in , ,

Arsenal wawanyamazisha Napoli

*Chelsea wazindukia Romania

*Man City na Man U kibaruani

 

Moto uliowashwa na Arsenal umeendelea kuteketeza wapinzani wake, baada ya usiku wa Jumanne hii kuwachapa Napoli 2-0.

 

Wakicheza mbele ya umati wa washabiki wao nyumbani Emirates, Arsenal wamekwea kwenye uongozi wa kundi lao la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

Alikuwa ni Mesut Ozil aliyenunuliwa kwa dau la kuvunja rekodi msimu huu aliyefunga bao la kwanza dakika ya nane kabla ya kumtengenezea pande Olivier Giroud aliyetikisa nyavu dakika ya 15.

 

Baada ya mabao hayo Napoli wa Italia wanaofundishwa na kocha wa zamani wa Liverpool na Chelsea, Rafa Benitez walijaribu kuzinduka na kufanya mashambulizi, lakini yaliokolewa na Arsenal.

 

Pamoja na Napoli kukosa shabaha kwa wengi wa washabuliaji wake kupiga mipira juu, mingine ilikabwa vyema na mabeki na viungo wa Arsenal na michache kuishia mikononi mwa golikipa Wojciech Szczęsny.

 

Katika mechi ambayo hapakuwa na mchezaji yeyote aliyeoneshwa kadi ya nyekundu wala ya njano, kipa wa Napoli, Pepe Reina aliokoa hatari nyingi langoni mwake wala hana lawama kwa mabao mawili ya kifundi na kishindo ya Arsenal.

 

Washika Bunduki wa London walitamba zaidi kwenye kiungo, ambapo licha ya kutokuwapo Santi Cazorla ambaye ni majeruhi, Kocha Arsene Wenger alithubutu kumwacha mtaalamu Jack Wilshere kwenye benchi hadi kipindi cha pili, akiwaamini Ozil na Aaron Ramsey ambao walifanya kazi yake vyema.

 

Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Borussia Dortmund wa Ujerumani walizinduka na kuwafunga Marseille mabao 3-0. Katika mechi iliyopita, Dortmund walifungwa na Napoli wakati Arsenal waliwafunga Marseille wa Ufaransa.

 

CHELSEA WAWACHINJA STEUA BUCHAREST

 

Chelsea wamepata ushindi wa kwanza kwenye msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kuwachapa Steua Bucharest mabao 4-0.

 

Wakicheza ugenini, Chelsea walipata mabao yao kupitia kwa Ramires aliyefunga mawili, Frank Lampard na Daniel Georgievski aliyejifunga.

 

Andre Schurrle alionesha mchezo mzuri kwenye wingi kwa Chelsea, ambapo ushindi ulikuwa muhimu, kwani katika mechi 11 za ligi hiyo zilizopita Chelsea wameshinda tatu tu na sasa wanashika nafasi ya tatu kwenye kundi lao.

 

Wanaoongoza kundi hilo ni FC Schalke ya Ujerumani ambao katika mechi ya kwanza waliwafunga Steua Bucharest na usiku wa Jumanne waliwafunga Basel kutoka Uswisi ambao katika mechi ya kwanza waliwafunga Chelsea.

 

BARCA, ATLETICO MADRID WASHINDA

 

 
Katika mechi iliyochezwa Uskochi, klabu bingwa ya nchi hiyo, Celtic walifungwa bao 1-0 na Barcelona waliocheza bila nyota wao, Lionel Messi ambaye ni majeruhi.

 

Celtic walilazimika kumaliza mechi wakiwa 10, baada ya nahodha wao, Brown kumchezea rafu mbaya Neymar aliyekuwa akielekea kufunga na baada ya hapo akampiga teke mkononi akiwa chini.

 

Zenit St Petersburg wa Urusi walitoka suluhu na FK Austria Wien kutoka Austria wakati Atletico Madrid kutoka Hispania waliwafunga FC Porto wa Ureno 2-1 wakati Ajax na AC Milan walikwenda sare ya bao 1-1.

 

KIVUMBI MAN U, MAN CITY CHAJA

 

Mechi za pili kwa makundi mbalimbali ya ligi hiyo zinaendelea Jumatano hii, ambapo Manchester United watakaribishwa na Shakhtar Donetsk wakati Manchester City watakuwa wenyeji wa Bayern Munich.

Bayern Leverkusen watacheza na Real Sociedad; Juventus na Galatasaray waliopata kocha mpya katika Roberto Mancini; Real Madrid watawakaribisha FC Kobenhavn; Paris Saint Germain watavaana na Benfica; RCS Anderlecht wanacheza na Olympiakos wakati CSKA Moscow wanacheza na Viktoria Plzen.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

MECHI ZA YANGA, SIMBA ZAINGIZA MIL 182/-

*WATATU KUSHIRIKI KOZI YA FUTURO ADDIS ABABA*