in ,

Natamani hadithi ya Zidane ifunikwe na jalada la Ole Gunnar Solskjær

Natamani hadithi ya Zidane ifunikwe na jalada la Ole Gunnar Solskjær

Tunaendelea kuhesabu hatua za kwenda mbele, ndizo hatua ambazo ni bora zaidi kwenye maisha kwa sababu ndizo hatua ambazo hutuwezesha kufikia kesho yetu.

Hapa ndipo ubora na umuhimu wa hatua za kwenda mbele unapoanzia. Na hapa ndipo kila kitu bora kinapoanzia. Hakuna siku ambayo kitu bora kilianzia kwa hatua za kurudi nyuma.

Hakuna atakayekusifu hata siku moja kipindi ambacho utakapoamua kutembea kwa kurudi nyuma. Na dunia itakushangaa sana.

Na kuna wakati mwingine dunia itakukataa kabisa na haitokuwa tayari kuwa na wewe kwenye safari ya maisha. Ndiyo maana watu wenye uchungu wa mafanikio hawaogopi kabisa kumwacha mtu ambaye hutamani kutembea kwa kurudi nyuma.

Sababu moja tu ambayo huimba vichwani mwa watu wengi, nayo ni mafanikio. Huu ndiyo wimbo ambao unawafanya wengi kufikiria kuwaza kwenda mbele.

Huu ndiyo wimbo ambao huwafanya wengi wenye uchu wa mafanikio kuwaacha wale ambao huonekana hawako tayari kukimbia kwenda mbele.

Ndiyo maana siyo jambo la ajabu kushuhudia watu wakifukuzwa kazi kwa ustawi wa mafanikio ya taasisi husika. Taasisi ni kitu cha muhimu sana.

Manchester United waliachana na Jose Mourinho kwa sababu tu ya afya ya taasisi yao. Waliona yeye hatokuwa na uwezo mkubwa wa kutibu afya ya taasisi yao.

Hawakujaribu kuwaza jinsi ambavyo aliwahi kuwa na mafanikio makubwa katika timu mbalimbali ambazo aliwahi kupitia.

Hawakuwaza mafanikio aliyokuwa ameyapata Chelsea, hawakujaribu hata kidogo kuwaza kuhusu mazingaombwe aliyoyafanya akiwa FC Porto.

Wao walichokuwa wamekifikiria ni mafanikio ya mbele tu. Walifikiria namna ya kuinua mguu wao na kupiga hatua kuelekea mbele.

Walihitaji mtu ambaye angewaongoza wachezaji waweze kuipigania Manchester United.

Ilihitajika Manchester United yenye njaa, Manchester United ambayo ilikuwa fahari ya England. Manchester United ambayo ilikuwa nembo kubwa ya mafanikio duniani.

Kitu ambacho Jose Mourinho alionekana kushindwa. Hakuwa na uwezo tena wa kuitengeneza Manchester United iwe ya kuogofya.

Ilionekana Manchester United ya kawaida sana. Manchester United ambayo hata timu ndogo zilikuwa na uwezo wa kwenda Old Trafford na kuchukua alama tatu bila usumbufu wowote.

Kwenye mikono yake alikuwa na Manchester United ambayo ilikuwa inatumia muda mwingi ikijilinda kuliko kushambulia, na kuna wakati ilikuwa inajilinda dhidi ya timu ndogo.

Utamaduni huu haukuwepo awali, Jose Mourinho alikuwa anajaribu kuitengeneza Manchester United ambayo haikuwa kutokea.

Manchester United ambayo ilikuwa haina mvuto wowote kuanzia ndani na nje ya uwanja. Ndipo hapo walipoamua kumleta Ole Gunnar.

Mchezaji ambaye sifa kubwa alizipata kama SUPER SUB wakati anacheza. Rasmi ma boss wa Manchester United waliamua kumfanya Super sub tena kipindi hiki akiwa kocha wa muda.

Hadithi ambayo inafanana sana na hadithi ya Zinedine Zidane na Real Madrid yake. Klabu ambayo aliitumikia kwa kiwango kikubwa akiwa mchezaji.

Walimwamini kuwa kocha wa muda kuchukua nafasi ya Rafael Benitez na kilichotokea baada ya hapo kilikuwa historia. Makombe 9 ndani ya misimu miwili.

Yote haya aliyafanikisha kwa sababu tu alikuwa anajua utamaduni wa Realmadrid. Alijua Real Madrid wanataka nini.

Alijua upi utamaduni wa Realmadrid na akaweza kuiongoza timu katika mstari sahihi wa Real Madrid.

Hiki ndicho kitu ambacho Manchester United wanakihitaji kwa sasa. Miaka mingi imepita baada ya Sir Alex Ferguson kuondoka. Na kila aliyekuwa anakuja alikuwa mtu ambaye hajui utamaduni wa Manchester United.

Ole Gunnar anajua vyema utamaduni wao, anajua ni kipi ambacho Manchester United wanataka. Na ndiyo maana naona hadithi ya Realmadrid na Zidane inaweza ikawa sawa kwa ndani ile nje ya kitabu jalada likawa limeandikwa Sir. Ole Gunnar na Manchester United.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Makocha wanaofaa kuchukua nafasi ya JOSE MOURINHO

Tanzania Sports

Man United bado wana nafasi ya nne bora