in ,

Ninavyokumbuka watemi wa Leeds United

Leeds United


LEEDS UNITED. Ni jina kubwa katika kandanda. Ni timu inayokumbukwa kwa
mengi. Mashabiki wahuni, vichaa wa mpira, watukutu, wajanja na wanalijua amsha
amsha ya soka viwanjani. Leeds ilikuwa Leeds haswa. Ilikuwa kiboko yao katika zama
zao na walinogesha mechi kila wikendi au katikati ya wiki za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwanini Leeds? Nimesema kidogo kuhusu sifa za mashabiki wa Leeds United. Lakini
vilevile tukubali Leeds United ni timu ambayo ilikuwa maarufu kuliko hata baadhi ya
timu zilizopo sasa. Kwenye hadhi ya Leeds United na umaarufu wao walikuwepo
Nottingham Forest, Reading, Liverpool, Stoke City, West Ham, Southampton, Shiefield
Wednesday na wakongwe wenzao kwa England.

Ingekuwa Serie A, ningetaja Parma, Napoli, AC Milan, Fiorentina, sampdoria, na wenzao. Kule Bundesliga ningezitaja Bayern Munich, Dortmund FC Cologne au EitratchF rankfurt.

Mabadiliko ya muundo wa Ligi Kuu England miaka 1990 yalileta umaarufu zaidi wa Manchster United, Arsenal,Tottenham na nyingine za kaliba yao. zipo timu zilizopotea kutokana na sababu mbalimbali na zilikuwa zinavutia wengi.
MIAKA 16 YA LEEDS UNITED Imepita miaka 16 tangu Leeds United iliposhuka daraja nchini England yaani mwaka 2004.

Tanzania Sports
Kikosi cha sasa cha Leeds United, baada ya kupanda daraja

Wakati huo nilikuwa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Meta, jijini
Mbeya. Nilikuwa nikiishi mtaa wa Forest uliopo Kata ya Kadeghe. La kufurahisha
zaidi niliishi mita 100 kutoka ukumbi maarufu wa starehe wa Dhando Complex.


Jirani yangu na mtani wangu mmoja alitokea mkoani Mtwara alipenda kushabikia timu ya Southampton. Yeye hakuambilika kuhusu Southampton, lakini mimi sikuambilika kuhusu Real Madrid. Kwenye Ligi Kuu England nilipendelea kuifuatilia Leeds United, iliyokuwa imejaza mastaa kibao kikosini mwao.


Kwa sasa Leeds United wamefanikiwa kutinga Ligi Kuu wakitokea Ligi daraja la
kwanza maarufu kama Championship. Mechi yao ya mwisho Ligi Kuu England
ilikuwa miaka 16 iliyopita walipomenyana na Chelsea na kufungwa bao 1-0
walipokuwa wakifundishwa na Claudio Raineri.

Tangu iliposhuka daraja mwaka 2004 Leeds United ikazidi kuporomoka na imewahi
kushuka daraja la kwanza na kwenda hadi la daraja la pili kati ya mwaka 2007 hadi
2010.


Palikuwa na matatizo ya umiliki na uongozi wa Leeds United ambayo yalichangia
kuiporomosha timu hiyo. Hadi sasa Leeds United wamekujisanyia pointi 87 katika
mechi 44, lakini zikiwa zimebaki mechi mbili wamejihakikishia kupanda Ligi Kuu.

Msimu huu Leeds United wapo chini ya kocha Marcelo Bielsa ambaye nimekuwa
nikivutiwa na aina ya soka la timu anazofundisha. Pasi nyingi, kasi, umiliki wa mpira wa kutosha, vipaji ni burudani ya aina yake ambayo anaitoa kwa mashabiki. Bielsa ni yule yule ingawa tatizo lake ni lileile; ukame wa makombe.


Soka lake ni lilelile. Anakuburudisha na kukupa ladha ya kipekee kutoka timu yake.
Unaweza kumwona anavyochuchumaa kwenye mstari wa uwanja yaani Touchline.
Unaweza kumwona akizunguka zunguka katika eneo lake. Bielsa ni fundi wa soka.


MASTAA WA NGUVU


Miaka 1990 na mwanzoni mwa miaka 2000 kulikuwa na amstaa wengi waliokuwa
wakichezea vilabu vikubwa barani Ulaya. Lakini siku hizi kuna uhaba wa mastaa wa
kiafrika kwenye vilebu vikubwa huko Ulaya (hii ni mada nyingine kwa siku nyingine).

