in , , ,

Kamati ya rufani ya TFF yawaadhibu watano….

Kamati ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imewaadhibu walalamikiwa watano kati ya saba baada ya kufanya mapitio
(revision) kwa uamuzi wa Kamati ya Maadili kutokana na maombi ya
Sekretarieti, huku Richard Julius Rukambura akifungiwa miaka 20 kujihusisha
na mpira wa miguu.

Sekretarieti ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati ya Rufani ya
Maadili ili kupata mwongozo kwa vile kulikuwapo mkanganyiko kwenye uamuzi
wa Kamati ya Maadili, hivyo kuiwia vigumu kwake kuutekeleza.

Uamuzi huo wa mapitio umesomwa leo jioni (Oktoba 15 mwaka huu) mbele ya
waandishi wa habari na wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu
Mwenyekiti Victoria Makani.

Rukambura amefungiwa miaka 20 baada ya kupeleka masuala ya mpira wa miguu
katika mahakama za kawaida kinyume na Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF na
kifungu cha 73(3)(b) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013. Adhabu
yake itamalizika Oktoba 15, 2033.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Rukambura ni
mwanafamilia wa TFF kwa vile aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Pamba ya
Mwanza, na fomu zake za kuomba uongozi TFF ziliidhinishwa na Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga. Vilevile ni ‘Leadership Aspirant’ kwa
mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.

Pia imesema kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kusajili Katiba ya
TFF inayokataza masuala ya mpira wa miguu kwenda katika mahakama za
kawaida, na kutaja vyombo vya haki vitakavyoshughulikia masuala hayo
(judicial organs), Kamati ya Maadili ilikosea kutomtia hatiani mlalamikiwa
kwa kuegemea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Shaffih Dauda, Kamati imebaini kuwa mwanafamilia wa TFF kwani ni
Mwenyekiti wa Bombom FC, fomu yake ya kuomba uongozi ilipitishwa na klabu
ya Simba na pia ameshakuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama
cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo yeye ni ‘Leadership
Aspirant’ kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la
2013.

Hivyo Dauda amepatikana na kosa la kimaadili kwa kutotekeleza maagizo rasmi
ya TFF ya kutosambaza barua iliyotoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga.

Kamati ya Rufani ya Maadili imempa onyo kali na faini ya sh. milioni moja
anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa kufanya hivyo
atafungiwa mwaka mmoja. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha
6(1)(a),(c) na (h) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.

Akilipa faini ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea nafasi ya uongozi
aliyoomba.

Nazarius Kilungeja amepatikana na kosa la kimaadili kwa mujibu wa kifungu
cha 73(8)(a) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwani akijua kuwa
ana adhabu ya kinidhamu ya kufungia miaka mitano na Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) iliyoanza 2009 alichukua fomu kuomba uongozi
TFF.

Hivyo, amefungiwa miaka mitatu, adhabu ambayo itakwenda sambamba na ile ya
RUREFA ambapo kifungo chake sasa kitamalizika Oktoba 15, 2016.

Sekretarieti ya TFF imepewa onyo kali kwa kupokea fomu yake ya kugombea na
malipo wakati akiwa amefungiwa. Onyo hilo pia limetolewa kwa Chama cha
Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Rukwa kwa kuidhinisha
fomu yake ya kugombea.

Naye Wilfred Kidao Mzigama ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF
amepatikana na kosa la kimaadili kwa kuwa na nyaraka la Kamati ya Utendaji
bila kibali na kukiuka taratibu za kuwasilisha malalamiko kwa mujibu wa
Ibara ya 12(2) na Ibara ya 50(1) na (5) ya Katiba ya TFF.

Amepigwa faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu
ambapo akishindwa atafungiwa mwaka mmoja. Akitekeleza adhabu hiyo ataweza
kuendelea na mchakato wa kugombea uongozi kwa nafasi aliyoomba.

Vilevile Kamati hiyo imetoa onyo kali kwa Sekretarieti ya TFF na wajumbe wa
Kamati ya Utendaji kwa kushindwa kudhibiti nyaraka muhimu za vyombo vyao.

