in

Niyonzima mwenye sura ya “Uongozi” na “Ufundi”

YANGA


Ulisikia alichokisema kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael baada ya mchezo wa Mwadui FC na Yanga SC uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage? Kwake yeye kupata alama tatu kilikuwa ni kitu cha muhimu na msingi sana jana.

Aliongea kuhusu eneo la kuchezea la uwanja (Pitch) , ubovu wa eneo lile la kuchezea liliwalazimisha watumie mipira mirefu kwa kiasi kikubwa, kitu ambacho hakikuwa kizuri kwa mujibu wake.

Tuachane na malalamiko ya ubovu wa uwanja wa CCM Kambarage yaliyotolewa na Luc Eymael. Tusahau pia alama tatu ambazo kocha mkuu wa Yanga alikuwa akizitaka kwenye mchezo huo dhidi ya Mwadui FC.

Turudi kutazama vitu viwili vya msingi kwenye ile mechi ya jana,  cha kwanza akili ya Haruna Niyonzima na cha pili ni miguu ya Haruna Niyonzima iliyokuwa imekanyaga zile nyasi za CCM Kambarage.

Haruna Niyonzima alicheza mbele ya Kelvin Yondani , mchezaji ambaye amezoea kucheza kama beki wa kati. Ni mara chache sana kwake yeye kucheza eneo la kiungo cha kuzuia kama alivyocheza jana.

Kwa jana Kelvin Yondani alitimiza majukumu makubwa sana ya kuilinda safu ya ulinzi ya Yanga. Mabeki wanne wa Yanga walikuwa salama kwa sababu ya ulinzi imara wa Kelvin Yondani aliokuwa ameuweka kwenye eneo la katikati ya uwanja.

Kulinda safu ya ulinzi ya Yanga ndilo lilikuwa jukumu la kwanza la Kelvin Yondani kwenye mchezo wa jana, na jukumu hilo alilitimiza, jukumu la pili lilikuwa jukumu la kuisogeza timu mbele.

Kuokota mipira na kuisogeza mbele eneo la kiungo cha ushambuliaji , eneo ambalo lilikuwa na kina Mapinduzi Balama na Haruna Niyonzima. Kelvin Yondani hakuwa mzuri sana kusogeza timu mbele.

Kitu ambacho kilikuwa kinawapa shida kina Haruna Niyonzima. Haruna Niyonzima alikuwa anashuka chini kuchukua mipira na kuisambaza sehemu mbalimbali za uwanja, goli la Yanga lilianzia kwake baada ya kuchukua mpira katikati na kuipeleka kwa Jaffary Mohammed. 

Akili yake ilijua kabisa namna ya kuiendesha timu na kufukia madhaifu ya Kelvin Yondani katika kupandisha timu. Alichoamua ni kutumia akili yake ipasavyo na kuhakikisha miguu yake ikionesha ufundi wa hali ya juu kuisaidia timu.

Alikuwa fundi mzuri jana,  akili yake pia ilikuwa na hekima kubwa, aliwaongoza wenzake kama kiongozi.  Wakati ambao timu ilitakiwa kuwa kwenye presha ya kawaida alihakikisha timu ina presha ya kawaida.

Kuna wakati ambao timu ilihitaji kupigana kwa nguvu, Haruna Niyonzima aliwatia moyo na kuhakikisha wanapigana kwa kiasi kikubwa kwenye mechi ya jana na kuna wakati alihimiza umoja ndani ya timu ili kuhakikisha timu inashinda mechi ya jana.

Uongozi wake ulikuwa kwenye sura yake, ufundi ulikuwa kwenye miguu yake, alihakikisha ufundi wake unaonekana kwa kiasi kikubwa mpaka timu yake ikafanikiwa kushinda.  Inawezekana hakuwa mchezaji bora wa mechi ila alikuwa mchezaji muhimu kwenye mechi hiyo.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Simba Sports Club

Naikubali Simba, Ajibu fundi sana- Shahanga

Simba Sports Club

Yanga Kuiadhibu Simba Kwa Morrison ?