in , ,

NI WAPI MIKOBA YA WENGER ITABEBEKA VIZURI?

LEONARDO JARDIM

Miaka nenda miaka rudi kumekuwa na danadana nyingi kuhusu hatma ya Arsene Wenger kwenye timu ya Arsenal. Pale ambapo unaamini kuwa muda wa mfaransa huyo unaweza kuwa umefika mwisho ndipo mpira utapigwa kutoka mguu mmoja kwenda mwingine. Joto likizidi mzee atashinda mechi 7 kati ya 10 za Mwisho na kombe la FA na hatusikii tetesi zozote za yeye kuondoka.

Lakini ni kama vile maji yamemfika shingoni mara hii lakini bado anapiga miguu aweze kupona. Kama atashindwa kutwaa taji lolote msimu huu basi inaweza kuwapa matumaini makubwa walio wengi lakini endapo atatwaa Europa ligi basi sioni nini kikimzuia asiendelee kuwaongoza washika mitutu hao. Amebakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake isitoshe atakuwa pia ameirudisha timu hiyo klabu bingwa Ulaya unadhani ataondoka mtu hapo? Thubutu!

Lakini kwa kuwa kutakuwa na maisha baada ya Wenger siku fulani mimi na wewe tusioijua basi nitajaribu kuyaangazia majina kadhaa yaliyohusishwa na kwenda kukalia benchi la ufundi pale Emirates.

BRENDAN RODGERS.

Brendan Rodgers

Ni kocha anaefundisha soka zuri na la kuvutia na la pasi nyingi ambayo iko katika falsafa ya Arsenal na hili lilithibiti kipindi yuko Swansea City mpaka timu hiyo kufikia kupewa jina la utani la Swanselona. Alikuza CV yake zaidi pale Anfield na ametoka kutwaa ubingwa wa ligi ya Uskochi akiwa na Celtic. Kwa mtazamo wangu ligi ya Uskochi sio kipimo sahihi kwa mtu anaetakiwa kuja kuifanya timu kubwa pale Uingereza kuwa ni yenye ushindani wa mataji hasa la ligi. Aliwahi kupata nafasi hiyo Liverpool akashindwa na kiukweli bado sio mtu ambae unaweza kumtazama kama mbadala sahihi wa Wenger na akaweza kuifanya timu hiyo kuwa na ushindani wa mataji makubwa.

JOACHIM LOW.

Joachim Löw

Kocha bora kabisa wa timu ya taifa duniani kwa miaka takribani 4 iliopita. Kiukweli Low ameonesha uwezo mkubwa akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani na aliwashangaza wengi kwa kushiriki michuano ya Confederation na kikosi cha wachezaji wadogo mno. Na tofauti kabisa na matarajio ya wengi akaweza kutwaa taji hilo. Anapewa nafasi kubwa kabisa ya kufanya vizuri kwa mara nyingine tena mwaka huu. Ni kocha anaejua kupata kilicho bora kutoka kwa wachezaji wake na mbinu zake mahiri za kushambulia kwa kasi kubwa kutokea nyuma kwenda mbele kwenye eneo la mpito. Naamini huyu ni chaguo sahihi la kumrithi Wenger hasa ikizingatiwa kuwa ameshafanya makubwa kwenye ngazi ya kinataifa na ni wazi anahitaji changamoto mpya na klabu kama Arsenal inaweza kuwa kipimo sahihi cha ubora wake.

MIKEL ARTETA.

MIKEL ARTETA

Kwa sasa yuko kwenye benchi la ufundi la Manchester City akisaidiana na Pep Guardiola. Anajifunza mengi lakini bado sio mtu sahihi wa kukabidhiwa kukiongoza kikosi cha kwanza pale Arsenal. Hana uzoefu isitoshe presha ni kubwa sana kwa sasa pale Emirates na ni wazi anaweza akashindwa kufikia matarajio ya timu hiyo. Anahitaji kutafuta changamoto kwenye timu isiyo na presha ya makombe ili atengeneze jina ikisha pengine ndio anaweza kutafuta changamoto kubwa kama hii ya Arsenal.

LEONARDO JARDIM.

LEONARDO JARDIM

Huyu ni kocha wa AS Monaco. Ametoka kutwaa taji la Ligue 1 msimu uliopita akikomesha utawala wa PSG na akiweza pia kufika nusu fainali ya klabu bingwa Ulaya. Bado hata hivyo simwoni kama mtu sahihi wa kuichukua mikoba ya Wenger. Arsenal inahitaji mtu mzoefu ambae mbinu na uwezo wake wa kufundisha timu kubwa na kwenye mazingira ya presha imeshathibitika. Kocha mwenye jina pia na CV kubwa kwa maana ya kufundisha timu kadhaa kubwa.

Thierry Henry nae anahusishwa lakini bado anahitaji kutafuta changamoto sehemu nyingine kabla ya kufikia kuchukua majukumu pale Arsenal. Lakini kwa mtazamo wangu Arsenal wanaweza kuwa wamefanya jambo la maana kabisa ikiwa wataweza kumnasa Antonio Conte ambaye yuko kitimoto pale Chelsea. Lakini hata Jose Enrique na mtu kama Carlo Ancelloti wanaweza kuwa machaguo mazuri pia. Arsenal inahitaji mtu mwenye uzoefu baada ya Wenger sio mtu anaejifunza kunyoa maana na mtu ambae ama hajafundisha timu nyingi kubwa au kufundisha ligi zenye ushindani mkubwa.

Report

Written by haatimabdul

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KILICHOWATOA PSG KLABU BINGWA ULAYA

Tanzania Sports

KWANINI MANCHESTER CITY NI BORA SANA MSIMU HUU?