Pia Kamati ya Rufani ya Maadili imempata na kosa la kimaadili Kamwanga
Tambwe kwa mujibu wa kifungu cha 73(8) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo
la 2013, kwa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wakati ana adhabu ya
kinidhamu inayomalizika 2014.

Hivyo, amepewa adhabu ya kufungiwa miaka mitatu ambayo itakwenda sambamba
na ile ya kinidhamu na kumalizika Oktoba 15, 2016. Pia Sekretarieti ya TFF,
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) na Chama cha Waamuzi wa
Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Ruvuma wamepewa onyo kali kwa
kupokea na kuidhinisha fomu zake za kugombea uongozi wakati akitumikia
adhabu ya kufungiwa.

Kamati ya Rufani ya Maadili imewakuta kutokuwa na hatia ya makosa ya
maadili kama ilivyobaini Kamati ya Maadili walalamikiwa Riziki Juma Majala
na Omar Isack Abdulkadir, hivyo wana haki ya kugombea uongozi kwa kufuata
Katiba na Kanuni za TFF.

Kwa mujibu wa kifungu cha 74(4) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013,
uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Maadili hauna fursa ya rufani wala
marekebisho kutoka chombo kingine chochote isipokuwa FIFA na Mahakama ya
Usuluhishi wa Michezo (CAS).

*TFF YATOA KITANDA CHA UPASUAJI HOSPITALI YA TEMEKE*

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekabidhi kitanda cha
upasuaji kwa Hospitali ya Rufani ya Manispaa ya Temeke, ikiwa ni sehemu ya
mchango wake kwa jamii.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo (Oktoba 15 mwaka huu) kwenye ukumbi wa
mikutano wa TFF ambapo Hospitali ya Temeke iliwakilishwa na Mwenyekiti wa
Bodi ya hospitali hiyo James Syaga, Mganga Mkuu Dk. Amaani Malima na
Matroni wa hospitali hiyo Deodata Msoma.

Akikabidhi kitanda hicho chenye thamani ya sh. milioni 6.8, Katibu Mkuu wa
TFF, Angetile Osiah alisema amefurahi kuwa ahadi ya kukabidhi msaada huo wa
Hospitali ya Temeke umetimia licha ya kuchukua muda mrefu kutokana na
ukweli kuwa fedha za kununulia kitanda hicho zinatokana na mchezo wa Ngao
ya Jamii wa mwaka jana kati ya Simba na Azam FC.

Alisema uamuzi wa kuiteua Hospitali ya Temeke ulitokana na ukweli kuwa
pamoja na kwamba ofisi za TFF ziko wilayani Ilala, shughuli nyingi kubwa za
Shirikisho linafanyika kwenye Manispaa ya Temeke na hivyo hospitali hiyo
hufanya kazi kubwa ya kuhudumia watu mbalimbali wanaopata matatizo wakati
wa michezo ya mpira wa miguu.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali, Dk. Malima aliishukuru TFF kwa kutimiza
ahadi yao na kwamba msaada huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa wana vyumba
vitatu vya upasuaji, lakini ni viwili tu vilivyo na vitanda kwa hiyo
kitanda hicho kitakamilisha chumba hicho kianze kufanya kazi.

Alisema Hospitali yake sio tu inahudumia wagonjwa kutoka wilayani Temeke,
bali kutoka hata Mkoa wa Mtwara na sehemu nyingine zinazozunguka wilaya
hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali, James Syaga, ambaye alisema anawakilisha
watu wanaohudumiwa na Hospitali ya Temeke, alishukuru kwa msaada huo na
kuiomba TFF kuendelea kuangalia uwezekano wa kusaidia hospitali hiyo.

*ASHANTI, PRISONS UWANJANI VPL*

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho
(Oktoba 16 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ashanti United na Tanzania
Prisons itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam
kuanzia saa 10 jioni.

Nayo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea kesho (Oktoba 16 mwaka
huu) kwa mechi moja ya kundi A ambapo Polisi Dar es Salaam itakuwa mwenyeji
wa Tessema kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Bundi kuwakwamisha Liverpool

England haoo Kombe la Dunia 2014, Brazil..