Rais aliyeliongoza Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa miaka 16, Sepp Blatter amechaguliwa tena kuliongoza kwa muhula wa tano.

Blatter alichaguliwa kwenye uchaguzi uliofanyika chini ya uvuli wa kukamatwa kwa maofisa saba waandamizi wa shirikisho hilo, wakituhumiwa na makosa ya rushwa na utakatishaji fedha.

Mpinzani wa Blatter, Prince Ali bin al-Hussein wa Jordan alifanikiwa kumnyima kura za kutosha kwenye raundi ya kwanza hivyo ikapangwa raundi ya pili ifanyike, lakini mwana huyo wa mfalme akajitoa.

Blatter (79) alisimama kuashiria ushindi wake, akasema yeye ni nahodha hodari ambaye anaweza kuiondoa Fifa kwenye dimbwi la tuhuma za rushwa zinazoikabili.

Mswisi huyo amechaguliwa licha ya kupigwa na wadau mbalimbali, wakiwamo wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) ambao bosi wao, Michel Platini alimtaka Blatter ang’oke.

Hata hivyo matakwa hayo hayakutimizwa, kwa kile Blatter alichodai kwamba alikuwa amechelewa mno, laiti maombi yangetolewa siku au wiki kadhaa kabla.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, naye akiwa jijini Berlin, Ujerumani alisema ilikuwa tamaa yake kwamba Blatter aondoke mapema iwezekanavyo.

Hata hivyo, Blatter amekuwa akipata uungwaji mkono mkubwa kutoka mashirikisho ya soka ya Afrika na Asia, kwa kile yanachoeleza kwamba ameendeleza soka kwao.

“Mie si mkamilifu, hakuna aliye kamili lakini tutafanya kazi nzuri kwa pamoja, nina uhakika huo. Nalibeba jukumu la kuirejesha Fifa pale inapotakiwa kuwa … twende Fifa! Twende Fifa!” akasema akifurahia ushindi.

Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) likisubiri maofisa hao wa Fifa wapelekwe Marekani kuunganishwa na wengine saba wasio wa Fifa ili wafikishwe mahakamani.

Uswisi imeanzisha uchunguzi juu ya mchakato wa kupata uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022, zilizopangwa kufanyika Urusi na Qatar.

Hata hivyo Urusi imempongeza Blatter kwa ushindi wake, ikiwa ni dalili wazi kwamba inalenga kuendeleza uhasama baina yake na Marekani.
Maofisa waliokamatwa ni Jeffrey Webb, Eugenio Figueredo (wote makamu wenyeviti wa Fifa), Eduardo Li, Rafael Esquivel, Jose Maria Marin, Costas Takkas na Julio Rocha – na wote wapo rumande jijini Zurich.

Watakuwa na fursa ya kukata rufaa juu ya kuwekwa kwao rumande ifikapo Juni 8, lakini mamlaka za Uswisi zimesema si rahisi wapewe dhamana.

Kumekuwa na habari kwamba Blatter amekuwa akikwepa kusafiri kuingia Marekani akihofia uwezekano wa kudakwa kwa sababu tangu miaka mitatu iliyopita Fifa imekuwa ikichunguzwa na mamlaka za huko.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

TETESI ZA USAJILI LEO

FAINALI KOMBE LA FA: