in , , ,

KUNA UMUHIMU WA KUWA NA SHINETA BADALA YA CHANETA

ENZI za miaka ya 1980 kurudi nyuma, Tanzania ilikuwa juu mno kwenye mchezo wa mpira wa pete, zaidi ukiitwa mchezo wa netiboli. Chama cha mchezo huo, Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), wakati huo kilisimamia vizuri mashindano mbalimbali makubwa ya mchezo huo yakiwemo mashindano ya mikoa. Hii ilikuwa dosari kubwa kwa maendeleo ya mchezo huo kwani CHANETA ilikuwa inasimamia matunda ya vipaji ambavyo hawakujishughulisha kupanda mimea yake, hawakuwa na mikakati ya kuyatunza  matunda hayo na wala hawakujipanga matunda hayo yakiisha, mengine yatapatikana vipi!

Watu walicheza netiboli kwa ushindani mkubwa kutoka kwa wachezaji wa timu kama Bora, Bandari, Bima, JKT Mbweni, JKU Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje, Polisi, Uhamiaji na nyinginezo ambapo nyingi zilikuwa za taasisi na zilikuwa Dar es Salaam. Hakukuwa na timu za wanachama huku mikoa ikiwa na uchache wa timu za mchezo huo. Wachezaji wa timu za mikoa walikusanywa toka sehemu mbalimbali au toka timu moja pekee iliyokuwepo na si toka timu za kueleweka za idadi fulani. Kwa msingi huo kulikuwa hakuna ligi yoyote ya timu mikoani,timu moja au mbili mkoa mzima zitachezaje ligi? CHANETA haikufanya lolote kukabili hali zote hizo bali ilikuwa mwandaaji na msimamizi tu wa mashindano ya kitaifa.
Angalia,leo CHANETA inajiandaa kwa uchaguzi wake wa taifa,inawahimiza wanachama wake kulipia ada zao ili waendelee kuwa hai ili wapate uwezo wa kikatiba ya CHANETA kushiriki kuchagua na kuchaguliwa. Wanachama hawa ni nani? Eti ni mtu mmoja mmoja na si vyama vya mchezo huo vya mikoa! Huu ni mfumo usio madhubuti kabisa na nadiriki kuuita wa kizamani. Kwanza, inasikitisha kwa mtu kutojisikia kuwa mwanachama wa chama fulani isipokuwa tu anapotazamia maslahi fulani. Inakuwaje mtu akawa mwanachama mfu lakini akalazimika kujifufua kwa  ajili ya kupata jambo fulani kama kupiga kura au kupigiwa kura kwa kesi hii ya uanachama wa CHANETA?
Ni muhimu sana sasa kwa CHANETA kujiua rasmi kutoka uhai ilio nao wa kuwa Chama Cha Netiboli cha Taifa na kujiumba upya katika uhai mpya wa kuwa Shirikisho la vyama vya mchezo wa netiboli vya mikoa yote ya Tanzania Bara (Zanzibar kuna CHANEZA). Kwa kuondoa wingi wa maneno, Shirikisho hilo jipya linapaswa liitwe Shirikisho la Netiboli la Taifa (SHINEZA) na wanachama wake wawe vyama vya mchezo huo vya mikoa.
Hivyo vyama vya mikoa vinapaswa vipewe majukumu maalum ya kutekeleza kwa kila mkoa kama jinsi ya na mahali pa kuwapata wachezaji chipukizi wa netiboli, uhamasishaji wa kuanzishwa timu nyingi za mchezo huo mikoani ambapo timu hizo zinapaswa ziwe na timu za marika tofauti, uanzishwaji wa ligi za mikoa za kupata mabingwa wa mikoa kwa mashindano ya marika tofauti.
Aidha, mikoa ihusike kusajili timu za maeneo hayo na usajili huo uwe wa masharti maalum ili kuepuka jambo baya kama lililoitokea timu kubwa na maarufu ya Bandari mwezi Oktoba mwaka jana pale Mamlaka ya Bandari ilipoizuia timu hiyo kwenye dakika ya mwisho kabisa isishiriki mashindano ya kitaifa huku ikiwa imashakamilisha taratibu zote za kushiriki mashindano hayo! Hilo  lisingetokea kama CHANETA ingejenga mfumo imara wa usajili wa timu zake ikitoa masharti maalum ya utekelezaji. Usajili huo ungefanywa kuanzia ngazi za chini ya ngazi ya taifa.
Ni jambo la kufurahisha sana kwamba licha ya mchezo wa netiboli kuonekana kama uko chini kwa sasa, timu yetu ya taifa mwaka jana mwezi Desemba ilishiriki mashindano ya mataifa sita yanayojulikana kama “Netball Nations Cup” huko Singapore ikipambana na wenyeji Singapore, Malaysia, Sri Lanka, Jamhuri ya Ireland na Namibia. Bila kujali kupewa nafsi ndogo kihabari (small coverage), Tanzania ilibeba kombe na haikushangaza kwa timu hiyo kupata mapokezi duni licha ya jambo hilo kubwa walilolifanya. Sababu ni kwamba mwamko wa mchezo huo umeshuka nchini tofauti na ilivyokuwa miaka ya 1980 kurudi nyuma.
Kama sasa hivi bila mikakati yoyote timu yetu ya netiboli inafanya makubwa hivyo, itakuwaje uongozi wetu wa mchezo huo ukijipanga vizuri na kuhakikisha mchezo huo unainuka,kubaki huko huko juu na kuendelea kupanda na kupanda? Jambo jingine la kusisimua ni kwamba Tanzania imepanda kwenye msimamo wa mwisho hadi sasa wa viwango vya mchezo huo duniani toka nafasi ya 19 mpaka ya 17 ikiwa ya nne barani Afrika. Imeziruka nchi maarufu kadhaa kwa mchezo huo kama ifuatavyo na nafasi zao kwenye mabano:-  Ireland (29), Singapore (19), Malaysia (24), Switzerland (33), Namibia (26), Zambia (23), Sri Lanka (22) and USA (18).
Hii inaonesha jinsi tulivyo na vipaji vikubwa vya mchezo huo vya kina nahodha Lilian Sylidion na kina Mwanaidi Hassan lakini hakuna mkakati imara wa kuvivumbua, kuviendeleza na kuvilinda vipaji hivyo kwa kukosekana kwa mfumo wa kuendesha mchezo huo toka ngazi ya chini. Kwa bahati mbaya sana sasa hivi vijana wa kiume wanahamasika kucheza mchezo huu ambao hasa ni wa kike huku wasichana wakihamasika kucheza soka ambayo kwa sasa karibuni ni ya wote, wanaume na wanawake. Katika mazingira haya, uongozi wa mchezo wa netiboli wa nchi yetu unapaswa ujizatiti kweli kweli kuwainua kinadada wetu katika mchezo huo Tanzania nzima. Hilo litawezekana tukihama toka kwenye u-CHANETA na kwenda kwenye u-SHINETA.
                              

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

70 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Pauni milioni 120 zatumika usajili

KUNA UMUHIMU WA KUWA NA SHINETA BADALA YA CHANETA