in , ,

‘Dream Team’ ya AFCON 2013

*Wamo Obi Mikel, Keita, Kone, Pitroipa, Emenike

 

Ilikuwa furaha kutazama Michuano ya 29 ya Kombe la Mabingwa Afrika (AFCON) iliyomalizika nchini Afrika Kusini.

Mengi yameonekana, kuanzia waamuzi wazuri na wale wenye utata, aina tofauti ya viwanja, chachu ya mashabiki kutoka nchi mbalimbali, na wachezaji wenyewe.

Mkusanyiko wa wachezaji wa timu 16 zilizoshiriki, tumeona kuanzia waliokuwa hawajulikani kabisa kutoka timu za madaraja ya chini hadi walioshiriki na kutwaa Kombe la Mabingwa wa Ulaya wakiwa Chelsea.

Michezo hii imeweka msingi wa majadiliano makubwa, ambapo makocha wa mataifa tofauti duniani wanaanza kutupa ndoano zao kuwanasa wachezaji kwa msimu ujao wa kiangazi.

Wachambuzi wa soka huwa hawaishii tu kwenye fainali kwa kombe kuchukuliwa, bali wanaangalia uwezekano wa kuunda timu, na kwa hali hii, inaweza kuitwa ‘Dream Team ya AFCON 2013’.

Kwa upande wa golikipa, ni Vincent Enyeama wa mabingwa wapya – Super Eagles wa Nigeria, aliyekuwa pia nahodha wao.

Alicheza kwa kujiamini sana, na katika mechi zote hakukumbana na balaa wala hakufanya ajizi kulinda lango lake, tofauti na ilivyotokea kwa baadhi ya magolikipa.

Enyeama mwenye uzoefu wa zaidi ya muongo mmoja katika timu ya taifa, alifanikiwa kuwaongoza wadogo zake, na alifanya vyema zaidi walipomenyana na Ivory Coast kwenye robo fainali, akiokoa hatari nyingi, ikiwamo kukabiliana na Kolo Toure wa Manchester City.

Tukija kwa beki ya kulia, tunaye Fousseiny Diawara wa Mali aliyerejea kwenye soka ya kimataifa karibuni na kuipa uhai na nguvu timu yake.

Ni wachache waliweza kumpita, japokuwa katika mechi zote alikabiliana na wachezaji mahiri; anatumia akili na maarifa, akihakikisha licha ya kujihami anapanda mbele kusaidia mashambulizi na kurudi mara.

Bakary Kone wa Burkina Faso ni mlinzi hodari, na mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa washindi hao wa pili, waliomaliza mashindano kwa kuruhusu mabao matatu tu, moja likiwa ni penati.

Kone (24) anachezea Olympique Lyon ya Ufaransa, na tulimshuhudia mara kwa mara akisogea kumsaidia mlinzi mwenzake wa kati, Paul Koulibaly mambo yalipomwelemea.

Nahodha wa Visiwa vya Cape Verde, Nando naye anaingia katika timu hii, na alionesha kiwango cha juu cha kupigana ‘vita’ uwanjani. Ni mlinzi wa kati wa klabu ya daraja la pili nchini Ufaransa anayepigiwa mfano.

Elderson Echiejile wa Nigeria anaingia hapa kwa sababu alikuwa tishio kwa mabeki na magolikipa, akivuma kutoka nyuma upande wa kushoto hadi langoni mwa adui.

Bao la kijana huyu mwenye umri wa miaka 25 dhidi ya Mali katika mechi ya nusu fainali lilikuwa muhimu katika kubadili mwelekeo wa mechi ile, ambayo hatimaye imekuja kuwapa ubingwa Nigeria.

Anarudi Braga ya Ureno alikokuwa akiwekwa benchi, akiamini kwamba ataanza kucheza mwanzo, vinginevyo klabu zitamnunua kuanzia Mei mwaka huu.

John Obi Mikel wa Nigeria na Chelsea alikuwa nguzo kubwa kwa timu yake tangu mwanzo, na ametokea kutawazwa mchezaji bora wa mashindano.

Amekuwa katika Super Eagles tangu 2006, japokuwa hakufanya vyema sana humo kabla ya michuano hii.

Anamudu vyema sehemu ya kiungo, ana nguvu anapokuwa na mpira, anawavuruga wapinzani wake na ni mahiri katika kuipeleka mbele timu yake, jambo ambalo ni msingi wa kupatikana mabao.

Kwa waliokuwa wakisikiliza au kutazama michuano hii watalikumbuka jina la Charles Kabore wa Burkina, kwa jinsi lilivyokuwa likitajwa mara kwa mara.

Ni tunda la Olympique Marseille, akitamba kwenye beki hadi kiungo, na utulivu wake uliisaidia sana timu ilipokuwa kwenye wakati mgumu, hasa kutokana na uamuzi mbaya wa mwamuzi.

Nahodha wa Mali, Seydou Keita (33) anaingia kwenye Dream Team bila wasiwasi. Alikuwa chachu kwa timu yake, akizunguka uwanja mzima kama mwenye mapafu ya mbwa, tamaa yake ikiwa ni kuona timu ikishinda. Anastahili sifa kwa alipoifikisha.

Jina la Jonathan Pitroipa wa Burkina Faso nalo limekuwa maarufu, kwa jinsi alivyowahangaisha mabeki, na pia kadi nyekundu aliyopewa kwenye nusu fainali, kisha ikafutwa na CAF, kwani mwamuzi aliboronga.

Unapata furaha unapomwangalia akipiga chenga zile za maudhi, kuumiliki mpira na kuwasalimu magolikipa kwa mipira ya akili inayowachanganya na kujikuta ipo nyavuni.

Mshambuliaji Victor Moses wa Chelsea ana mwaka tu kwenye timu ya taifa ya Nigeria, lakini kishindo chake mwaka huu kilikuwa na mwangwi mkubwa.

Alicheza huku akiuguza majeraha wakati wote wa mashindano, akafunga mabao mawili dhidi ya Ethiopia na kuiwezesha Nigeria kuvuka hatua ya makundi, jambo lililokwishaanza kuonekana gumu.

Nyota mpya ya Nigeria ni Emmanuel Emenike, anayekumbusha wengi jina la mshambuliaji mwenzake wa zamani, Emmanuel Amunike.

Huyu ndiye mfungaji bora wa mashindano haya, kibindoni akiwa na mabao manne. Alisononeka kwa kukosa fainali kwa sababu ya mamivu ya msuli wa paja, vinginevyo tungekuwa tunazungumzia idadi kubwa zaidi ya mabao.

Nyota huyu wa Spartak Moscow ana mtindo wa uchezaji unaowiana na mfungaji bora wa jumla wa Nigeria katika historia, Rashidi Yekini, akitisha kwa kasi na nguvu.

Nigeria imebahatika kupata nafasi ya kukaa na kombe hilo hadi mwaka 2015, itakapolipeleka Morocco kwa ajili ya kulitetea na timu nyingine 15, lakini kwa sasa hii ndiyo timu ya AFCON 2013.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

NOTICE TO OUR CUSTOMERS AND THE GENERAL PUBLIC

VIWANJA VYA MICHEZO NI MALI YA WANANCHI VIRUDISHWE KWAO