Italia, Uholanzi zafuzu Kombe la Dunia

Mambo yameanza Ulaya, baada ya Italia na Uholanzi kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.

Nchi mbili hizo zimekuwa za kwanza Ulaya kupenya kwenye mtihani mgumu, ambapo mshambuliaji wa Manchester United, Robin van Persie aliwafungia Uholanzi mabao mawili yaliyowazamisha Andorra. Kwa upande mwingine, ushindi wa Uturuki wa mabao 2-0 dhidi ya Romania ndio uliwahakikishia Wadachi hao kwamba hawataweza tena kufikiwa katika kundi lao la ‘D’.

Italia walitakiwa tu kuwafunga Jamhuri ya Czech ili kufuzu, na ndicho alichowasaidia mshambuliaji mtata, Mario Balotelli aliyepachika bao la ushindi baada ya lile la awali la Giorgio Chiellini la kusawazisha bao la mapema la Libor Kozak wa Czech.

Nchi za mabara mengine ambazo zimeshafuzu kucheza fainali hizo ni wenyeji Brazil, Japan
Australia, Iran, Korea Kusini, Argentina, Costa Rica na Marekani.

Ubelgiji, Ujerumani na Uswisi zinahitaji pointi mbili kila moja ili kujihakikishia nafasi ya kwenda Brazil mwakani. Wajerumani wana uhakika walau wa kuingia hatua ya mwisho ya mtoano, baada ya kuwafunga Visiwa vya Faroe 3-0 kwa mabao ya wachezaji wa Arsenal, Per Mertesacker na Mesut Ozil pamoja na lile la Thomas Muller wa Bayern Munich.

Kadhalika Bosnia-Hercegovina na Ugiriki zimejihakikishia kucheza mtoano wakati Ufaransa nao wakisogea kidogo kwenye hatua hiyo, huku Hispania wakiongoza kwenye kundi hilo hilo.
Argentina walitinga fainali hizo baada ya kuwabanjua Paraguay 5-2.

Marekani waliwafunga Mexico 2-0 wakati Costa Rica wanaoshika nafasi ya pili walikwenda sare ya 1-1 na Jamaica na kufuzu katika nafasi tatu za kwenda Brazil moja kwa moja.

 

Posted under:  

Tags:  , , , ,

Comments