in ,

Nani bora kati ya AJIBU na MIQUISSONE

Akili yangu bado inatafakari kwenye hili swali, sitaki kabisa kutoa jibu kwa haraka haraka kwa sababu kuna kitu bado nakisubiria kwa Ibrahim Ajib.

Kwa sasa hana kwenye moyo wake ila nina amini kesho atakipata, naisubiri sana hiyo kesho, kesho ambayo italeta ukamilifu wa kipaji cha Ibrahim Ajib.

Kipaji ambacho Mungu aliamua kukitoa ulaya na kukileta kwenye miguu ya Mtanzania Lakini kwa bahati mbaya Mungu alisahau kitu kimoja tu huko ulaya.

Ibrahim Ajib ana miguu ya ulaya na moyo wenye macho ya Kitanzania. Miguu yake haipo kwa wachezaji wengi wa Tanzania Lakini moyo wake unafanana na mioyo ya wachezaji wengi wa Tanzania.

Mioyo isiyokuwa na njaa ya mafanikio, mioyo iliyoridhika kukaa sehemu ambayo siyo sehemu kubwa kulingana na ukubwa wa kipaji Lakini kwake yeye kama mkono unapata nguvu ya kufika kinywani haya ndiyo mafanikio makubwa sana kwake.

Watanzania wengi wanatamani Ibrahim Ajib asogee kwenda mbele Lakini yeye anatamani kuendelea kuwepo sehemu ile ile aliyopo. Kwake yeye sehemu aliyopo ni sehemu bora zaidi kuliko huko mbele tunakotamani sisi.

Ana kipaji cha mafanikio, hana moyo wa mafanikio. Hana njaa, macho yake yanaishia uwanja wa Taifa tu pale Chang’ombe.

Uwanja ambao kwake yeye ndiyo faraja kucheza. Leo hii uwanja huu umevamiwa na mmakonde kutoka Msumbiji, mtu ambaye ana mguu wa almasi na moyo wa dhahabu.

Miguu yake inang’aa kila ikishika mpira, moyo wake una njaa haswaa. Unatamani ufike sehemu ambayo maisha yake ya mpira wa miguu yatakuwa na thamani kubwa kama Dhahabu.

Hiki ndicho ambacho Ibrahim Ajib hana kwa sasa na ndicho kitu ambacho natamani akipate kesho, moyo wenye njaa, Hana njaa ya mafanikio.

Hii ni tofauti sana na kwa Luiz Miquissone ambaye ana moyo wenye njaa sana. Inawezekana kabisa wote wanavipaji vikubwa Lakini kinachowatofautisha ni mioyo. Kuna mmoja ana moyo wenye njaa na mwingine hana moyo wenye njaa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

VAR ina maswali kuliko majibu

Tanzania Sports

Mo Farah matatani