in , ,

NI MARA CHACHE KUSHUHUDIA USIKU USIO NA GIZA KAMA USIKU WA NOU CAMP

Miujiza huonekana kitu cha kawaida pindi ambapo haijatendeka, ukubwa
wa miujiza huonekana pale tu inapotendeka.

Ndipo hapo mwanadamu yoyote huwa anaamini chochote kinawezekana chini
ya jua pindi tu pale anaposhuhudia muujiza husika.

Huamini hata sehemu ambayo huonekana ngumu kwa macho ya nyama ya
wanadamu wengi, kwake yeye kukatiza juu ya maji ya bahari huku
akitembea huonekana kama ni jambo la kawaida machoni pake na hii ni
Kwa sababu nyuma aliwahi kushuhudia muujiza uliompa nguvu na kuamini
kuwa kitu chochote kinawezekana katika dunia.

Lakini muujiza ni vigumu kutendeka bila ya mtu kutembea na imani ndani yake.

Imani humpa mtu kufanya muujiza wowote duniani.

Hata kuna jambo lolote gumu analolipitia maishani mwake hutembea na
imani ya kulishinda kwa sababu ana imani kupitia muujiza ndipo hapo
nguvu yake ya kupigana huongezeka maradafu.

Ndicho kilichotokea kwa Barcelona ni mara chache sana katika dunia hii
kukutana na usiku kama ule usiku wa Nou Camp.

Usiku wenye nuru angavu inayoficha giza kwa pamoja, usiku ambao jua,
nyota na mbalamwezi huwaka na kung’aa kwa wakati mmoja.

Historia ilikuwa inawahukumu kwa kiasi kikubwa Barcelona kwa sababu
haijawahi kutokea timu yoyote ile kupindua matokeo ya 4-0, ila wao
walizidi kutuaminisha zaidi kuwa mwanamke alikuja duniani kuzaa na
historia mara nyingi zipo kwa ajili ya kuvunjwa.

Imani kubwa ilikuwa ndani ya wachezaji wa Barcelona ndiyo maana hata
kabla ya mchezo Neymar alinukuliwa akisema wana asilimia 1% moja ya
kupita, ila wana 99% ya imani kuwa watapita, Luis Enrique
aliwaaminisha watu kabla ya mchezo kikosi chake kinaweza pindua
matokeo.

Hawakuwa mashujaa mdomoni pekee, ushajaa wao ulijidhirisha uwanjani.
Neymar akawa Daudi akahusika kuongoza majeshi yake kumpindua Sauli,
mfalme ambaye alikuwa anajivunia utajiri wake aliotoka nao mjini Paris
kuja kuuoneshea umwamba mjini Barcelona.

Pamoja na kwamba Suarez, Messi na Neymar walihusika kwenye magoli
lakini Neymar ndiye aliyekuwaa taa iliyokuwa inang’aa kupita taa zote
za mlima Sinai.

Kitu kilichowabeba PSG na kilichowaangusha Barcelona Katika mchezo wa
kwanza ndicho hicho hicho kilichoibeba Barcelona na kuiangusha PSG
katika mchezo wa pili.

Ubora wa kiungo cha PSG kiliufanya ubora wa kiungo cha Barcelona
usionekane kule Paris, lakini hali ilikuwa tofauti mjini Barcelona.
Sergio alilinda beki zake ipasavyo. Iniesta akatengeza nafasi nyingi
sana na Rakitic akaleta uwiano wa kulinda na kushambulia hali
iliyowafanya viungo wa PSG kutokuwa wenye ubora.

Inawezekana lilikuwa wazo zuri kwa PSG kuweka watu kumi nyuma ya mpira
na kujilinda na hii ni Kutokana na faida ya magoli manne waliyokuwa
nayo lakini aina yao ya kujilinda haikuwa salama.

Kwanza mabeki wote wa pembeni hawakuwa na kasi ukilinganisha na kasi
ya Wachezaji wa pembeni wa Barcelona yani Neymar na Rafinha.

Marking mbovu za mabeki wa kati wa PSG pia zilikuwa mbovu.Ile hali ya
wao kujilinda kwa muda mrefu kulisababisha presha kubwa ndani yao, na
siku zote ukiruhusu presha ndani ya timu husababisha Wachezaji kuwa na
makosa mengi hii ni kutokana na umakini kupungua unaposhambuliwa kadri
muda unavyoenda.

Cavan tayari ameshakuwa mkubwa tena jiwe linatomaniwa na kila Fundi
mwashi lakini ndivyo hivo timu yake ilicheza kitoto na kusahahu ukubwa
wake aliokuwa nao ndani ya uwanja.

Barcelona hawakuwaruhusu PSG kukaa na mpira hata kwa sekunde
thelathini kama wao walivyofanyiwa kule Paris ndiyo maana sikumbuki
hata kama Verrati na Rabiot kama walikuwepo.

Pamoja na kwamba Barcelona walishinda ila wanatakiwa waingie sokoni
kutafuta beki wa kulia. Tangia kuondoka kwa Dani Alves kumekuwa na
pengo kubwa sana ambalo Alex Vidal na Sergio Roberto hawajaliziba

Jana walitumia mfumo wa mabeki watatu kuliziba na Rafinha kumchezesha
kama Right Wing Back. Pengo halikuonekana Kwa kiasi kikubwa kwa sababu
Barcelona muda wote walikuwa wanashambulia hivo huwezi ona madhaifu ya
mabeki katika hali hii na pili Ubora wa Barcelona ulikuwa unaanzia
katikati na mipira mingi ilichezwa katikati kwenda mbele.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ARSENE WENGER AAMBIWA:

Tanzania Sports

YA GAMBIA YALIKUWA FUNZO LA KWENDA GABON NA INDIA.