England wawafunga Norway kwa tabu

Hali ya Timu ya Taifa ya England bado si nzuri, kwani usiku wa Jumatano hii wamepata wakati mgumu mbele ya Norway.

Licha ya nahodha mpya, Wayne Rooney kusherehekea nafasi yake mpya kwa kufunga bao, lilitokana na penati na hata washabiki waliojitokeza walikuwa wachache.

Hii ilikuwa mechi yao ya kwanza tangu watolewe kwenye hatua ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia kwa kufungwa na Italia na Uruguay.

Kocha Roy Hodgson alifurahia ushindi huo lakini akasema wazi kwamba inabidi wakaze buti ili kuwashawishi washabiki wao kuwarudia, maana idadi iliyojitokeza, 40,181 ni ndogo kuliko zote katika dimba la Wembley.

Hii ilikuwa mechi ya matayarisho kwa ajili ya kujiandaa katika hatua za kufuzu kwa Euro 2016, ambapo England watakabiliana na Uswisi ugenini Jumatatu hii.

Hodgson anasema kwamba wataendelea kucheza mbele ya washabiki wachache, lakini sababu anayoitoa ni kwamba timu pinzani wanazocheza nazo hazina mvuto.

Kipa Joe Hart naye anasema kwamba washabiki walijitokeza wachache si kwa sababu England wanacheza vibaya, bali kwa sababu ilikuwa usiku wa Jumatano wakati ambapo shule zimeshaanza muhula mpya, lakini nahodha Rooney anasema kwamba ni jukumu la wachezaji kuchemka na kurejesha imani ya washabiki.

Raheem Sterling alicheza vyema kwa England, kutokana na kasi yake na alilitia lango la Norway katika hatari, na ndiye pia alisababisha penati iliyozaa bao.

Vijana wa Hodgson walishindwa kulenga mpira langoni hadi dakika ya 68 kwa penati ya Rooney na walitawala mchezo kwa asilimia 63.
 
Hatari kubwa iliyomkabili kipa wa Norway Orjan Nyland na kuokoa ilikuwa shuti kali la mshambuliaji mpya wa Arsenal, Danny Welbeck dakika za mwisho, na mpira kumalizika kwa England kulenga mpira golini mara mbili tu.

Hilo, hata hivyo, halimwingii akilini Hodgson ambaye anasema: “Mashuti mawili tu langoni? Msinipige na takwimu hapa. Mbona tulitawala mchezo kwa kiasi kikubwa namna ile halafu mnazungumzia juu ya takwimu za kulenga goli, vipi kuhusu mashuti ambayo wachezaji wao walizuia?” akamaka Hodgson.

Katika mechi nyingine za kimataifa za kirafiki, Ujerumani walipigwa 4-2 na Argentina, Jamhuri ya Ireland wakawachapa Oman 2-0, Urusi wakawakandamiza Azerbaijan 4-0 na Lithuania wakatoshana 1-1 na Emarati.

Kadhalika Ukraine waliwafunga Moldova 1-0, Latvia wakawashindwa Armenia 2-0, Denmark wakalala 2-1 mbele ya Uturuki wakati Jamhuri ya Czech walifungwa 1-0 na Marekani.

Posted under:  

Tags:  ,

Comments