in , , ,

Klabu zetu za soka ziwe na mipango inayotekelezeka..

*Viongozi wanachonga sana, vitendo haba!

*Vilabu vinashindwa nini kuwa na maduka ya kuuza vifaa vyao?

*Udhamini wa makampuni na mabenki ni mkubwa michezoni

 

MFUMO wa uendeshaji wa mambo nchini Tanzania unarudisha nyuma maendeleo yake kutokana na kuwa na dosari mbili kubwa zinazohusiana. Kwanza, mfumo huu umekosa utekelezaji wa mambo wa namna moja kuhusu jambo moja na pili mfumo huu unatangaza hatua za utekelezaji si kwa mipango ya kitaasisi bali kwa kufuata matashi ya anayeongoza eneo fulani la utendaji.

Dosari hizi zinaturudisha nyuma katika mipango mingi ikiwemo ya michezo inayohusu mjadala huu. Nitakupa mifano michache nikianza na mambo mengine. Nchini mwetu sasa hivi kimfumo utaona Balozi wetu mmoja akishtakiwa kwa ubadhilifu wa fedha baada ya kununua nyumba ya ubalozi kwenye nchi anayotuwakilisha lakini kwa bei ya kutia shaka. Hapa tuhuma ipo na nyumba iliyonunuliwa ipo.

Udhamini wa Mabenki (NMB) katika kukuza michezo vilabuni, na taasisi nyingine Nchini.

Afisa wa Benki Kuu anashtakiwa kwa ujenzi wa majengo ya minara miwili ya benki hiyo kwa gharama ya kutia shaka. Tuhuma ipo na majengo ya minara ipo. Tatizo linakuwepo pale Afisa wa Wizara ya Mambo ya nje ya nchi anapotuhumiwa kuiba pesa kwa kuandaa safari hewa za nje za Rais lakini hashtakiwi! Hapa tuhuma ipo lakini safari za nje za Rais hazipo. Huyu hashtakiwi licha ya kwamba hana cha kuonesha kwa fedha anazotuhumiwa kuiba tofauti na Balozi yule na Afisa yule wa Benki Kuu walioshtakiwa licha ya kuwa na vitu vya kuonesha kwa fedha waliyotuhumiwa kuiba!

Hapa kwetu sasa mtu anaweza kushambuliwa na watu wengine akang’olewa kucha, meno na kutiwa chongo lakini hakuna ukamataji wowote unaofanywa huku wengine wakitendewa jambo lisilo la hatari kama hilo, msako wa watuhumiwa huwa si wa kawaida na watuhumiwa hao kukamatwa mara moja!

Sasa hivi hata ajira za nafasi kubwa kwenye taasisi za umma hutegemea zaidi matashi ya wanaoongoza taasisi hizo. Wale wanaopewa nafasi hizo kiujamaa nao huanza kupangua watu wenye ujuzi na uzoefu wa nafasi hizo kupachika watu wao kiujamaa bila kujali weledi na hilo huteremka mpaka chini. Miaka kadhaa ijayo, taasisi za umma zitakuwa hoi kabisa kwa kukosa watu wa kutosha wenye weledi! Hii ndiyo Tanzania na mfumo wake huo wa kuua maendeleo.

Haya ni matokeo ya kuwepo nchini mwetu kwa mfumo huu unaokosa utekelezaji wa mambo wa namna moja kuhusu jambo moja na unaochukua hatua za utekelezaji si kwa mipango ya kitaasisi bali kwa kufuata matashi ya anayeongoza eneo fulani la utendaji. Mfumo huu ndiyo unaoathiri maendeleo ya soka yetu yenye kielelezo cha Yanga na Simba.

Klabu hizi zimeibuka kila mara na mikakati kadhaa ya utekelezaji ambayo haimo kwenye maandishi yoyote ya kuheshimiwa na yeyote atakayekuwa madarakani wakati wowote. Kwa Yanga kwa mfano, kila mara utasikia mikakati mipya mpaka unapata kizunguzungu. 1.Kuanzia sasa kambi ya Yanga itakuwa makao makuu tu mtaa wa Twiga na Jangwani na hilo litafanywa kwa kuboresha makazi klabuni hapo ili yawe na hadhi ya hoteli fulani kubwa. Mara utasikia timu iko kambini hoteli hii na ile. Mpango wa Twiga na Jangwani hamna. 2. Tunaaanza kuujenga uwanja wa Kaunda kwa kuweka majukwaa ya kukaa watazamaji 30,000 (nusu ya wale wa Uwanja wa Taifa!) 3. Kaunda haijaanza kujengwa, mara tunasikia ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Mtaa wa Twiga na kamati imeundwa. 4. Vita vinatangazwa kwa wanaotumia nembo ya Yanga kujitajirisha kuacha mara moja au hatua za kisheria zitachukuliwa. Tunaendelea kuuziwa vifaa vya Yanga kama jezi, fulana, tracksuits na kofia na watu wakitengeneza pesa kama nini sijui! Hayo ni manne tu miongoni mwa mengi tunayosikia toka Yanga kutegemea nani yuko madarakani kwa wakati husika. Tatizo ni kwamba haya hayako kwenye maandishi yoyote na hayana tarehe ya mwisho ya utekelezaji (time frame)

