LIGI YA MABINGWA ULAYA

*Liverpool na Real Madrid, Arsenal na Dortmund tena
*Chelsea kundi mchekea, Man City na Bayern Munich

 
Wakati Cristiano Ronaldo amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ulaya, timu ya Liverpool imepangwa kundi moja na Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).

Liverpool waliopata kutwaa kombe hilo mara tano watakabiliana na mabingwa wa Ulaya – Real-  ikiwa ni mara ya kwanza katika miaka mitano Liverpool wanafuzu, baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).

Pamoja nao kwenye kundi hilo, ni FC Basel ya Uswisi ambao wamekaa vizuri pia na walipata kuwapelekesha Chelsea, huku wengine ambao hawapewi uzito lakini wanaweza kufanya maajabu ni Ludogorets wa Bulgaria.

Mabingwa wa England, Manchester City watakabiliana na Bayern Munich kwa mara ya tatu katika misimu minne, na kundi lao lina timu nyingine za CSKA Moscow wa Urusi na Roma wa Italia.

Arsenal watakumbana na Borussia Dortmund wa Ujerumani, ikiwa ni msimu wa pili mfululizo wakati Chelseawapo kundi mchekea, wakiwa na Schalke wa Ujerumani, Sporting Lisbon wa Ureno na Maribor wa Slovenia waliowatoa Celtic wa Uskochi kwenye mechi za kufuzu hivi karibuni.
photo00000

Ofisa utawala mkuu Chelsea, David Barnad amenukuliwa akisema kwamba Jose Mourinho alimtumia ujumbe kumwambia kwamba alifurahishwa na droo ilivyopangwa, akisema kwamba hakutana kuwa kwenye kundi moja na timu za England.

Arsenal waliofuzu kwa msimu wa 17 mfululizo baada ya kuwapiga Besiktas wa Uturuki 1-0, wapo pia na Galatasaray wa huko huko Uturuki na Anderlecht wanaotoka Ubelgiji.

Ofisa utawala wa Arsenal, David Miles amesema wanawajua vyema Dortmund na wanatarajia watavuka hatua ya makundi na lengo lao ni kumaliza wa kwanza kwenye kundi lao.

Mkurugenzi wa Soka wa Manchester City, Txiki Begiristain amedai kwamba lao ndilo kundi la kifo, akikumbukia msimu uliopita walivyoshika nafasi ya pili nyuma ya Bayern na akasema wapinzani wao wote wanacheza soka nzuri, hivyo kazi itakuwa ngumu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Liverpool Ian Ayre amesema kwamba ni wazi watakuwa na kazi ngumu lakini akasema hawangekuwa huko kama haingekuwa kazi ngumu, akiongeza kwamba ndizo changamoto za soka na kwamba wakati mwingine zina raha yake na kuwa wamejiandaa vyema kwa yote yaliyo mbele yao.

“Ni kundi linalovutia, ndiyo mashindano yetu haya, tumekuwa mabingwa mara tano na tulipata kuwa na usiku wenye furaha dhidi ya timu kama Real Madrid,” akasema akikumbukia walipowatandika Real 4-0 kabla ya kuwafunga tena 1-0 kwenye marudiano.

Wakati hayo yakijiri, mchezaji wa zamani wa Manchester United ambaye sasa anakipiga Real Madrid, Ronaldo ametangazwa kuwa mchezaji bora wa Ulaya katika droo iliyofanyika Monaco, Ufaransa.
Ronaldo ambaye ni mchezaji bora wa dunia pia, alisema anafurahishwa na kutambuliwa kwake huko baada ya kuwapiga kumbo Arjen Robben na Manuel Neur wa Bayern Munich waliokuwa wamefuzu kwenye hatua hiyo ya mwisho.

Ronaldo alisema kwamba anasubiri kwa hamu kupambana na Liverpool, maana hajapata kufanya hivyo akiwa na Real na kubwa kwake ni kuwapiga Liverpool, aliyosema ni timu nzuri. Hata hivyo, alisema anafurahia kundi lao na Real watafanya vyema.

Posted under:  

Tags:  ,

Comments