Tanzania Sports
Lucas Radebe


LUCAS RADEBE; Huyu ni miongoni mwa mastaa waliotia for a Elland Road.
Alikuwa mwamba wa Leeds United. Mrefu, ngangari, mwanaume wa shoka na
aliwakilisha vema uwezo na ufundi wake katika kanda. Radebe alitumia muda mwingi kuichezea Leeds United kwenye dimba la Elland Road. Alijiunga na Leeds mwaka 1994 akitokea Kaizer Chiefs ya kwao Afrika kusini.


SOLOMON OLEMBE; Ni nani amesahau kasi ya mwanandinga huyu? Staa kutoka
Cameroon huyu alichezea Leeds msimu wa 2003/2004 akitokea klabu ya Olympique
Marseille ya nchini Ufaransa. Ni miongoni mwa wachezaji wakubwa waliotokea barani Afrika na kutamba huko ulaya. Alikuwa winga machachari.


JAMES MILNER; Huyu amekulia akademi ya Leeds United. Kwa sasa yuko
Liverpool. Ni mchezaji ambaye anawakilisha kizazi cha zamani cha miamba ya soka.
Inashangaza kumwona bado akiwa dimbani kunyukana na kizazi kipya cha soka. Ni
burudani mno. Uzuri, alipikwa Leeds United.

ALLAN SMITH; Moja ya wachezaji mahiri waliopatikana katika kikosi cha Leeds ni
huyu. Alikuwa kiungo mahiri na zaidi alikuwa na tabia za kihuni huni tu. Uwanjani
alikuwa bonge la bishoo. Nywele zake zilikuwa zinawekwa dawa, na hata baadaye
alipojiunga na Manchester United ya Alex Ferguson alikuwa amewaka rangi ya
dhahabu katika nywele zake. Smith alikuwa kipenzi cha mashabiki, lakini kitendo cha
kujiunga Man United aliitwa Yuda, kwamba alikuwa amewasaliti. Yuda Smith alikuwa
anafurahisha ndani ya jezi za Leeds.


JERMAINE PENNANT; wengine wanadhani ni staa wa Arsenal, lakini ukweli ni
kwamba huyu ni mmoja wa wachezaji mahiri waliokulia Leeds United. Alikuwa winga
machachari sana. Achana na ujinga ujinga wake, lakini Leeds ndiko alikopikwa.
NICKY BARMBY; Alitengeneza jina lake katika kikosi cha Leeds kabla ya kuhamia
Liverpool. Ni mwamba ambao ulikuwa kivutio katika kikosi cha Leeds.


MARK VIDUKA; nani amesahau mabao makali ya mwamba huyu? Nani amesahau
mateso waliyopata mabeki na makipa? Viduka alikuwa Viduka haswa. Namkumbuka
kwa mabao zaidi kuliko mbwembwe zingine. Ilikuwa unasikia chumaaaaaaa! Ujue
tayari.

Tanzania Sports
kazi kweli kweli


ERICK BAKKE na LAN HARTE; Tukianza na Harte, yeye alikuwa beki wa kati
akiwa sambamba na Radebe. Erick Bakke na Lan Harte walikuwa na sifa moja
muhimu; mabingwa wa kupiga mipira ya adhabu au mipira iliyokufa.
Wengine ni Oliver Dacourt,Nigel Martin, Harry Kawell. Huyu Kewell alikuwa kasi na
‘ball control’ ya hali ya juu.

Ninakumbuka kasi yake ilivyowatoa jasho mabeki wa timu
pinzani. Ilikuwa burudani sana. Huyu Oliver Dacourt alikuwa Mfaransa, nywele kibao
kichwani halafu mkorofi fulani lakini mpira miguuni ilikuwa dhahabu tupu.
Katika nyakati za Alex Ferguson naamini alikuwa haipendi Leeds United sababu ya
upinzani wao katika Ligi Kuu. Mara nyingi walikuwa wakimtoa jasho.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Dar young africans

Ubovu Yanga, kwenye uongozi mpaka kwenye timu..

VAR ikitumika kwenye mechi ya Simba, Yanga

VAR ikitumika kwenye mechi ya Simba, Yanga