Arsenal wateswa na Bayern

Historia imeendelea kujirudia, ambapo Arsenal wanapata shida katika hatua ya 16 bora, pale walipoanza kwa kupoteza mechi ya kwanza.

Wakicheza uwanja wa nyumbani wa Emirates kama msimu uliopita, Arsenal walipata kipigo cha 2-0 huku wakicheza 10 kwa zaidi ya dakika 45.

Arsenal walianza vyema mchezo na kushambulia kama mbogo waliojeruhiwa na nusura wajipatie mabao katika robo saa ya kwanza.

Walipata penati baada ya Mesut Ozil kuangushwa kwenye eneo la hatari, lakini mchezaji huyo Mjerumani alikosa penati kama alivyopata kukosa mara tatu zilizopita.

Bayern nao walikosa penati iliyotolewa kwa madai kwamba kipa wao, Wojciech Szczęsny kudaiwa kumwangusha Arjen Robben.

Szczesny alipewa kadi nyekundu, nafasi yake ikachukuliwa na Lukasz Fabianski aliyecheza vyema na penati ya Bayern iliota mbawa.

Hata hivyo, Arsenal waliendelea kuishiwa nguvu kwa kuzidiwa mtu mmoja kadiri mchezo ulivyoendelea.

Hali hiyo ilichangiwa pia na beki hodari wa kushoto, Kieran Gibbs kutoka mapema baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nacho Monreal aliyesumbuliwa vilivyo na Robben.

Mabao ya Wajerumani yalifungwa na Tony Kroos na Thomas Muller na kuwapa vijana wa Arsene Wenger wakati mgumu kupindua matokeo hayo watakapokwenda Bayern kurudiana.

Katika mechi nyingine, Atletico Madrid kutoka Hispania waliwalaza AC Milan 1-0 katika mechi iliyochezwa nchini Italia.

Hali hiyo inafanya timu wageni katika mechi nne zilizokwishachezwa kuwafunga wenyeji, kwani Barcelona waliwafunga Manchester City dimbani Etihad na Paris Saint Germain kuwanyonga Bayer Leverkusen kwao.

Posted under:  

Tags:  , , ,

Comments