in , , ,

NGUVU ZINA WAKATI MARIO

Juzi Inter Milan wamegomea ofa ya Liverpool kutaka kumsajili Mateo Kovacic huku wakiwapa Mario Balotelli kama nyongeza kwenye mkataba huo. Balotelli amekuwa mchezaji wa nyongeza. Cha ajabu zaidi hata kocha wake mlezi Roberto Mancini anakataa kumrudisha Inter Milan. Balotellli alitesa kwenye soka siku za nyuma.

Pamoja na ukosefu wa nidhamu na utukutu wake alivumiliwa na Manchini na Mourinho na akawa mmoja kati ya wachezaji waliotegemewa kwenye vikosi vya makocha hao. Wakati Jose Mourinho akiwa Inter alikuwa akikerwa sana na tabia za Balotelli. Aliwahi kumsimamisha kujihusisha na kikosi cha Inter Milan kutokana na utovu wa nidhamu.

Bado baadae akawa anampa Mario nafasi ya kucheza ingawa kulikuwa na washambuliaji wazuri kama Samuel Eto’o na Diego Milito wakati huo Inter Milan. Hii inaonyeha ni kiasi gani Mourinho alitambua uwezo wa Mario Balotelli ambaye alikuwa kijana mdogo wa chini ya miaka 20.

Kocha wake mlezi Roberto Mancini pia alitambua uwezo wa Mario. Alipohamia Manchester City 2010 aliiona kila sababu ya kumvuta mshambuliaji huyo Etihad. Alikuwa tayari kuvumilia matukio yoyote ya utovu wa nidhamu ambayo Balotelli angeyafanya wakiwa pamoja Etihad.

Wakati fulani Mancini aliwahi kusema, “Tatizo ni sababu ya umri wake, anaweza kufanya makosa fulani. Huyo ni Mario. Yeye ni mwehu. Ila nampenda kwa kuwa ni kijana mzuri”. Hizo zilikuwa ni nyakati za furaha mno kwenye maisha ya soka kwa Mario Balotelli. Nyakati ambazo makocha waliweka pembeni kasoro zake zisizovumilika na kumtumia kwenye vikosi vyao.

Kiwango cha Balotelli kiliwahi kumvutia pia kocha wa timu ya taifa ya Ghana wakati huo Claude Le Roy ambaye Agosti 2007 siku chache kabla ya Balotelli kutimiza miaka 17 alimwita mchezaji huyo aichezee timu ya taifa ya Ghana.

Balotelli alikataa akisema kuwa alikuwa akisubiri nafasi ya kuichezea timu ya taifa ya Italia wakati utakapofika. Novemba 2008 akiwa na umri wa miaka 18 aliifungia Inter Milan bao lake la kwanza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Anorthosis Famagusta ya Cyprus na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuifungia bao Inter kwenye michuano hiyo.

Alikuwa akitabiriwa kuwa angekuja kuwa mchezaji tishio siku za usoni. Mancini aliwahi kusema kuwa kwa kuwa alikuwa na umri mdogo kulikuwa na nafasi kubwa ya mchezaji huyo kuendelea kuwa bora zaidi. Disemba 2010 Balotelli alishinda tuzo ya “Golden Boy” inayotolewa kila mwaka na waandishi wa habari za michezo kwa mwanasoka wa Ulaya mwenye umri chini ya miaka 21 aliyefanya vizuri zaidi.

Aliposhinda tuzo hiyo Balotelli alitamba kuwa kati ya waliowahi kushinda tuzo hiyo ni mmoja tu aliyemzidi kidogo kiwango ambaye ni Lionel Messi. Alimaanisha kuwa kati ya washindi wa nyuma kama Rafael van der Vaart, Wayne Rooney na Sergio Aguero hakuna aliyegusa kiwango chake. Nyakati za furaha zilimpa jeuri Mario.

Ubora wa Mario ulidhihirika zaidi pale alipoitwa kuiwakilisha Italia kwenye michuano ya Uefa Euro 2012. Akawa mchezaji wa kwanza mweusi kuiwakilisha timu ya taifa ya Italia kwenye michuano mikubwa. Akaonyesha kiwango safi kwenye michuano hiyo hasa kwenye mchezo wa nusu fainali alipoitungua Ujerumani mabao mawili maridadi na kuipeleka Italia fainali.

Hizo zilikuwa nyakati za dhahabu kwa Mario. Kwa sasa hazipo tena. Mario hana nguvu tena ya kutamba kwa sasa kwenye ulimwengu wa soka kiasi ambacho hata kocha wake mlezi Roberto Mancini anagoma kumrudisha Mario Inter Milan kwa kisingizio cha utovu wa nidhamu. Nguvu zina wakati Mario.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Man U wamtaka Ronaldo

MAN UNITED WAWAFUNGA BARCA