in , ,

NYALLA, NYAULINGO, NYENZI WASHINDA RUFANI

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imewarejesha warufani wote watatu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa
Kamati mpya ya Utendaji ya TFF utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu jijini Dar
es Salaam.

Samwel Nyalla, Ayubu Nyaulingo na Ayoub Nyenzi walikata rufani mbele ya
Kamati hiyo inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard
Luanda kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwaondoa katika
uchaguzi huo ambapo wote wanagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji
kuwakilisha kanda mbalimbali.

Akisoma uamuzi wao leo (Oktoba 11 mwaka huu) mbele ya Waandishi wa Habari
kwenye ofisi za TFF, Jaji Luanda amesema baada ya kusikiliza hoja za
Mrufani Nyalla walipitia Kanuni za Uchaguzi za TFF na kugundua yafuatayo;

Ibara ya 10(3) imeweka masharti makuu mawili ya ujazaji wa fomu za kugombea
uongozi. Fomu hiyo ni lazima iwe na saini ya mgombea na ni lazima
ithibitishwe na viongozi wa shirikisho.

Kamati imepitia Kanuni za Uchaguzi haijaona sehemu fomu hiyo ya uongozi
imeambatanishwa ili kuifanya kuwa Kanuni ya Uchaguzi. Ni maoni ya Kamati
kuwa ni vizuri fomu za kugombea zikawa ni sehemu ya Kanuni za Uchaguzi.

Kwa vile Kanuni za Uchaguzi za TFF za 2013 pia hazijaainisha nini adhabu
kwa mgombea aliyekosea kujaza Fomu namba 1 ya kugombea uongozi, Kamati
inaona itakuwa si haki kumnyima mgombea nafasi ya kushiriki katika uchaguzi
kwa vile tu fomu yake haijajazwa vipengele vyote.

Nyalla aliondolewa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa maelezo
kuwa si mtu makini anayeweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu baada ya
kushindwa kujaza Fomu namba 1 kipengele cha 15 kinachohusu malengo ya
mgombea uongozi.

Kwa upande wa Nyaulingo ambaye aliondolewa kwa kukosa uzoefu uliothibitika
kulingana na Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za
Uchaguzi za TFF, Kamati ya Rufani imeamua ifuatavyo;

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya
kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa
kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.

Mrufani alifafanua historia yake katika masuala ya michezo kuanzia
alipokuwa anasema Chuo Kikuu kuanzia 2005-2009 na pia ushiriki wake kama
mchezaji wa Rukwa United iliyowahi kushiriki Ligi ya Mkoa wa Rukwa na ligi
nyingine za kitaifa.

Kwa kusoma maana ya ‘Familia ya TFF’ iliyoko kwenye utangulizi wa Katiba ya
TFF, pamoja na Ibara ya 29(3) na 29(6) ya Katiba hiyo, Kamati imejiridhisha
kuwa Mrufani ana sifa za kugombea uongozi wa Shirikisho na amekidhi kigezo
cha sifa za ugombea.

Ameshiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu kama mchezaji na mtawala, hivyo
kutimiza kigezo kilichohitajika cha ushiriki katika uongozi na utawala wa
mchezo wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.

Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya
Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani anapewa
nafasi ya kushiriki katika uchaguzi.

Kuhusu Ayubu Nyenzi aliyeondolewa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa Ibara ya
29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, na
pia kushindwa kuthibitisha uraia wake mbele ya Kamati ya Uchaguzi, Kamati
ya Rufani katika uamuzi wake imesema;

Imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo
kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati
ya Uchaguzi.

Baada ya uchambuzi wa kina, Kamati imeona kuwa kulingana na maelezo
yaliyotolewa na Mrufani na viambatanisho vilivyowasilishwa, Kamati haina
shaka kuhusu uraia wake. Uthibitisho wa uraia unapaswa kufanywa kwa umakini
na taasisi yenye mamlaka ya kiserikali kufanya hivyo.

Kamati pia imejiridhisha kupitia Fomu namba 1 iliyojazwa na kusainiwa na
Mrufani kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010, Nyenzi ameshika nyadhifa za
utawala wa mpira wa miguu na hasa katika klabu ya Yanga, uzoefu unaomfanya
kuwa na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi katika TFF kulingana na Ibara ya
29(3) ikisomwa pamoja na Ibara ya 29(6).

Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya
Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani atashiriki
katika uchaguzi wa TFF kwa nafasi anayogombea.

* *

*Wakati huo huo,* Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF inakutana keshokutwa
(Oktoba 13 mwaka huu), kufanyia mapitio (revision) ya uamuzi wa Kamati ya
Maadili kwa waombaji uongozi wanane kama ilivyoombwa na Sekretarieti ili
kutoa mwongozo wa utekelezaji wa uamuzi huo.

