in , , ,

Nani zaidi: Clattenburg au Chelsea?

*Wachezaji Chelsea wajiandaa kutoa ushahidi

*Mwamuzi Clattenburg amewasilisha ripoti nzito

 

Mwamuzi Mark Clattenburg aliyechezesha mechi kati ya Chelsea na Manchester United amewasilisha ripoti inayogusia tukio la ajabu mchezoni.
Mwamuzi huyo anayedaiwa kuwanyonga Chelsea, analalamikiwa kuwa mbaguzi, lakini zipo taarifa kwamba ripoti yake inayo mengi ya kuvuta hisia.
Clattenburg aliyewaonyesha kadi nyekundu Branislav Ivanovic na Fernando Torres kabla ya kukubali goli lililodaiwa kuwa la kuotea la Javier Hernandez ‘Chicharito’, alikwaruzana pia na John Obi Mikel.
Ni kwa Mnigeria huyo, mwamuzi Clattenburg anadaiwa kutoa lugha isiyofaa ya ubaguzi wa rangi na pia kumdhihaki nyota mwingine wa Chelsea, Juan Mata.
 Chama cha Soka cha England (FA) kimeanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo, ambapo licha ya kutegemea kwa kiasi kikubwa waamuzi wasaidizi, kinadaiwa kuomba ushahidi wa video kutoka Sky Sports.
Pamoja na kwamba bado malalamiko rasmi yaliyofunguliwa na Chelsea ni tuhuma tu, waamuzi wa zamani wanasema ikiwa kweli alifanya makosa hayo, huu utakuwa mwisho wa kazi ya Clattenburg.
Tayari ameenguliwa kwenye orodha ya waamuzi wanaochezesha mechi mwishoni mwa wiki hii, na anadaiwa kurejea moja ya matukio ya ajabu katika ripoti yake ya mechi ya Jumapili, ambapo United waliwafunga Chelsea 3-2.
Tukio analorejea Clattenburg katika mechi hiyo halijaelezwa hasa ni lipi, lakini ni kati ya yale ambayo waamuzi huyajumuisha pale wanapotaka FA iingilie kati.
Yawezekana polisi wakahusishwa pia, baada ya mwanasheria wa umoja unaolegalega wa wanasoka weusi, Peter Herbert kuandika malalamiko kwa Polisi wa Jiji la London.
Ofisa Mtenadaji Mkuu wa Chelsea, Ron Gourlay, Mikel na kocha Roberto Di Matteo, kwa pamoja walitaka Clattenburg awaombe radhi walipingia kwenye vyumba vya waamuzi Stamford Bridge. Clattenburg  aliwakatalia, ndipo Chelsea wakakutana na kuamua kuwasilisha malalamiko rasmi, ambayo huenda yatakata mzizi wa fitina kwa kuanika kilichojiri na yupi ni mkosaji.
Obi anadai kutolewa lugha hiyo ya kibaguzi baada ya kuonyeshwa kadi ya njano katika dakika ya 76 ya mchezo.
Taarifa zaidi zinaonesha kwamba kuna mchezaji wa Hispania wa Chelsea anayehusishwa na sakata na mwamuzi huyo, akidai kwamba alitukanwa. Wahispania waliocheza dhidi ya United ni Torres, Juan Mata na Cesar Azpilicueta.
Sky Sports wanaweza kusaidia uchunguzi, kwa kutoa sehemu ya mikanda yao kutokana na kamera 20 zinazotegeshwa kwenye mechi kubwa kunasa matukio.
Hata hivyo, waamuzi wasaidizi watategemewa kueleza wanachokumbuka au watakachoamua kusema, kwa vile vinasa na vipaza sauti wanavyotumia muda wote wa mechi havirekodiwi.
Waamuzi wasaidizi walikuwa Michael McDonough na Simon Long waliokuwa kwenye mistari ya pembeni na mwamuzi wa akiba alikuwa Michael Jones, ambaye pia husikia kila mwamuzi wa kati anachosema.
Madai ya ubaguzi wa rangi yanakuja wakati nahodha wa Chelsea, John Terry akitumikia adhabu ya kukosa mechi nne na ameshalipa pauni 220,000 kwa makosa ya kumtolea lugha isiyofaa Anton Ferdinand wa Queen Park Rangers (QPR) mwaka mmoja uliopita.
Ikiwa kweli Clattenburg alitoa maneno ya kibaguzi, soka ya England itakuwa imeingia doa kubwa, ikiwa ni wiki moja tu baada ya baadhi ya wachezaji weusi kugomea kampeni ya kuvaa fulana kupinga ubaguzi wa rangi, kwa vile hawaoni hatua za dhati dhidi ya wabaguzi.
FA ilichosema tu ni kwamba imeanza uchunguzi na haina maoni yoyote kwa sasa kuhusu mchezo huo wa Jumapili, ambao ulikuwa wa kwanza kwa United kushinda Stamford Bridge katika miaka 10.
Hali bado ni tete, kwa sababu wababe hao wawili wa soka wanakutana tena Jumatano hii hapo hapo Stamford Bridge katika mchezo wa kombe la ligi – Capital One Cup.
Jumapili ilibidi makocha Alex Ferguson na Roberto Di Matteo watenganishwe na maofisa, baada ya Di Matteo kudai kwamba timu yake haitendewi haki.
Ferguson aliridhia matukio ya kadi zote nyekundu na kufurahia magoli, lakini alipata kumlalamikia mwamuzi huyu huyu kwa wingi wa kadi anazotoa.
Wachezaji wa Chelsea wanadaiwa kuwa tayari kutoa taarifa za maandishi kuhusu kuunga mkono malalamiko yao, lakini iwapo yatabainika si ya kweli, yanaweza kushusha hadhi yao na ya klabu kwa kiasi kikubwa.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Chelsea wavunjiwa daraja lao

Zanzibar National Beach Volleyball Championship ends