Kichapo chawaduwaza Real Madrid

*Ancelotti asema bado wana nafasi

Siku chache baada ya kufungwa na Barcelona na kulalamika kwamba wanaonewa na waamuzi, Real Madrid wameshikwa pabaya baada ya kufungwa na Sevilla 2-1.

Real walishajiimarisha kwenye msimamo wa ligi na kuongoza kwa kuwapita watani zao wa jadi nchini Barcelona na watani zao wa jijini Madrid, Atletico Madrid lakini kufungwa na Barca wikiendi iliyopita na kupoteza tena pointi tatu Jumatano hii kumewaacha taabani.

Cristiano Ronaldo aliwanyanyua washabiki wao kwa kupachika bao kutokana na mpira wa adhabu ndogo dakika ya 14, lakini wenyeji walirudi kwa nguvu na kusawazisha dakika tano tu baadaye kabla ya kuzamisha jahazi la Madrid dakika ya 72.

Jitihada za Ronaldo, Karim Benzema, Gareth Bale na nyota wengine hazikufaa kitu, kwani hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa vijana hao wa Carlo Ancelotti walikuwa nyuma na hivyo kuachwa nafasi ya tatu kwa pointi 70.

Atletico wanaongoza ligi kwa pointi 73 baada ya kuwafunga Granada 1-0 Jumatano hii wakati Barca nao walishikilia nafasi ya pili kwa pointi 72 baada ya kuwakung’uta Celta Vigo 3-0. Timu zote hizo zimebakisha mechi nane kukunja jamvi la La Liga.

Ronaldo alilalamika kwamba kila wanapocheza na Barca huwa waamuzi wanapendelea upande wa pili kwa sababu hawataki washinde, kwa vile wanajua wakifanikiwa watatwaa ubingwa wa Hispania, jambo ambalo kuna watu hawapendi litokee.

Kocha Ancelotti mwenyewe anasema kwamba wanatakiwa wajijenge kisaikolojia kwamba wanaweza kushinda, lakini anasema kichapo hicho kidogo kutoka kwa Sevilla walikistahili kwa sababu hawakukabili mashambulizi ya ghafla ya wapinzani wao na ndiyo walitumia kupata mabao mawili.

“Tulikubali kufungwa mabao mawili kwa njia ile ile za ‘conter-attack’ wakati tulipohitaji kuweka uwiano mzuri mchezoni. Tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha tunashinda mechi zetu maana tumepoteza mbili mfululizo jambo ambalo si zuri katika hatua hii.

“Tujiamini tu kwamba tunaweza kushinda, tupo pointi tatu tu nyuma ya Atletico na mbili nyuma ya Barcelona, hakuna kisichowezekana,” akasema Ancelotti aliyerithi mikoba ya Jose Mourinho wa Chelsea klabuni hapo msimu huu.

Posted under:  

Tags:  , , ,

Comments