Tunahitaji maduka kama haya ya vilabu vyetu
Tunahitaji maduka kama haya ya vilabu vyetu

Tukienda Msimbazi nako; 1.Sasa mtazamo wetu ni kuwainua vijana na kuwaandaa kuwa timu ya baadaye. Manung’uniko tayari yanasikika toka huko huko Simba kwamba vijana hawa hawana uzoefu. Sijui watapataje uzoefu bila kuchezeshwa! 2. Tunajenga uwanja wa kuchukua watazamaji wengi huko Bunju, barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam. Eneo la ujenzi tumeshapata. Sasa hivi haisikiki kauli yoyote kuhusu mpango huo. 3. Mali za Simba kwenye eneo la makao makuu zinanufaisha watu binafsi. Simba si shamba la bibi. Klabu sasa lazima inufaike na mali zake badala ya watu binafsi. Mkakati huo hauonekani kabisa. Hayo ni matatu tu miongoni mwa mengi tunayosikia toka Simba kutegemea nani yuko madarakani kwa wakati husika. Tatizo ni kwamba haya hayako kwenye maandishi yoyote na hayana tarehe ya mwisho ya utekelezaji (time frame)

Tatizo la leo kusemwa hili la utekelezaji likisemwa na huyu na kesho kusemwa lile la utekelezaji likisemwa na yule ni tatizo la kimfumo wa nchi ambapo hatuna taasisi zenye watu bali sasa tuna watu wenye taasisi! Atakachoamua mtu ndiyo maamuzi ya taasisi. Hizo timu za maamuzi ni maboya tu ya kuhalalisha
kwamba maamuzi husika hayakuwa ya mtu. Kwa mfumo wetu wa sasa, wanaoongoza taasisi wanaogopwa kama nini sijui. Kinachoamuliwa na timu za maamuzi ama kimetokana na kauli ya kiongozi mkuu kwamba “tufanye uamuzi huu” au kimetokana na wajumbe kufahamu matashi ya kiongozi mkuu.

Hata kama tunashindwa kuubadili mfumo wote wa nchi ili kila kitu kiende kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizopo chini ya Katiba yetu bila kubagua watuhumiwa na wajeruhiwa, ni vizuri tuanzie kwenye michezo kwa kujenga mfumo wa kimichezo wa mipango yake kuwa kwenye maandishi yanayotaja mikakati ya utekelezaji na tarehe za mwisho za utekelezaji huku katiba za maeneo husika zikilazimisha utekelezaji wa mipango iliyopo uheshimiwe na kila atakayekuwa madarakani.

Tusipokwenda namna hii, tutakuwa kila mwaka tunaibua vipaji vya ajabu vya Copa Coca Cola na kuviacha vipotee tu. Ni ujinga huu wa kutupa vipaji vya Copa Coca Cola ndiyo utawapoteza watoto wakali wa Simba ambao soka yao inaleta matumani siyo tu ya Simba kali ya baadaye bali ya timu ya Taifa. Nina mashaka kuna siku ataingia kiongozi Simba na kuwatupa watoto hao kutokana na kutokuwepo kwa maandishi ya kumlazimlazimisha aendelee kuwalea.

Ni kwa utaratibu huu wa kuweka mipango yetu kwenye maandishi ya kuheshimiwa na wote, Yanga na Simba watakuwa na viwanja vyao vya soka kwani utekelezaji wa hilo utakuwa wa lazima kwenye maandishi na utakuwa na muda wa utekelezaji wa kila hatua huku kila aingiae madarakani atalazimishwa kikatiba kuendeleza kazi hiyo. Hebu twendeni namna hiyo kwa maendeleo yetu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Ni Paolo Di Canio Sunderland

Chelsea waua Mashetani Wekundu