*VITAMBULISHO KURIPOTI KOMBE LA DUNIA*

Maombi ya vitambulisho kwa waandishi wa habari (Accreditation) wanaotaka
kuripoti Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil
kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) yataanza kupokelewa
kwa mtandao Desemba 7 mwaka huu kupitia akaunti ya FIFA Media Channel.

Mwisho wa kupokea maombi hayo itakuwa Januari 31 mwakani, hivyo kwa
waandishi wanaotaka kupata vitambulisho hivyo ni lazima wawe na akaunti ya
FIFA Media Channel pamoja na utambulisho wa mtumiaji wa akaunti hiyo (user
ID).

Kwa mujibu wa FIFA, kila nchi itapewa idadi maalumu ya nafasi kwa waandishi
(waandishi wa kawaida pamoja na wapiga picha) baada ya mechi za mchujo za
Kombe la Dunia kumalizika ambapo vigezo mbalimbali vitazingatiwa ikiwemo
nchi kufuzu kwa fainali hizo.

Hivyo, nchi ambayo itakuwa imefuzu itakuwa na nafasi zaidi kulinganisha na
zile ambazo hazitakuwa na timu katika fainali hizo za Brazil.

Mgawanyo wa nafasi zitakazotolewa kwa Tanzania utapangwa na Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kulingana na maombi yatakayokuwa
yamewasilishwa FIFA kupitia FIFA Media Channel.

TFF inatoa mwito kwa waandishi wa habari za mpira wa miguu ambao hawana
akaunti FIFA Media Channel kuhakikisha wanakuwa nayo mapema ili waweze
kutuma maombi yao.

* *

*SIMBA YAIVAA PRISONS, YANGA MGENI BUKOBA VPL*

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inakamilisha
raundi ya nane kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kwa mechi tatu zitakazochezwa
Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.

Simba ina fursa ya kuendelea kukamata usukani wa ligi hiyo iwapo itaishinda
Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne
Chale inashika nafasi ya kumi na moja katika msimamo wa ligi hiyo.

Ili iendelee kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo
iliyoanza Agosti 24 mwaka huu, Tanzania Prisons ambayo katika mechi yake
iliyopita ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting
inalazimika kuifunga Simba.

Licha ya sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita dhidi ya Ruvu
Shooting, Simba inayoongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Azam na
Mbeya City matokeo mazuri katika mchezo huo ni muhimu kwao kama ilivyo kwa
wapinzani wao Tanzania Prisons.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na
sh. 20,000 ambapo tiketi zitauzwa uwanjani kwenye magari maalumu kuanzia
saa 4 kamili asubuhi.

Mabingwa watetezi Yanga wao watakuwa mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba
kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wanaofundishwa na Mganda Jackson Mayanja
akisaidiwa na Mrage Kabage.

Kagera ambayo inapishana na Yanga kwa tofauti ya pointi moja ilipoteza
mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya kulala kwa mabao 2-1 kwenye
Uwanja wa Azam Complex. Wakati Yanga ikiwa katika nafasi ya nne kwa pointi
12, Kagera Sugar ni ya sita kwa pointi kumi na moja.

Iwapo Kocha Ernst Brandts atawaongoza vijana wake wa Yanga kuibuka na
ushindi katika mechi hiyo na Simba kufanya vibaya kwenye mechi dhidi ya
Tanzania Prisons huenda akakamata uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha timu
14.

Mwamuzi Zakaria Jacob wa Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya Ashanti
United na Coastal Union itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi,
Dar es Salaam.

Raundi ya tisa ya ligi hiyo inaanza keshokutwa Jumapili (Oktoba 13 mwaka
huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers (Mabatini, Mlandizi),
Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na JKT Ruvu (Azam
Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu, Turiani).

Mechi zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam TV kupitia TBC1 wikiendi
hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Jumamosi katika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu
itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.

* *

*FDL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI HII*

Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote matatu inaendelea wikiendi hii
ambapo kundi B litakuwa na mechi moja tu kati ya Lipuli na Mlale JKT
itakayochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya
Samora mjini Iringa.

Transit Camp itakwaruzana na Tessema katika Uwanja wa Mabatini mjini
Mlandizi wakati Polisi Dar itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam katika mechi za kundi A zitakazochezwa
kesho (Oktoba 12 mwaka huu).

Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kuzikutanisha
Friends Rangers na Villa Squad.

Timu zote nane za kundi C zinashuka viwanjani kesho (Oktoba 12 mwaka huu)
kusaka pointi tatu. Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma utakuwa mwenyeji wa
mechi kati ya Polisi Dodoma na JKT Kanembwa ya Kigoma.

Pamba na Mwadui zitacheza katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza,
Polisi Tabora itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi mjini Tabora wakati uga wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma
utatumika kwa mechi kati ya Polisi Mara na Stand United ya Shinyanga.

* *

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Kagera yaipania Yanga Kaitaba…

Ni Simba, Azam, Yanga