MADOLA

MWENDESHA baiskeli wa kimataifa, Richard Laizer ameng’ara michuano ya kimataifa iliyoandaliwa na Shirikisho la Mbio za Baiskeli za Kimataifa (UCI) nchini Ufaransa baada ya kushinda nafasi ya tatu.

Akizungumza jana Laizer alisema alishinda nafasi tatu kati ya waendesha baiskeli 56 waliyoshiriki michuano hiyo iliyofanyika juzi (Jumatatu) akitanguliwa na Mfaransa na Mjerumani na kutunikiwa kombe la shaba.

Mchezaji huyo wa klabu ya Arusha anayeichezea timu ya MTN Qhubaka Feeder Team Pro ya Afrika Kusini ameweka kambi ya miezi mitatu nchini Switzerland ambayo imeandaliwa na UCI wakati huo akitarajia kushiriki michuano ya kimataifa inayoandaliwa na shirikisho hilo kila wikiendi nchini Ufaransa, Italy, Hispania, Ujerumani na Switzerland.

“Siku za kawaida tunaendelea na mazoezi nchini Switzerland na inapofika Ijumaa jioni tunaenda katika nchi itakayoandaa mashindano hayo ambako tutashindana Jumamosi na Jumapili ambapo Jumatatu tunarudi Switzerland kuendelea na mazoezi,” alisema.

Laizer ni mmoja wa wanamichezo watakaoliwakilisha taifa katika michuano ya Jumuiya ya Madola ambayo inatarajia kutimua vumbi Julai 23 hadi Agosti 3 mwaka huu mjini Glasgow, Scotland.

Anatarajia kwenda nchini Scotland akitokea Switzerland mara tu michuano ya Madola itakapoanza na ikimalizika atarejea tena nchini Switzerland ambako atakaa hadi Septemba 15 mwakani.
NDONDI

WACHINA wamewazawadia seti za vifaa vya mazoezi mabondia waliokuwa wameweka kambi nchini humo kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Jumuiya ya Madola.

Akizungumza jana Kocha mkuu wa timu hiyo, Hassan Nzonge alisema kila bondia amepewa ‘gloves, gumsheet, headguard na pad’ kama zawadi.

Nzonge alisema zawadi hiyo itapunguza tatizo la uhaba wa vifaa linaloikabili timu ya taifa ambayo imekuwa ikifanya mazoezi kwa kupokezana vifaa.

“Japokuwa vifaa hivi ni mali ya bondia mwenyewe lakini watalazimika kutumia katika mazoezi yote ya timu ya taifa na kupunguza utengemezi wa vifaa vichache vinavomilikiwa na Shirikisho la ngumi za ridhaa la taifa (BFT),” alisema.

Nzonge alisema katika kambi hiyo kila bondia aliweza kutumia vifaa vyake kutokana na nchi ya China kuwa na vifaa vingi kuliko mabondia waliopo katika kambi ya taifa.

Aliongeza kuwa, “Mabondia wote waliweza kufanya mazoezi kwa wakati kulingana na ratiba iliyokuwa imepangwa tofauti na ilivyikuwa hapa nchi ambapo walilazimika kusubiriana kutokana na uchache wa vifaa,”
 

Posted under:  

Tags:  , ,

Comments