye mechi ya Kombe la FA raundi ya tatu dhidi ya Nottingham Forest.

Wamiliki wenza wa West Ham, David Gold na David Sullivan walitangaza kuendelea kumuunga mkono kocha huyo hata baada ya kichapo kutoka kwa timu hiyo ndogo Jumapili iliyopita.

Hata hivyo, kwa kichapo hiki kikubwa zaidi kama walichopata Tottenham Hotspur kiasi cha kumfukuza kocha wao, Andre Villas-Boas, inaelekea sasa hali itakuwa ngumu kwa Big Sam.

Mashabiki wa West Ham tayari wametoa ujumbe tofauti dhidi ya bosi wao wakitaka atafakari kama anatosha bado kwenye nafasi aliyo nayo.
Sullivan alikuwapo uwanjani na alisikia kelele za mashabiki dhidi ya mteule wake huyo. Watarudiana katika nusu fainali ya pili Januari hii na ilishangaza kuamini kama West Ham hawa ndio waliowafunga Manchester United, mahasimu wa City.

Posted under:  

Tags:  , , ,

Comments